Yanga yakomaa na Dabi, kupeleka timu Kwa Mkapa

Uongozi wa Yanga umesema kuwa mchezo wao dhidi ya Simba leo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa uko palepale licha ya watani wao kutoa taarifa kuwa hawatocheza.

Taarifa ambayo imetolewa na Yanga leo, Machi 8, 2025 imesema kuwa mchezo huo utachezwa kama kawaida kwa vile taratibu zimefuatwa.

“Uongozi wa Young Africans Sports Club unapenda kuutaarifu Umma kuwa, mchezo wetu wa Ligi Kuu ya NBC, uliopangwa kuchezwa leo tarehe 8/3/2025, dhidi ya Simba SC, saa 1:15 usiku upo palepale na hakuna mabadiliko yoyote.

“Young Africans SC kama wenyeji wa mchezo, tunaamini taratibu zote za mchezo kama inavyoelekezwa kwenye kanuni za Ligi Kuu ya NBC, ziko sawa na maandalizi yote yako tayari.

“Uongozi wa Young Africans SC utapeleka timu uwanja wa Benjamin Mkapa kama inavyoelekezwa kwenye kanuni, na hatutakuwa tayari kucheza mchezo huu siku nyingine tofauti na leo.

“Tunawaalika uwanjani Wanachama, Mashabiki, Wapenzi wa Klabu yetu na Wadau wengine waliosafiri kutoka mikoani, nchi za jirani na sehemu mbalimbali duniani kote kuja kushuhudia mchezo huu mkubwa Barani Afrika,” imesema barua hiyo ya Yanga.

Taarifa hiyo ya Yanga imetolewa saa chache baada ya Simba kutoa taarifa ya kugomea mechi hiyo ikidai kuwa kulikuwa na uvunjifu wa kanuni baada ya timu yao kuzuiwa kufanya mazoezi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, jana Ijumaa, Machi 7, 2025.

Related Posts