Wafanyabiashara walia kuahirishwa Dabi | Mwanaspoti

WAFANYABIASHARA wanaofanya shughuli zao Uwanja wa Benjamin Mkapa, wameonyesha masikitiko makubwa kufuatia kuahirishwa kwa mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya Yanga dhidi ya Simba.

Mchezo huo uliotarajiwa kuchezwa leo saa 1:15 usiku, umeahirishwa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) ambayo ilitoa taarifa yake saa sita kabla ya kufika muda wa mchezo uliopangwa.

Kitendo cha kuahirishwa mchezo huo, wafanyabiashara waliozungumza na Mwanaspoti wamebainisha kuwa wamepata hasara na kuomba mamlaka husika iwe inatoa taarifa mapema ili kuondoa usumbufu kama huo.

Mmoja kati ya mama anayefanya shughuli za kuuza chakula ambaye hakutaka kutajwa jina, amesema mchana ni muda wa watu kula lakini mbaya zaidi ndio taarifa imetoka kwamba mechi haitachezwa.

Amesema kuwa, wamekuja kutafuta riziki lakini wameambulia hasara tu jambo ambalo limewaumiza wengi.

“Tulikuja kutafuta kipato lakini bahati mbaya riziki haikuwa upande wetu, lla wangetoa taarifa mapema tusingeingia hasara.

“Tunaomba siku nyingine wenye mamlaka watoe taarifa mapema ili tujue tunafanyaje kwa sababu hizi ni hasara za wazi kabisa, biashara kama ya jezi ndio haiharibiki lakini sisi wa chakula unadhani inakuwaje?” alihoji mama huyo.

Related Posts