Wakili ashinda rufaa kuhusu ubunge wa Cecil Mwambe

Dar es Salaam. Mahakama ya Rufani Tanzania, imeagiza kusikilizwa shauri la kikatiba lililokuwa limefunguliwa na Paul Kaunda, dhidi ya Spika wa Bunge na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), ambalo lilitupwa katika hatua ya pingamizi.

Msingi wa shauri hilo ni hatua ya Spika wa Bunge wa wakati huo, Job Ndugai kumrejesha bungeni, mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe licha ya kukihama chama chake cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kuhamia CCM.

Kaunda ambaye ni wakili wa Mahakama Kuu, alilalamika kuwa uamuzi wa Spika ulikiuka ibara ya 71(1)(e) ya Katiba inayosema mbunge atakoma kuwa mbunge iwapo atahama kutoka chama kilichomdhamini kugombea nafasi hiyo.

Hata hivyo, kesi hiyo ilikupambana na pingamizi la awali kuwa, ilikuwa ni mbaya kisheria, haina mashiko wala uhalali. Pingamizi hilo lilikubaliwa na jopo la majaji, Issa Maige, Stephen Magoiga na Seif Kulita na kutupa kesi hiyo.

Kaunda hakuridhika na uamuzi huo akakata rufaa ambayo katika hukumu ya rufaa iliyotolewa jana Machi 7, 2025 jijini Dar es Salaam na jopo la majaji Shaban Lila, Patricia Fikirini na Lameck Mlacha, ambapo ameshinda rufaa hiyo.

Katika hukumu, majaji hao wamekubali sababu za rufaa zilizowasilishwa na mlalamikaji wakisema pingamizi lililoondoa kesi hiyo halikuwa na hoja za kisheria na wala halikuwa na sifa ya kuitwa pingamizi la awali.

“Kutokana na hayo tuliyosema, rufaa inakubaliwa. Tunaagiza kuwa shauri hili lisikilizwe kama shauri la kikatiba na jopo la majaji wengine bila kuchelewa,” inaelekeza hukumu ya majaji hao wa Mahakama ya Rufaa.

Katika kesi hiyo ya Kikatiba ambayo sasa itasikilizwa na jopo la majaji wengine, wakili huyo ambaye ni mlalamikaji katika shauri hilo anaeleza kuwa mwaka 2015 Mwambe alichaguliwa kuwa mbunge wa Ndanda kwa tiketi ya Chadema.

Alihudumu kama mbunge wa Ndanda kwa tiketi ya chama hicho hadi Februari, 2020 ilipodaiwa kuwa alihama Chadema na kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM).

Kwa mujibu wa nyaraka za kesi hiyo, inadaiwa baada ya kuhama aliacha kuhudhuria vikao vya Bunge lakini baadaye alirejea bungeni baada ya kuitwa na Spika, hatua ambayo ilipingwa na Chadema kwa kumwandikia barua rasmi Spika.

Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alimwandikia barua Spika akimjulisha kuwa Mwambe alishakoma kuwa mbunge baada ya kuhama kutoka Chadema kwenda CCM na kumtaka aache kuendelea kumlipa stahiki kama mbunge.

Barua hiyo ilipomfikia Spika, alikuja juu na kutamka maneno: “Namshangaa Mnyika kwa sababu haya maneno anayosema ilipaswa aambatanishe na barua ya mheshimiwa Mwambe anayothibitisha haya anayosema. Hakuambatanisha.”

“Pili mimi Spika sina barua ya Mwambe inayothibitisha kwamba ameacha ubunge kwa hiari yake mwenyewe na kama chama hiki kimechukua hatua, sina viambatanisho vinavyoonyesha vikao halali ambavyo vilifanya maamuzi hayo.

“Kwa hiyo hii barua haina maana, haina mantiki na nichukue nafasi hii nawaambia wabunge wote including (pamoja) wabunge wa Chadema na wengine wanaotishwatishwa huko kwamba msibabaike na msiwe na wasiwasi.

“Mnaye Spika atawalinda mwanzo mwisho. Habari ya ukandamizaji, ubabaishaji haina nafasi hapa. Fanyeni kazi zenu kwa kujiamini, mmeaminiwa na wananchi, fanyeni kazi zenu wala msiwe na wasiwasi,” mwisho wa nukuu ya Spika.

Siku iliyofuata, Mwambe alinukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari yakiwamo magazeti, televisheni na redio akisema: “Ni kweli nilishajiondoa Chadema siyo mwanachama tena, nikajiunga  na CCM na kuachia nafasi yangu ya ubunge.

“Lakini nimerudi bungeni kutii wito wa mheshimiwa Spika Ndugai aliyenirudisha bungeni kumalizia muda uliobaki, mimi ni mwanachama wa CCM lakini nimetii wito wa Spika,” inaeleza nukuu iliyopo katika nyaraka za shauri hilo.

Katika shauri hilo, mdai anaeleza yeye anaona kuna suala la kikatiba ambalo linahitaji kupitiwa na Mahakama chini ya ibara ya 26(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama ilivyofanyiwa mabadiliko madogo mwaka 2002.

Kaunda anaiomba mahakama kuwa matamshi yaliyotolewa na Spika ya kumtambua Mwambe kama mbunge wa Ndanda wakati alishahama chama kilichomdhamini na kujiunga na CCM yalikiuka ibara ya 71(1) ya Katiba.

Anaiomba mahakama itamke kuwa Mwambe alikoma kuwa mbunge wa Ndanda kuanzia Februari 15, 2020 alipojiunga na CCM.

Pia anaiomba mahakama itamke kuwa Mwambe anapaswa kurejesha stahiki zote alizozipata kuanzia alipohama kutoka Chadema na kuingia CCM.

Shauri hilo lilitupwa baada ya kuwekewa pingamizi ambalo lilikubaliwa na mahakama, hivyo alikata rufaa akiwa na sababu mbili.

Moja, mahakama ilikosea kisheria ilipotamka kuwa shauri hilo halikuwa na maana.

Sababu ya pili ni kuwa, Mahakama Kuu ilikosea kisheria ilipoamua shauri hilo halikuhusu suala la kikatiba ambalo linapaswa kushughulikiwa na mahakama ya kikatiba na ni la kawaida, lingeweza kushughulikiwa kwa mapitio ya mahakama.

Related Posts