Moshi. Viongozi wa vyama vya ushirika nchini wametakiwa kufanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia mifumo ya sheria za ushirika na taratibu za kifedha ili kuepuka migogoro na upotevu wa rasilimali za vyama hivyo.
Rai hiyo imetolewa jana Machi 7, 2025 na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, anayeshughulikia umwagiliaji na ushirika, Dk Stephen Nindi wakati wa ziara yake mkoani Kilimanjaro, yenye lengo la kuangalia mageuzi yanayofanywa na Serikali katika uboreshaji wa mifumo ya utendaji kazi na mifumo ya usimamizi wa vyama vya ushirika.
Dk Nindi amesema mifumo ya kisheria na miongozo ya ushirika inapokiukwa ndipo migogoro huibuka na rasilimali za ushirika kupotea, jambo ambalo kwa sasa Serikali isingependa kuona hayo yakitokea.
“Kwa sasa Serikali imeamua kuongeza nguvu kuwahudumia wakulima wadogo kupitia ushirika, hivyo nitoe wito kwa viongozi katika vyama vya ushirika, wahakikishe wanafanya kazi kwa weledi na kwa kuzingatia kanuni, sheria na miongozo ili kuwezesha kupatikana kwa tija kwa wakulima wanaohudumiwa katika vyama hivyo,” amesema Dk Nindi.
“Tusipojali mifumo ya kisheria, taratibu za fedha na za kiuongozi, tutaendelea kuwachanganya wakulima na kusababisha upotevu wa rasilimali za vyama vya ushirika, hivyo niwaase viongozi, wafanye kazi kwa kuzingatia weledi na waangalie sheria inasema nini na kanuni inasema nini.”
Dk Nindi ambaye pia ametembelea Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Kilimanjaro (KNCU) na kuzungumza na viongozi wa chama hicho, amesema ni wajibu wa vyama vikuu kutoa hamasa kwa wanachama wake ili wazalishe kwa tija na kujiongezea kipato kupitia kilimo.
Amesema ni jukumu pia la vyama vikuu kuvisimamia kwa tija vyama vya msingi na kuhakikisha vinakusanya mazao kwa usahihi ikiwa ni pamoja na kutunza akaunti za wanachama, lengo likiwa ni kuitengeneza kesho iliyo bora kwa vyama hivyo na wanachama wake.
“Niombe vyama vikuu viongeze tija ya kuvihudumia vyama vya msingi na kutoa hamasa ya vyama vya msingi na wanachama wao ili waweze kuzalisha kwa tija. Vyama vya ushirika viwe kama mwavuli ambao unahakikisha kunakuwa na usalama kwa vyama vya msingi na wanachama vinavyowahudumia,” amesema.
Meneja wa KNCU, Dk Honest Kessy amesema katika kuhakikisha chama hicho kinaboresha mifumo yake ya utendaji kazi, wamejiwekea mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuimarisha mikataba ya mali za chama hicho na kuongeza ufuatiliaji.
“Katika msimu huu tumejiwekea malengo na mikakati ya kusimamia na kudhibiti mali tulizonazo, kuimarisha biashara ya mauzo ya nje, kuweka miundombinu ya KNCU kujiendesha kitaasisi, kusimika na kutumia mfumo wa kielektroniki na kuimarisha uhusiano na huduma kwa wanachama,” amesema Dk Kessy.
“Katika mikakati hiyo tumejiwekea kila mwisho wa mwezi, tunakaa vikao katika ngazi ya menejimenti, kila mkuu wa idara na kitengo, anawasilisha alichokifanya kulingana na mpango kazi wetu, kuangalia kilichofanyika na kama kuna changamoto. Na kila baada ya miezi mitatu tunakaa kikao cha bodi kupitia taarifa zetu na vilevile kutushauri.”
Akizungumzia bei ya kahawa kwa msimu huu, Dk Kessy amesema imeendelea kuimarika na sasa imepanda kutoka Sh4,000 hadi Sh9,000 kwa kilo moja.
“Bei za kahawa mwaka huu ziko juu, wakati mwaka jana tulimlipa mkulima Sh4,643 kwa kilo moja, kwa msimu huu tutamlipa mkulima Sh9,000 kwa kilo, hii ni furaha kwa mkulima na bei inatoa hamasa ya kilimo cha kahawa,” amesema Dk Kessy.
Mkuu wa Wilaya ya Siha, Dk Christopher Timbuka amesema wanaendelea kushirikiana na vyama vya ushirika, lengo likiwa ni kuhakikisha vyama hivyo vinaendelea kujiimarisha na kupiga hatua za kimaendeleo.