Dar es Salaam. Jaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Dk Modesta Opiyo amewataka wanawake wa Mahakama kutafakari kwa makini mchango wao kwa jamii inayowazunguka.
Pia, ametoa wito kwa wanawake kuendeleza juhudi katika utaoji haki na usawa kwa jamii bila ubaguzi.
Jaji Opiyo ametoa kauli hiyo jana usiku, Machi 8, 2025 katika hafla ya kusherehekea Siku ya Wanawake Duniani kwa watumishi wanawake wanaofanya kazi Mahakama ya Tanzania, Mkoa wa Dar es Salaam.
Amesema kaulimbiu ya maadhimisho ya siku ya wanawake kwa mwaka huu ni: “Wanawake na wasichana 2025: Tuimarishe Haki, usawa na Uwezeshaji.”
Amesema kaulimbiu hiyo, inawakumbusha wanawake wote waliopo Mahakama ya Tanzania kujiuliza maswali kwa nafasi zao mmoja mmoja.
“Je? tumefanikiwa kutoa haki kwa wanawake wenzetu wanaofika kupata huduma mahakamani kwa kiasi gani? na je? Dhana ya usawa katika maamuzi na utendaji kazi wetu tunaizingatia ipasavyo au bado baadhi yetu tuna mitazamo ya mila potofu dhidi ya mwanamke?” amehoji Jaji Opiyo huku akiwataka wanawake wa Mahakama kutafakari kwa makini mchango wao kwa jamii inayowazunguka.
“Nakumbuka Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, Machi 10, 2024 wakati akitoa hotuba yake katika kongamano la maadhimisho ya Siku ya Majaji Wanawake Dunia iliyofanyika jijini Dar es Salaam, aliwahi kusema, Mahakama imekuwa ikiona mchango wa majaji na mahakimu wanawake. Wanawake wanaleta mezania na mtazamo chanya kufahamu na uzoefu tofauti, uwiano wa kisheria na kukuza jamii inayoshirikishwa zaidi na wenye usawa,” amesema.
Akitoa takwimu za mchango wa wanawake katika masuala ya usawa, Jaji Opiyo amesema watumishi wanawake wa Mahakama kwa Mkoa wa Dar es Salaam, wapo 531 na idadi hiyo ni kubwa ikijumuisha watendaji wa Mahakama, majaji, naibu wasajili, mahakimu na watumishi wa kada nyingine.
“Umahiri wetu unatokana na kushirikiana na watumishi wanaume, tunatekeleza jukumu zima la utoaji haki kwa wananchi kwa wakati. Hivyo, nitoe rai kwa watumishi wenzangu wanawake kuendeleza juhudi katika utoaji haki kwa jamii na mahali pa kazi na bila kuziacha nyuma familia zetu,” amesisitiza.
Aidha, takwimu zilizopo kwa sasa zinaonesha, katika mhimili wa Mahakama kuna usawa wa kijinsia katika nafasi mbalimbali za uongozi.

Baadhi ya Watumisi Wanawake wa Mahakama ya Tanzania kwa Mkoa wa Dar es Salaam, wakiwa katika picha ya pamoja na Jaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi Dk Modesta Opiyo na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, Salma Maghimbi, wakati wa sherehe ya Siku ya Wanawake Dunia, iliyofanyika jana usiku jijini Dar es Salaam.
Mathalani majaji wa Mahakama ya Rufani wapo 39, wanawake 13 sawa na asilimia 33; majaji wa Mahakama Kuu wapo 104, kati yao wanawake ni 40 sawa na asilimia 38.
Naibu wasajili wapo 82, wanawake ni 42 sawa na asilimia 51 na watendaji wa Mahakama wapo 42 kati yao wanawake wako tisa sawa na asilimia 21.
” Ingawa bado kuna kazi ya kufanya, lakini wanawake tunatakiwa kijivunia mafanikio haya na kuendeleza juhudi ili uwezo wetu uweze kuonekana katika utendaji kazi,” amesema Jaji Opiyo.
“Natoa wito na kuendelea kuhamasisha utaoji wa haki bila kusahau watu wenye uhitaji maalumu,” amesema.
Jaji wa Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Salma Maghimbi amesema jukumu lao kama wanawake ni kuhakikisha wasichana wanajengewa uwezo na wanakuwa katika misingi ya haki ili waje kuwa viongozi wa baadaye watakao jenga Taifa kwa kusimamia haki na usawa kwa jamii.
” Lakini, kwa sisi wanawake, kazi yetu ni kuhakikisha tunakuza Taifa lenye usawa, lenye haki na kuendelea kufanya uwezeshaji kwa kila sekta,” amesema Jaji Maghimbi.
Katika hafla hiyo, wanawake hao walipata elimu kuhusiana na afya zao, namna ya kukabiliana na afya ya akili na maandalizi ya maisha ya wanawake baada ya kustaafu.
Mtaalumu wa masuala ya uraibu na afya ya akili kutoka Taasisi ya MDH, Dk Said Mkwizu amewataka wanawake kupata muda wa kutosha wa kupumzika mara baada ya kutoka kazini pamoja na kula chakula bora chenye lishe.
Aloisia Shemdoe ambaye ni Mtafiti wa Afya ya Jamii, amewasihi wanawake kutumia vyakula vya asili ili kuboresha miili yao na kuepuka kula vyakula vilivyosindikwa hasa walio katika safari ya ukomo wa hedhi.