Kada CCM aliyemwagiwa tindikali aandika barua THBUB, ajibiwa

Moshi. Kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Idrisa Moses maarufu Makishe, ameiandikia barua Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), akiiomba kuanza uchunguzi huru kuhusu tukio la kumwagiwa tindikali.

Septemba 20, 2024 saa 2:00 usiku, watu wasiojulikana walimmwagia Makishe ambaye ni mkazi wa mjini Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro kimiminika kinachodhaniwa ni tindikali na kuharibu sura yake na jicho moja haliwezi kuona tena.

Mwenyekiti wa THBUB, Jaji mstaafu Mathew Mwaimu, alipoulizwa na Mwananchi jana Jumamosi, Machi 8, 2025 amejibu kwa kifupi:-“Tumeipokea (barua) na hatua za awali tumeona ni suala linalotupasa kufuatilia na kulifanyia uchunguzi. Nimeshatoa maelekezo.”

Katika barua hiyo, kada huyo amedai kwa jinsi sura yake ilivyoharibika, hata watoto wake wadogo, mmoja anayesoma chekechea na mwingine anayesoma darasa la kwanza wanaogopa kumsogelea isipokuwa kama amevaa miwani.

“Ninakuandikia (mwenyekiti) barua hii nikitambua majukumu iliyonayo Tume kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 130,” anaeleza kada huyo katika barua yake hiyo ya Machi 5, 2024.

“Ibara hiyo imeainisha majukumu ya Tume kuwa, pamoja na (b), kufanya shughuli za kupokea malalamiko ya uvunjaji wa haki za binadamu kwa jumla, ibara ndogo ya (c), Tume itafanya uchunguzi juu ya mambo yanayohusu uvunjaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.”

“Ni kutokana na majukumu hayo mazito ya Kikatiba, ninakuandikia barua hii ili Tume yako ifanye uchunguzi huru wa tukio langu la kumwagiwa tindikali,”ameandika Makishe.

Makishe amesema anatambua Ibara ya 130 ya Katiba haizuii Tume kufanya uchunguzi wowote hata kama jambo linachunguzwa na chombo kingine na kusema yapo matukio ilichunguza licha ya kuwa polisi nao wanachunguza.

Mfano ni kifo cha mwanafunzi wa Chuo Kikuu Dodoma (Udom), Nusura Abdalah ambacho kilizua utata, pia THBUB inachunguza matukio ya kupotea na kutekwa kwa watu nchini, ambayo polisi nao wanachunguza.

Kwa nini anaiomba Tume ichunguze

Makishe katika barua hiyo, amesema amesukumwa kuiomba tume kuchunguza kutokana na uzito na mazingira ya tukio lenyewe ili tume ifanye uchunguzi huru wa kufahamu nini kilitokea, nani walifanya hivyo na sababu za kufanya hivyo.

“Dalili za awali, zinadai uwepo wa genge la wenye nguvu kifedha. Ninasema hivyo kwa sababu kushambuliwa kwangu kulikuja saa chache tangu kutokee majibishano katika group la WhatsApp ambalo nilipata vitisho,” amedai.

“Ni nadharia inayotumika katika jinai (criminology) kwamba, kama kuna mtu anapata matatizo, iwe kifo au kuumizwa vibaya kama ilivyonitokea, mshukiwa au washukiwa wa kwanza wanakuwa wale waliotoa vitisho dhidi ya mtu huyo,” amesema.

“Dalili za nani wanaweza kuwa walisuka, kufadhili na kutekeleza uhalifu huu ziko wazi na niko tayari kuwaeleza wachunguzi utakaowatuma…”

“Ni matumaini yangu kuwa utalipokea ombi langu hili kwa mtizamo chanya na si kwamba siiamini ofisi yako, bali mazingira niliyoyaeleza yananisukuma hivyo.

“Ibara ya 13.-(1) ya Katiba ya Tanzania inasema kuwa watu wote ni sawa mbele ya sheria, wana haki, bila ya ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria, hivyo naiomba ofisi yako ianzishe uchunguzi huru wa tukio hili.”

Baada ya tukio hilo kutokea, Septemba 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa alitoa taarifa kuwa polisi wameanzisha uchunguzi.

Kamanda Maigwa alinukuliwa akiwaambia wanahabari kuwa siku ya tukio, Makishe ambaye ni dereva bodaboda akiendesha pikipiki yake aina Sinorai,  alikodishwa na mtu asiyemjua saa 2:00 usiku kutoka kijiweni kwake.

Mtu huyo alimtaka ampeleke eneo la Njoro katika Manispaa ya Moshi.

Kwa mujibu wa Kamanda Maigwa, baada ya kufika, abiria aliyembeba alimwambia asimame ili amchukue mwenzake ndipo alipojitokeza kijana mwingine aliyemwagia kimiminika hicho usoni na kumpora pikipiki yake hiyo aina ya Sinorai.

Baadaye pikipiki hiyo ilipatikana imetelekezwa na watu hao katika Msitu wa Njoro ambao hauko mbali na eneo la tukio na Desemba 2024, polisi walimrudishia Makishe simu yake na pikipiki hiyo wakati wakiendelea na uchunguzi.

Akizungumzia jamii ilivyompokea baada ya kutoka hospitali na kurejea nyumbani na kuwa na mwonekano tofauti na alioondoka nao, Kada huyo wa CCM amesema jamii hususan watoto wake wadogo wamekuwa ni watu wa kumuogopa.

“Watoto wangu wadogo, sasa hivi wananiona kama mtu wa maajabu. Mmoja yuko darasa la kwanza mwingine yuko Chekechea. Wananiogopa na wakati mwingine huwa wanakosa hata ile amani au ile raha ya kuwa karibu na mimi,” amesema Makishe.

“Kwa hiyo unakuta wakati mwingine muda wote lazima ukae umevaa miwani ili kuepuka ile hali halisi ya uso ukiwa wazi. Wanakuwa na ile hofu na uoga. Lakini pia jamii ambayo imenizunguka watu wananiona kama nimekuwa ajabu fulani,” amesema.

Kada huyo amesema: “Mwenyewe pia vinanikera na kuniumiza kwa namna ambavyo jamii inavyoweza kunichukulia hususan watoto wangu. Yaani jamii ya nje hainiumizi sana, lakini watoto wangu ni kitu kinaniuma sana maana wameharibika saikolojia sana.”

“Kuna wakati mwingine walikuwa wanasema na ukiunganisha kabisa maneno yao unaona kuna wanachokiongea kinatoka moyoni.  Wanasema baba ulitoka halafu ukasema unakuja halafu baadaye kaka akatuambia twende baba ameumia,” amesema Makishe.

“Wananiambia tuliambiwa walikuumiza walikumwagia tindikali na pikipiki yako. Tukiwashika tutawaua. Yale maneno yanawatoka kama watoto lakini ukiyatafakari unabaini wanaumia moyoni mwao.”

Machi 5, 2022 Tariq Awadhi au Kipemba anayejishughulisha na utalii mjini Moshi alimwagiwa kimiminika kinachoaminika ni tindikali na hadi leo sasa hakuna mtu aliyefikishwa kortini kuhusiana na tukio hilo.

Tukio hilo lilitokea usiku wa saa 2:00 wakati Tariq akitokea nyumbani kwake Shant town kwa ajili ya kupata chakula cha jioni ambapo vijana wawili wakiwa na bodaboda wakamwagia kitu usoni na mikononi na kumjeruhi vibaya.

Aprili 19, 2022, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa alisema wanamshikilia mtuhumiwa aliyemwagia Tariq tindikali na kwamba alikiri kutenda kosa hilo ambapo baadaye aliachiwa kwa dhamana.

Tangu Makishe amwagiwe tindikali zimepita siku 170 hadi kufikia leo Machi 9,2025 wakati kwa tukio la Tariq zimepita siku 1,100 na katika matukio yote mawili, hakuna mshukiwa ambaye amefikishwa mahakamani hadi sasa.

Related Posts