NMB na Nelson Mandela kushirikiana kukuza vipaji vya teknolojia ya kidijitali

Arusha. Benki ya NMB imeingia makubaliano ya ushirikiano na Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela ya Afrika (NM-AIST) ili kukuza maendeleo ya vipaji na ubunifu katika nyanja mbalimbali za teknolojia za kidijitali.

Hati ya Makubaliano (MoU) imesainiwa leo Jumapili Machi 9, 2025 yanayolenga kutambua, kulea, na kukuza vipaji vya ubunifu katika teknolojia ya kidijitali kwa miaka mitano.

Makubaliano haya pia yatawezesha kufanyika utafiti na ubunifu utakaozalishwa na wahitimu wa NM-AIST, hasa zinazoshughulikia changamoto za kijamii katika sekta za kifedha, ujasiriamali na ajira kwa kutumia suluhisho za kiteknolojia.

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini, Ofisa Mkuu wa Rasilimali Watu wa Benki ya NMB, Emmanuel Akonay amesema makubaliano hayo ni muendelezo wa juhudi za taasisi yao katika kukuza sekta ya elimu, ubunifu na teknolojia.

“Leo, hatutii saini tu, bali tunajenga pia msingi thabiti kwa ajili ya ukuaji wa teknolojia nchini, tunaamini maendeleo endelevu yanategemea usimamizi wa rasilimali watu kupitia maarifa na ujuzi ili kukabiliana na mabadiliko ya haraka ya kiteknolojia,” amesema.

“NMB itaendelea kutambua na kukuza vipaji mbalimbali, lengo likiwa ni kutengeneza wataalamu wenye ujuzi mkubwa katikaTeknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) ambao utasaidia kutatua changamoto za kifedha.”

Makamu Mkuu wa Chuo cha NM-AIST, Profesa Maulilio Kipanyula, amesema ushirikiano huo utaleta mchango katika sekta ya elimu, hasa kwa vijana wenye vipaji vya ubunifu katika nyanja ya teknolojia na Tehama.

“Taasisi yetu inajikita kutoa mafunzo katika ngazi ya uzamili na uzamivu, na pia tunalenga katika masuala ya utafiti na ubunifu na ili kufikia malengo haya, ni muhimu kufanya kazi na wadau ili kuboresha tija ya elimu yetu, ndio maana leo tuko benki yetu pendwa kufanikisha hili,” amesema Profesa Kipanyula.

 “Lengo letu ni kuwawezesha vijana kuona teknolojia na ubunifu kama fursa,  tunaangalia namna ya kutoa mchango katika kuzalisha ajira mpya kupitia sekta ya teknolojia,” amesema.

Mmoja wa wanafunzi wa chuo hicho, Erica Kimei, amesema changamoto inayowakumba wanafunzi wa elimu ya juu ni upatikanaji wa fedha za kufanya utafiti na kuendeleza kwa vitendo ili ilete tija kwa jamii na nchi kwa jumla.

“Changamoto kubwa ya wanafunzi wa elimu ya juu ni uwezeshaji wa kufanya tafiti zenye tija, ingawa tunaweza kujitolea kufanya tafiti nzuri, lakini ukata wa fedha husababisha tafiti nyingi kubaki kwenye makabrasha.

“Tunawaomba taasisi za elimu ya juu na kifedha kuendeleza ushirikiano kama huu ili kukuza bunifu, teknolojia na uvumbuzi, tunazoibua,” amesema Kimei.

Related Posts