Dar es Salaam. Tunapoadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, kuna haja ya kutambua na kusherehekea mchango wa wanawake nchini katika kukuza uchumi wa familia na jamii kwa ujumla.
Licha ya changamoto wanazokabiliana nazo, bado wamekuwa nguzo katika ustawi wa familia kupitia shughuli za kiuchumi, hasa kwa kutumia vikundi vya kijamii vya kuweka na kukopa (Vicoba).
Kupitia Vicoba, wanawake wengi wa kipato cha chini na cha kati wamekuwa wakipata fedha za kuanzisha na kuimarisha biashara ndogo ndogo, kugharimia elimu ya watoto na kuboresha hali ya maisha kwa ujumla.
Kwa kutumia fedha za mikopo, wanaweke wamekuwa wakianzisha biashara kama za kuuza mboga, vyakula, nguo na bidhaa nyingine, hivyo kuongeza kipato cha familia.
Kutokana na mafunzo yanayotolewa kupitia Vicoba, wanawake hujifunza kuhusu uwekaji akiba, kupanga bajeti na kutumia fedha kwa uangalifu, hivyo kujua mbinu za ujasiriamali.
Wanawake wameweza kujenga mtandao wa kijamii wa kusaidiana, kubadilishana mawazo na kuhamasishana katika safari ya kujikwamua kiuchumi.
Nyamlawa Mkima, mkazi wa Kinondoni, Dar es Salaam, ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya Mashuka Quality, akizungumza na Mwananchi, anashuhudia matunda aliyovuna kupitia Vicoba tangu alipojiunga mwaka 2022, akiwekeza fedha kidogo kidogo.
Anasema alipokopa, alianza na Sh4 milioni zilizomwezesha kununua bidhaa kwa ajili ya duka lake.
“Vicoba vimeniwezesha kupiga hatua hadi hapa nilipo baada ya kushikwa mkono na ndugu zangu walionipa ushauri wa kujiwekea akiba ambayo itanipa faida,” anaeleza.
Anasema baada ya kukua kiuchumi kutokana na elimu aliyopata kutoka kwa wataalamu wa fedha na kuhudhuria semina kadhaa kuhusu masuala ya fedha, aliongeza kiwango cha mkopo.
Nyamlawa anasema sasa anaweza kukopa hadi Sh10 milioni. Anasema mwaka 2024 aliagiza mzigo kutoka nchini China kwa mara ya kwanza kwa gharama ya Sh13 milioni.
“Ninapoangalia haya ninayofanya, najikuta nahamasisha wengine kujiunga kwenye Vicoba kwani naamini katika uwekezaji mtu anaweza ‘kutoka’ kimaisha bila kumtegemea mtu au mikopo ya benki,” anasema.
Anasema mbali na kuongeza wigo wa biashara, amekuwa mstari wa mbele kusaidia familia yake kupitia biashara anayofanya.
Anaeleza Vicoba ni sehemu ya kumkutanisha na watu mbalimbali wanaojumuika pamoja kwenye matukio ya kijamii.
“Vicoba si tu chanzo cha fedha bali pia jukwaa la kijamii ambako wanawake wanabadilishana mawazo, kusaidiana na kujifunza ujasiriamali,” anasema.
Kwa upande wake, Salha Salum, mkazi wa Kigamboni mkoani Dar es Salaam, anayemiliki duka la mapambo ya nyumbani, anasema amekuwa msaada kwa familia yake kutokana na Vicoba.
Anasema ni kutokana na harakati zake kupitia vikundi hivyo ameweza kumjengea mama yake nyumba eneo la Kigamboni.
Anaeleza kupitia Vicoba alipata fedha za matibabu alipotetereka kiafya. Pia, vimekuwa msaada kwa kipindi cha Januari ambacho kumekuwa na matukio mbalimbali, ikiwemo ulipaji wa ada na ununuzi wa sare za shule.
Mwalimu wa Vicoba kutoka jumuiya ya kukuza uchumi Ilala (Jukuila), Zaina Mahimbo anasema wamekuwa wakihimiza wanachama kuweka akiba kidogo kidogo ili hatimaye wajikwamue kiuchumi.
“Kupitia mafunzo, wanawake wanajifunza umuhimu wa kuweka akiba kwa malengo maalumu kama vile biashara, elimu ya watoto au dharura za kifamilia,” anasema.
Anasema wanachama hupewa mwongozo wa jinsi ya kukopa kwa busara, kutumia mikopo kwa njia sahihi na kuhesabu faida.
Mafunzo hayo huwasaidia kuepuka madeni yasiyolipika na kutumia fedha walizokopa kwa maendeleo, badala ya matumizi yasiyo ya lazima.
Mahimbo anasema wamekuwa wakihimiza vikundi kusajiliwa rasmi na Serikali ili kupata faida kama vile ulinzi wa kisheria na fursa za mikopo kutoka taasisi za fedha.
Wanachama huhamasishwa kufungua akaunti za vikundi benki ili kudhibiti fedha zao kwa usalama zaidi.
Ili kuhakikisha wanawake wanajitegemea kifedha, anasema hupewa elimu ya ujasiriamali, ikiwa ni pamoja na jinsi ya kuanzisha na kukuza biashara, usimamizi wa fedha, mbinu za masoko na namna ya kutengeneza bidhaa bora zinazokidhi mahitaji ya soko.
Vicoba huwa ni nguzo muhimu kwa wanachama wanapopitia changamoto za kifedha kama magonjwa, misiba au dharura nyingine. Hivyo wanachama kuweka akiba kwa ajili ya dharura ili kuhakikisha hakuna anayebaki bila msaada wanapokumbwa na matatizo.
Katika kuhakikisha wanakiundi wanapata manufaa, anasema wanashirikiana na wataalamu wa benki kutoa elimu zaidi kwa wanachama kuhusu jinsi ya kutumia huduma za kifedha kwa faida yao.
Hii ni pamoja na mikopo nafuu, akaunti za akiba na uwekezaji mdogo unaoweza kuwasaidia kukuza mitaji.
Hata hivyo, anasema wanawashauri wanachama kuchagua viongozi waaminifu na wenye uadilifu watakaoweza kusimamia kikundi kwa haki na uwazi.
“Viongozi wa Vicoba wanapaswa kuwa watu wenye ujuzi wa kusimamia fedha, kufanya uamuzi sahihi, na kuhakikisha kila mwanachama anapata fursa sawa ya kunufaika na kikundi,” anasema.
Annastazia Kalenga, mtaalamu wa masuala ya fedha anasema ili kuimarisha mafanikio haya ni muhimu kuwekeza katika elimu ya kifedha na kuwa na usimamizi mzuri wa mifumo ili iendelee kuwa chanzo cha maendeleo kwa wanawake wengi zaidi.
Anasema vikundi vinapaswa kuwa na uongozi thabiti wenye uadilifu na mfumo wazi wa uhasibu ili kuhakikisha fedha zinasimamiwa ipasavyo.
Serikali na taasisi mbalimbali zinapaswa kutoa mafunzo ya usimamizi wa fedha kwa wanachama wa Vicoba ili waweze kutumia mikopo yao kwa tija.
Anasema mifumo ya Vicoba imeleta mapinduzi makubwa katika maisha ya wanawake wengi nchini Tanzania.
“Licha ya changamoto zilizopo, kama usimamizi hafifu wa fedha, bado mifumo hii inabakia kuwa nyenzo muhimu katika kuhakikisha maendeleo ya wanawake na jamii kwa ujumla,” anasema.