AUNT BETTIE: EX wangu ananitega, anadai hajanisahau

Niliachana na mpenzi wangu miaka mingi iliyopita, ila hatukugombana tuliona hatuwezi kufika mbali, tukaamua kuachana na kila mmoja akafuata njia yake.

Sijamuona kwa miaka mingi. Ajabu nilipofunga ndoa mapema mwaka uliopita nikapigiwa simu na namba nisiyoijua kabla sijauliza jina nikaitambua sauti, kwanza nilistuka sana kwa sababu tulikuwa tunapendana ila hatukuweza kwenda pamoja katika safari ya kujitafuta kimaisha.

Kuanzia siku hiyo amekuwa akinipigia simu mara kwa mara kuniuliza hili na lile ikiwamo kunikumbusha nyakati nzuri tulizowahi kupitia wakati tulipokuwa pamoja.

Amenichanganya zaidi baada ya kuwa anarudia mara kadhaa kwamba amejaribu kunisahau ameshindwa.

Kwa shida sana nikamuuliza kama ameolewa akanijibu ndio na ana watoto wawili na mumewe hana shida anampenda. Nami nikamueleza nimeoa mwaka uliopita, ila halikuwa suala muhimu kwake wala hakulijadili zaidi ya kunisihi tuonane, nilikutana naye msisitizo ulikuwa kwamba ameshindwa kunisahau. Ananichanganya sana, naomba ushauri nifanyeje?

 Kwanza pole kwani nakuelewa, kujitokeza kwake baada ya miaka kadhaa na kusema kuwa ameshindwa kukusahau kunaweza kuwa jambo gumu na la kuchanganya, hasa ukizingatia kuwa sasa umeshaoana na mtu mwingine.

Kwanza, inatakiwa kutafakari kuhusu hisia zako mwenyewe. Ni muhimu kufahamu jinsi unavyohisi kuhusu mpenzi huyo wa zamani. Je, bado una hisia naye? Au umeshahamia kwenye maisha mapya na umekuwa na furaha katika ndoa yako?

Hii itakusaidia kujua jinsi ya kujibu hisia zake. Kwa sababu ni rahisi kubabaishwa na kumbukumbu za zamani, lakini ni muhimu kukumbuka kwa nini mliachana.

Inawezekana kweli ameshindwa kukusahau au ameona thamani yako baada ya kuwa mbali na wewe kutokana na aina ya mapenzi uliyokuwa ukimpa ana anayoyapa alipo, lakini hilo lisiyumbishe msimamo na mtazamo wako kuhusu maisha yako mengine uliyoyaanzisha.

Ni muhimu pia kufikiri kuhusu mtu (mke) uliye naye sasa. Mbali na hisia zinazoweza kuibuka, unahitaji kutafakari juu ya ndoa yako. Huku ukijikumbusha kuwa ndoa ni ahadi na hustahili kutafakari sana kwenye matukio kama haya.

Katika hali yako, kutafuta uhusiano na mtu wa zamani mwenye mwenza mwingine kunaweza kuleta machafuko na kuathiri ndoa yako.

Kauli yake kuwa ameshindwa kukusahau ina lengo la kulazimisha mawazo yake yawe kama ya kwako kuwa wewe ulikuwa ndiyo chaguo lake sahihi. Hapa ndipo ni muhimu kuweka mipaka madhubuti.

Uzuri wa kuwepo na mipaka ni kwamba inakutengenezea nafasi ya kudumisha heshima na uaminifu kwake bila kuathiri maisha yako ya sasa. Unaweza kuchuja hisia zake na kumsaidia kuelewa jinsi ambavyo umekuwa na mabadiliko katika maisha yako.

Kwa hivyo, unaweza kujaribu kukutana naye au kuzungumza naye kwa njia ya simu ili kumjibu kwa upole lakini kwa uwazi. Mweleze jinsi unavyohisi kuhusu ndoa yako na si rahisi tena kuwa na uhusiano ukizingatia na yeye ana maisha mengine na mwenza wake. Mwambie kwa uwazi kuwa unathamini kumbukumbu zenu za pamoja huko zamani, lakini kwa sasa, umeshapata uhusiano tofauti na unaheshimu hilo.

Zingatia na ni muhimu sana kumaliza mazungumzo kwa upendo, lakini kuonesha wazi kuwa huna nia ya kurudi kwenye uhusiano huo wa zamani. Unaweza pia kumsihi kwa msisitizo aendelee na maisha yake aachane na mawazo ya kukushawishi muanzishe tena uhusiano kwani hilo halitawezekana. Unapofanya hivyo, utadumisha heshima, upendo na maadili mema kwa wote wawili.

Hili si jambo rahisi kama hutakuwa imara kudhibiti hisia zako, kwa kuwa mliwahi kuwa wapenzi bila shaka una hisia naye, sema na moyo wako malizana naye uendelee na maisha mengine. Vizuri zaidi kama utapunguza mazungumzo naye kwenye simu kuepuka ushawishi endelevu.

Related Posts