Mwanza. Wakazi wa Kijiji cha Buzilasoga Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza wametishia kubomoa majengo chakavu yaliyopo katika Shule ya Msingi Buzilasoga ili kuepusha maafa kwa watoto wao wanaosoma shuleni hapo.
Uamuzi huo wa kubomoa madarasa mabovu ambayo ni mawili, unakuja baada ya wananchi hao kutakiwa kuchanga Sh2,000 kila mmoja kwa ajili ya kutengeneza madawati ya kukalia wanafunzi wakiwa darasani.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye mkutano wa hadhara Machi 7, 2025, wanakijiji hao wamesema hatua ya kufikia kutaka kubomoa madarasa mabovu ni kuepusha hatari na hasara kwa jamii inayoweza kujitokeza.
“Ombi letu ni kubomoa majengo hatarishi, kwa mfano kuna watoto wanasoma pale wana miaka minne hawajui kama maeneo hayo yana hatari, lakini tukisema tusubiri mpaka barua itokee kwa mkurugenzi ni lini? amehoji Robert Petro, mkazi wa kijiji hicho.
Mkazi mwingine wa kijiji hicho, Jackson Lucas amesema hawajakataa kuchangia mchango wa madawati lakini usalama wa watoto wao ni muhimu, na kama hawaruhusiwi kuyabomoa basi shule ifungwe hadi yatakaporekebishwa.
“Sio kwamba tumekataa kuchanga pesa ya madawati, hata sasa tunaweza kuchanga, tunawapenda watoto wetu, lakini watasomea wapi? Ikiwa madarasa ni mabovu, kama sisi haturuhusiwi kubomoa hayo madarasa ni sawa pelekeni, lakini sisi kama kijiji ni bora tuifunge shule na Serikali itajua sababu nini?” amesema.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Buzilasoga, Enock Bahati ameungana na wanakijiji hao akieleza kuwa kuna haja ya kubomoa majengo ya madarasa chakavu kwa sababu yana nyufa, ambazo zinaweza kuhatarisha maisha ya wanafunzi wawapo masomoni.
“Ingawa tumewasilisha taarifa kwa ngazi zote za Serikali, hii changamoto ni hatari kwa watoto wetu. Madarasa yameharibika na mengine yamefungwa kutokana na uchakavu wake hadi imesababisha wanafunzi kusomea chini na nje ya madarasa, hivyo wakati tunasubiri utaratibu kwa Serikali, wito wangu walishughulikie mapema ili kuondoa adha hii,” amesema Bahati.
Kaimu Mtendaji wa Kijiji cha Buzilasoga, Adveta Ngunda amesema utaratibu wa kubomoa majengo ya shule haupo chini ya wananchi, hivyo wananchi wawe na subira jambo hilo limeshatolewa taarifa katika ngazi husika za Serikali.
“Wananchi hawaruhusiwi kubomoa taasisi mpaka kibali au ruhusa itoke kwa mkurugenzi, pia, mkurugenzi hawezi kuruhusu wananchi wabomoe majengo hayo, kuna utaratibu wake, hata hivyo jana (Alhamisi) nimepeleka barua kwa mkurugenzi, inawezekana bado ipo kwenye mchakato na haijashughulikiwa,” amesema Adveta.
Alipotafutwa kwa simu kuzungumzia ubovu wa madarasa hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Sengerema, Binuru Shekidele amesema hadi kufikia leo hajapata taarifa yoyote kuwa wananchi wanataka kubomoa majengo mabovu ya shule hiyo.
“Kwa sasa hilo silijui, ngoja nilifuatilie kwa undani wa taarifa hizo halafu nitakujulisha,” Shekidele.