KITENDO cha Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi Kuu Bara (TPLB) kutangaza kuahirisha mchezo wa Kariakoo Dabi kati ya Yanga na Simba, kimeacha maswali mengi na kuzua mijadala kuanzia mtaani hadi katika mitandao ya kijamii.
Kabla ya TPLB kutoa taarifa ya kuahirishwa kwa mchezo huo jana saa 7:53 mchana, tayari Simba ilitoa tamko la uamuzi wa kugomea kucheza ikidai imenyimwa haki ya kikanuni ya kufanya mazoezi kwenye uwanja wa mechi siku moja kabla.
Taarifa iliyotolewa na Simba usiku wa Machi 8, 2025, ilifafanua kuwa uamuzi wa kugomea mechi umechukuliwa kwa vile kanuni zimekiukwa.
“Simba Sports Club imesikitishwa na vitendo visivyo vya kiungwana dhidi ya timu yetu kuelekea Mchezo wa Ligi Kuu NBC dhidi ya Yanga, Simba ikiwa timu mgeni.
“Kwa mujibu wa Kanuni 17(45) ya Kanuni za Ligi Kuu Bara, Timu Mgeni ina haki ya kufanya mazoezi kwenye uwanja wa mechi angalau mara moja kabla ya siku ya mechi katika muda tarajiwa wa mchezo husika. Kwa makusudi Simba imenyimwa haki hiyo licha ya kufika uwanjani katika muda husika.
“Katika sintofahamu hiyo, Simba iliarifiwa na Meneja wa Uwanja kuwa hana maelekezo ya kuruhusu mazoezi kufanyika bila maelekezo ya kamishna wa mchezo. Pamoja na kamishna wa mchezo husika kufika, mabaunsa wa klabu ya Yanga walivamia msafara wa Simba huku wakiendelea na vurugu na wakizua msafara wa simba kuingia uwanjani kufanya mazoezi.
“Jitihada za Simba kupata fumbuzi wa changamoto hiyo hazikuzaa matunda kwa zaidi ya masaa mawili kabla ya Simba kuondoka eneo la nje ya uwanja kwa sababu za kiusalama ambazo zimerekodiwa kwa ajili ya ushahidi.
“Kufuatia ukiukwaji huo wa Taratibu za Mchezo, Simba haitoshiriki mchezo husika na haki zote zimehifadhiwa. Simba inahimiza kuchukuliwa kwa hatua stahiki dhidi ya wahusika wote wa sakata hili,” ilifafanua taarifa hiyo ya Simba.
Kanuni hiyo ya 17(45) inafafanua hivi: “Timu ngeni itafanya mazoezi kwenye uwanja wa mechi angalau mara moja kabla ya siku ya mechi katika muda tarajiwa wa mchezo husika. Sababu zozote za kukwamisha timu mgeni kukidhi ipasavyo au kupata haki hii zitathibitishwa kwanza na kamishna wa mchezo.â€
Simba ilienda uwanjani hapo saa 1 usiku muda ambao mchezo huo ulipangwa kuchezwa kwa ajili ya kufanya mazoezi, lakini ilizuiwa na wanaosemekana kuwa makomandoo wa Yanga na hivyo kulazimika kuondoka.
Wakati Simba ikitoa tamko hilo, Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo, Crescentius Magori, alikazia kwa kusema: “Siyo mechi ya kesho (jana) tu, hatuchezi ligi mpaka hawa walioshiriki kwenye huu upuuzi waadhibiwe.”
Saa chache baada ya Simba kutoa taarifa ya kugomea mechi hiyo, uongozi wa Yanga ukajibu kwa kusema wangepeleka timu uwanjani na kweli walifanya hivyo.
Taarifa yao ya mapema kabla ya kuahirishwa kwa mchezo huo ilisema: “Uongozi wa Young Africans Sports Club unapenda kuutaarifu Umma kuwa, mchezo wetu wa Ligi Kuu ya NBC, uliopangwa kuchezwa leo (jana) tarehe 8/3/2025, dhidi ya Simba SC, saa 1:15 usiku upo palepale na hakuna mabadiliko yoyote.
“Young Africans SC kama wenyeji wa mchezo, tunaamini taratibu zote za mchezo kama inavyoelekezwa kwenye kanuni za Ligi Kuu ya NBC, ziko sawa na maandalizi yote yako tayari.
“Uongozi wa Young Africans SC utapeleka timu uwanja wa Benjamin Mkapa kama inavyoelekezwa kwenye kanuni, na hatutakuwa tayari kucheza mchezo huu siku nyingine tofauti na leo.
“Tunawaalika uwanjani wanachama, mashabiki, wapenzi wa klabu yetu na wadau wengine waliosafiri kutoka mikoani, nchi za jirani na sehemu mbalimbali duniani kote kuja kushuhudia mchezo huu mkubwa barani Afrika.â€
Makamu wa Rais wa Yanga, Arafat Haji, ameandika hivi: “Nitakuwa wa mwisho kuamini kuwa kwa msimu wa 2024/25 Yanga SC itacheza mchezo mwingine wa Derby zaidi ya uliokuwa umepangwa tarehe 8/03/2025.”
Msafara wa kikosi cha Yanga uliwasili uwanjani hapo saa 10:30 jioni ukisindikizwa na ving’ora vya polisi, huku mashabiki wa timu hiyo waliokuwa ndani na nje ya uwanja walionekana kuwa na furaha kuwashangilia mastaa wao.
Wakati hayo yote yakiendelea, taarifa ya Bodi ya Ligi ilisema imeahirisha mechi hiyo ili kupata fursa ya kuchunguza zaidi undani wa tukio hilo.
“Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha leo (jana) Machi 8, 2025 ilipitia shauri la klabu ya Simba kuzuiliwa kuingia kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa ajili ya kufanya mazoezi ya mwisho kuelekea mchezo namba 184 wa Ligi Kuu ya NBC (Young Africans SC vs Simba SC) uliopanga kufanyika kwenye uwanja huo leo (jana) kuanzia saa 1:15 usiku.
“Katika shauri hilo, klabu ya Simba iliiandikia barua Bodi ya Ligi kueleza kuhusu tukio tajwa hapo juu, huku pia ikieleza nia yao ya kutoshiriki mchezo huo kwa sababu imezuiliwa kutumia haki yao ya kikanuni kama ilivyoainishwa kwenye Kanuni ya 17:45 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
“Baada ya kupokea barua hiyo, Bodi ya Ligi iliwaagiza maofisa wake wa mchezo (ambao walishuhudia tukio hilo), kutuma taarifa ya tukio haraka ili hatua zinazostahili ziweze kuchukuliwa, ikiwemo kuitishwa kwa kikao cha dharura cha Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi. Baada ya kupitia taarifa mbalimbali zikiwamo za maofisa wa mchezo na vyanzo vingine, Kamati ilibaini kuwa Klabu ya Simba, wakati ikielekea kutumia haki yake iliyoainishwa kwenye Kanuni ya 17:45 ya Ligi Kuu, haikuwasiliana na ofisa yeyote wa mchezo, timu mwenyeji wala mamlaka ya uwanja kuhusu nia yao ya kufanya mazoezi katika uwanja huo ili maandalizi ya kikanuni yafanyike.
“Katika taarifa hizo, Kamati ilibaini pia kuwa walinzi ambao baadhi walifahamika kwa sura kuwa ni wa klabu ya Yanga, walishiriki tukio la kuzuia basi la klabu ya Simba kuingia uwanjani kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:45 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
“Kwa sababu pia Bodi ilipokea taarifa ya Ofisa Usalama wa mchezo ambayo imeainisha matukio kadhaa yaliyoambatana na tukio hilo la klabu ya Simba kushindwa kufanya mazoezi, na kwamba baadhi ya matukio yanahitaji chunguzi ambao hauwezi kukamilika kwa wakati, Bodi ya Ligi kupitia Kamati yake ya Undeshaji na Usimamizi wa Ligi imeamua kuahirisha mchezo tajwa hapo juu kwa mujibu wa Kanuni ya 34:1 (1.3) ya Ligi Kuu kuhusu Kuahirisha Mchezo, ili kutoa nafasi ya kupata taarifa zaidi zitakazosaidia kufanya uamuzi wa haki. Bodi itatoa taarifa kamili,” ilisema TPLB.
Ikiwa itabainika maofisa wa usalama wa Yanga walihusika kuizuia Simba kufanya mazoezi, kanuni ya 47 (1) inafafanua adhabu ambayo inaweza kupata.
“Klabu ina wajibu na jukumu la kuhakikisha kuwa wachezaji, viongozi, wanachama na wapenzi wake wanajiheshimu na hawajihusishi na vitendo vyovyote vya utovu wa nidhamu kama vile matusi, vitisho, vurugu, vitendo vinavyoashiria imani za kishirikina na vitendo vyovyote vingine visivyokuwa vya kimichezo kwenye viwanja vya michezo.
“Klabu ambayo mashabiki/wachezaji/viongozi wake watafanya vitendo hivyo itatozwa faini ya Sh5 milioni na kwa makosa ya kujirudia, faini itatozwa kati ya Sh10 milioni na Sh20 milioni,” inafafanua kanuni hiyo.
Ikiwa Simba itabainika imegomea mchezo, kanuni ya 47(6) inafafanua kuwa adhabu kubwa ni timu kushushwa daraja.
“Klabu itakayoshindwa kupeleka timu uwanjani baada ya kuhudhuria kikao cha maandalizi ya mchezo itatozwa faini ya Sh5 milioni na kushushwa daraja. Kiongozi aliyeshiriki kutopeleka timu uwanjani atafikishwa kwenye Kamati ya Nidhamu au Kamati ya Maadili ya TFF,” imefafanua kanuni hiyo.
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Angetile Osiah ‘Ngeta’ alisema kinachosababisha kanuni kushindwa kufuatwa ni Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kushindwa kujisimamia yenyewe.
“Endapo Bodi ya Ligi ingekuwa huru haya yasingetokea, naamini yanatokea kwasababu Shirikisho linafahamu kuna mtu ataangushiwa jumba bovu, Bodi inachaguliwa na viongozi wa klabu na baadhi ya wajumbe, lakini ikijisimamia watashikana mashati wenyewe,” alisema na kuongeza.
“Wanaoongoza mpira wanaziogopa Simba na Yanga, sio rahisi kufanya uamuzi, kikanuni timu zote zimekosea, ni utoto kuzuia timu ambayo kikanuni ipo sahihi kufanya mazoezi lakini pia timu kususia kucheza mchezo ni makosa.”
Ngeta alisema watu wamesafiri kutoka umbali mrefu na wengine wameacha majukumu yao ili kutazama mpira, kampuni zimewekeza pesa nyingi, wafanyabiashara wadogo wadogo pia wamewekeza fedha zao, je hao wanazingatiwa vipi katika kufidiwa hasara?”
Alisema kanuni iliyopo ya kuadhibiwa kwa timu ambazo zinafanya makosa hayo haziathiri timu hizo kwani zimekuwa zikifanya makosa kwa makusudi zikiamini zitalipa kwa mujibu wa kanuni.
“Najiuliza ni kwanini bodi ilianzishwa kama haiwezi kujisimamia na kwanini kama ina umuhimu hawaipi uhuru wa kujisimamia yenyewe na kuwa na uamuzi wao, naamini wakijisimamia wenyewe haya madudu hayawezi kutokea.”
Wakati huohuo, Ngeta alisema kuahirishwa kwa mchezo huo kutakuwa na vikao vya kimyakimya wakiziita Simba na Yanga kulimaliza hilo kwa kuwatumia watu mashuhuri na viongozi wa kisiasa.
“Yanga wametoa taarifa kuwa wao wataenda uwanjani kama kawaida na hawatacheza mchezo mwingine baada ya huu, naamini hilo halitafanyika, busara zitatumika kwa viongozi wa kisiasa na watu mashuhuri kuzituliza hizi timu na mchezo utachezwa katika tarehe mpya.”
Hapa kuna maswali ambayo yameibuka baada ya kuahirishwa kwa mchezo huo huku mashabiki na wadau wa soka wakibaki hawana majibu ya moja kwa moja.
1. Kama Simba haikutoa taarifa ya kwenda kufanya mazoezi, kipi kinachofanya mchezo uahirishwe hata kama kanuni za kuzuiwa kufanya mazoezi ilikuwa upande wao?
2. Waliolipa viingilio wanafidiwa vipi gharama zao?
3. Gharama za mchezo ujao zitabebwa na nani?
4. Yanga wamesisitiza kama mechi haijachezwa Machi 8, 2025 hawachezi tena, nini hatma yake?
5. Hii si mara ya kwanza tukio kama hili linatokea, matukio ya namna hii yanatoa picha gani juu ya udhibiti wa hadhi ya ligi yetu?
6. Licha ya Simba kuwa na haki kikanuni kufanya mazoezi uwanja wa mechi siku moja kabla, kanuni ipi inawafanya wagomee mchezo?
7. Ni uamuzi gani wa haki utatolewa ambao utasimamia kanuni?