Simba wakishikilia msimamo wao, Bodi ya Ligi itaweza kuwapoka alama 15?

Kanuni ya 31 ya Ligi Kuu msimu wa 2024/25 yenye vipengele saba na vidogo viwili, inasema: Timu yoyote itakayokosa kufika uwanjani bila sababu za msingi zinazokubalika na TFF/TPLB, na/au kusababisha mchezo usifanye itakabiliwa na adhabu zifuatazo:

1.1. Kutozwa faini ya shilingi milioni tano (5,000,000/=) ambapo milioni mbili na laki tano (2,500,000/=) itachukuliwa na Bodi ya Ligi Kuu, na shilingi milioni mbili na laki tano (2,500,000) itachukuliwa na timu pinzani.

1.2. Kulipa fidia ya maandalizi/uharibifu wowote unaoweza kujitokeza.

1.3. Kupokwa alama 15 (kumi na tano) katika msimamo wa ligi, na viongozi wa jambo hilo watachukuliwa hatua zaidi za kinidhamu.

Kanuni inaendelea huko mbele na kutaja adhabu nyingine nyingi.

Hii ina maana kwamba endapo Simba itasimamia tamko lake kwamba haichezi mechi yake dhidi ya Yanga, na sababu zake zisipokubalika kwa TFF na Bodi ya Ligi, basi inaweza kukutana na adhabu hizo.

Lakini swali ni je, wasimamizi wa mpira wetu, TFF na Bodi ya Ligi, wanaweza kusimamia kanuni hizi?

Uzoefu unaonyesha kwamba Yanga na Simba huwa haziguswi pale zinapofanya kosa kubwa ambalo hukumu yake italeta mtikisiko kwao.

Kesi wanazohukumiwa nazo ni hizi ndogo ndogo zenye adhabu rahisi.

Lakini adhabu kama ya kanuni hii ya sasa kwamba Simba ipokwe alama 15, haijawahi kutokea.

Nitatumia kisa cha Yanga mwaka 2003 kama mfano.

Mwaka 2003 klabu ya Yanga chini ya uongozi wa mwenyekiti Francis Kifukwe na katibu mkuu Jamal Malinzi, ilifungua kesi mahakama ya Ilala kwa hakimu mkazi Agatha Kabuta.

Yanga walifungua kesi hii kupinga mabadiliko ya mfumo wa uchezaji wa ligi ya Muungano.

Ligi ya Muungano ndiyo iliyokuwa Ligi Kuu ya Tanzania kuanzia 1982 hadi 2003 ilipovunjika.

Ligi hii ilishirikisha timu za Bara na Visiwani, na ndiyo iliyotoa wawakilishi wa Tanzania kwenye mashindano ya Afrika.

Bingwa wa ligi hii ndiyo alitambuliwa na CAF na FIFA kuwa bingwa rasmi wa Tanzania na ndiye aliyeshiriki mashindano ya Klabu Bingwa Afrika.

Mshindi wa pili alishiriki mashindano ya Kombe la CAF, na mshindi wa tatu alishiriki Kombe la Washindi, katika miaka ambayo hakukuwa na Kombe la Nyerere (ambalo sasa ni CRDB).

Mwaka 2003 Ligi ya Muungano ilipangwa kuchezwa kwa mtoano, mfumo ambao mara ya mwisho ulifanyika mwaka 1992.

Yanga ilipangwa kucheza dhidi ya Jamhuri ya Pemba, kwenye Uwanja wa Gombani.

Wakatoka Dar es Salaam kwenda Pemba kupitia Unguja, lakini wakiwa hapo wakatoa taarifa kwamba hawataenda Pemba kwa sababu hawataki kucheza ligi ya mtoano.

Aliyetamka maneno haya alikuwa Jamal Malinzi, ambaye miaka 10 baadaye akawa Rais wa TFF.

Waandaaji wa mashindano hayo, FAT na ZFA (sasa ni TFF na ZFF) wakaipa Jamhuri ushindi wa mezani.

Yanga wakaenda mahakamani kufungua kesi kupinga hilo.

Kitendo cha Yanga kwenda mahakamani kilikuwa ukiukwaji wa sheria za mpira na adhabu yake ilikuwa kufutwa.

Sakata la Yanga lilifanana na lile la klabu ya Sigara ya Temeke Dar es Salaam.

Mwaka 1997 walimsajili kipa Peter Manyika kutoka Mtibwa Sugar ambayo ilikuwa inacheza Ligi Kuu kwa mara ya kwanza baada ya kupanda daraja mwaka 1996.

Lakini usajili wa Manyika ukaonekana na shida nyingi na Sigara wakapokwa alama zote walizopata wakiwa na Peter Manyika.

Hiyo ikawafanya washuke daraja na wakapanga kwenda mahakamani.

Wakati huo timu ilikuwa chini ya Azim Dewji.

Lakini Katibu Mkuu wa FAT, Ismail Aden Rage, aliwapa onyo kali kwamba wakienda mahakamani atawafuta kabisa kwa miongozo ya FIFA inayokataza timu za mpira kufungua kesi kwenye mahakama za kawaida.

Sigara wakaogopa kwenda mahakamani, na Azim Dewji akaitelekeza timu.

Lakini mwaka 2003 Yanga walienda mahakamani ila FAT ilishindwa kuichukulia Yanga hatua yoyote.

Je, safari hii TFF itakuwa na jeuri ya kuipoka Simba alama 15 kwa kutopeleka timu uwanjani, au watatafuta adhabu rahisi…au sababu zitaeleweka?

Related Posts