Bei za petroli, dizeli zapaa Zanzibar, Zura yatoa sababu

Unguja. Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (Zura) imesema bei za mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa/ndege zimepanda kwa sababu ya kuongezeka gharama za uingizaji wa nishati hiyo nchini.

Akitoa taarifa za mabadiliko hayo kuanzia  leo Jumapili, Machi 9, 2025, Kaimu meneja kitengo cha uhusiano Zura, Shara omar Chande amesema bei hizo zimepanda kutokana na ongezeko la bei katika soko la dunia.

Lita ya mafuta ya petroli itauzwa kwa Sh2, 939 ikilinganishwa na Sh2, 819 za mwezi uliopita, ikiwa ni ongezeko la Sh120 sawa na asilimia 4.25.

Mafuta ya dizeli lita moja itauzwa Sh3, 135 ikilinganishwa na Sh2,945 tofauti ya Sh190 sawa na asilimia 6.45 huku mafuta yakiongezeka kwa Sh77 kutoka Sh2,423 hadi Sh2,500 sawa na asilimia 3.17.

“Mafuta ya taa yataendelea kuuzwa kwa bei ileile ya Sh3, 200,” amesema.

Ametaja sababu nyingine ni uingizaji wa mafuta na kuongezeka kwa wastani wa thamani ya dola ya Marekani ikilinganishwa na shilingi ya Tanzania.

Hata hivyo, ametumia fursa hiyo kuwahimiza wananchi kununua mafuta katika vituo halali na kudai risiti za kielektroniki kila wanaponunua nishati hiyo, ili kuepuka udanganyifu na kuiongezea mapato Serikali.

Naye Ofisa Mkaguzi Mwandamizi, Ali Abdallah Ali amesema licha ya kuongezeka kwa bei za mafuta matumizi ya wastani wa mapato yameongezeka licha ya kutokuwa na takwimu za ongeeko hilo.

Amesema wamejipanga kuhakikisha kipindi cha sikukuu ya Iddi hakutakuwa na upungufu wa mafuta kwani kipindi hicho nishati hiyo imekuwa ikitumika kwa kiasi kikubwa.

Nao baadhi ya watumiaji wa nishati hiyo wamesema kupanda kwa mafuta wakati wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, kunaashiria pia bidhaa muhimu za vyakula vitapanda bei kulingana na mahitaji.

“Inawezekana hali ikawa ngumu kutokana na kuongezeka kwa gharama za mafuta, kama tunavyojua kwa sasa ni Mwezi Mtukufu bidhaa zinahitajika kwa wingi, sasa mafuta yakipanda yataleta shida, Serikali ingeweka mkono wake,” amesema Hajra Zahor, mkazi wa Magogoni.

Related Posts