Matano agusia mambo mawili Ligi Kuu Bara

BAADA ya kukusanya pointi sita kwenye mechi mbili mfululizo nyumbani na ugenini, kocha mkuu wa Fountain Gate, Robert Matano amesema nafasi ya kushuka au kupanda katika nafasi kwa timu zote ni kubwa na bado inatishia mwelekeo wa Ligi Kuu Bara.

Matano ameiongoza Fountain Gate kwenye mechi saba baada ya kukabidhiwa mikoba ya Mohamed Muya ambaye alisitishiwa mkataba kutokana na matokeo yasiyoridhisha, amefungwa mechi tatu, sare mbili na ushindi mbili.

Akizungumza na Mwanaspoti, Matano alisema ana kibarua kigumu kuendelea kuijenga timu hiyo ili kuendeleza walipoishia kwenye mechi zilizobaki akidai haitakuwa rahisi kwake kutokana na kila timu kuhitaji matokeo ili kujihakikishia nafasi ya kucheza msimu ujao na nyingine kuwinda ubingwa.

“Wachezaji wangu wana mabadiliko makubwa kwenye maeneo mengi tofauti na tulivyoanza nafurahishwa na namna ambavyo wamekuwa wakibadilika na kunielewa naendelea kusuka vizuri safu ya ulinzi na ushambuliaji ili kusiwe na makosa madogomadogo ambayo yatatuondoa kwenye malengo,” alisema na kuongeza:

“Ukikwama kidogo kupata matokeo kwenye mchezo mmoja unashushwa hii ni kutokana na idadi ndogo ya alama tuliyoachana na timu tunazofukuzana nazo. Ili kuweza kukwepa changamoto ya kuingia kwenye presha ya kushuka daraja tunahitaji kupata matokeo.”

Matano alisema ligi bado ina nafasi kwa kila timu kubaki msimu ujao, hivyo kocha na kikosi kitakachochanga karata zake vizuri ndicho kitakachoweza kucheza ligi msimu ujao, huku akidai kuwa kumaliza nafasi nne za juu kama mipango yao ilivyokuwa ni mtihani na sasa wanapambana kucheza msimu ujao.

Akizungumzia mchezo wao na KMC wakiibuka na ushindi wa mabao 2-1,  alisema licha ya kutanguliwa kufungwa wachezaji wake walicheza kama fainali wakipambana hadi dakika za mwisho na ndio siri ya ushindi walioupata.

“Haiishi hadi iishe ndio ilikuwa kauli ya wachezaji wangu baada ya kukutana vyumbani na hicho ndio walichokifanya na hatimaye kuibuka na ushindi tukiendelea na ushindani huu nafasi yetu ya kufanya vizuri ipo,” alisema.

Related Posts