Unguja. Wakati Chama cha ACT- Wazalendo kikisema kinamshtaki Mkuu wa Wilaya ya Magharibi A, Sadifa Juma Khamis kwa madai ya kuingilia mchakato wa uandikishaji daftari la mpiga kura na kuwaweka watu ndani, kiongozi huyo amesema yupo tayari kwenda mahakamani kwa kuwa, ndiko watakapopimana hoja zao.
Akijibu tuhuma hizo baada ya kupigiwa simu na mwandishi wa Gazeti la Mwananchi leo Jumapili Machi 9, 2025, Sadifa amesema yupo tayari chama hicho kiende mahakamani kufungua mashtaka na hakuna aliyeonewa.
Taarifa iliyotolewa na Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Omar Said Shaaban inasema watamshataki Sadifa kwa jina na sio kwa nafasi wala cheo chake ili kukomesha vitendo vya baadhi ya viongozi hao wa kisiasa kutumia vibaya madaraka waliyonayo.
Shaaban ambaye pia ni Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar wa Serikali ya Mapinduzi amesema huo ndio mkakati wa chama kwa sasa, watakuwa wanawashtaki wakuu wa mikoa na wilaya kwa majina kutokana na vitendo vya kuvunja sheria wanavyofanya.
Amedai kuwa, Sadifa alitoa agizo Machi mosi na 3, 2025 la kuteswa, kupigwa na kuwekwa ndani raia wawili kinyume cha maelekezo ya sheria na taratibu zilizopo.
“Hivyo, tumeamua kuwashauri na kusimamia kila raia, awe mwanachama wetu asiwe mwanachama ambaye ni mwathirika wa matendo ya viongozi, tutawafungulia mashataka mahakamani kwa kuomba fidia na kuomba radhi,” amesema Shaaban.
Wakuu wa mikoa na wilaya chini ya kifungu cha 13 sheria ya tawala za mikoa namba nane ya mwaka 2014, wanapewa mamlaka kumuweka mtu ndani kwa saa 24 iwapo wataona anaweza kuhatarisha amani.
Shabaan amesema wametoa msaada kwa waathirika hao kupata wakili na tayari ameshamuandikia barua Sadifa na imeonesha kupokewa kupitia sheha wake.
Amesema, katika barua hiyo wamedai mambo mawili ikiwamo fidia ya Sh200 millioni kwa kumsababishia mateso na barua hiyo imemtaka Sadifa kuomba radhi hadharani kwa maandishi na kukiri kutenda kosa hilo.
Amesema, wakili wa wadai hao wamemtaka afanye hivyo ndani ya siku saba kwa kumpa fursa ya hiari kujibu au kutokujibu, pia anaweza kuwaita wahusika wakapatana juu ya kiwango hicho.
“Hata hivyo, akiamua kukaa kimya, haitazuia wadai kwenda mahakamani ambako huko wanaweza kudai zaidi ya hiki kilichodaiwa kwenye barua, tuna vielelezo vingi za kesi za namna hii ambapo Mahakama ilitenda haki kwa raia walioathiriwa,” amesema Shabaan.
Shabaan amesema ipo tabia ya baadhi ya wakuu wa mikoa na wilaya kuingilia michakato ya uandikishaji katika daftari la mpigakura kinyume na taratibu na sheria zilizopo kwa kigezo cha kulinda amani na usalama na kutumia vyombo vya ulinzi na usalama kuwalenga watu fulani.
“Kama ilivyo kawaida kwa nchi ambazo kiwango chake cha kuheshimu michakato ya kidemokrasia ni kidogo ikiwamo hapa kwetu, michakato kama hii hukumbwa na vitimbwi na mikasa mbalimbali ya uvunjifu wa sheria, haki za binadamu na haki za kikatiba,” amesema.
“Tayari vitimbi na mikasa hiyo vimeanza kujitokeza na tunatarajia vitaendelea kujitokeza hadi kufikia uchaguzi mkuu Oktoba 2025,” amesema.
Amesema ACT-Wazalendo kwa kuwa imebeba matumaini ya wananchi katika kulinda haki za raia na haki za kikatiba, wameamua kupinga jambo hilo kwa mwelekeo mpya.
Hata hivyo, Sadifa amesema endapo wataenda mahakamani lazima watoe uthibitisho wa madai hayo na mahakamani ndio itaamua.
“Hata mimi nilitamani jambo hili liende mahakamani ili tukaulizane na kujengeana hoja, mimi sijaweka mtu ndani watakwenda kutoa ushahidi wao wa maandishi ya mkuu wa wilaya” amesema Sadifa.
Amesema Mahakama zimetengenezwa kwa ajili ya watu, hivyo hamu yake waende huko na wasichelewe kwa sababu wao wenyewe wanaweza kushtakiwa kwa kile alichokiita kashfa.
Sadifa amesema, katika wilaya hiyo daftari lilikuwa huru na hakuna aliyenyimwa haki yake ya msingi wala aliyewekwa ndani katika kipindi chote cha uboreshaji wa daftari la kudumu la mpigakura katika wilaya yake.
Hata hivyo, ACT -Wazalendo imetoa wito kwa viongozi hao hususani katika kipindi hiki cha kuelekea kweye uchaguzi, kujiepusha na utendaji kazi wa hisia badala yake waongozwe na kanuni za kiutumishi.
Katibu wa Idara ya Habari, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma, Salim Bimani amesema wamejiandaa vyema katika kuongoza nchi hii.