Dar/Mwanga. Rais Samia Suluhu Hassan ameeleza magumu yaliyopitiwa wakati wa utekelezaji wa mradi wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe, akisema kuna wakati ililazimika kusukumana, kusutana na hata kushitakiana na makandarasi.
Historia inaonyesha mradi huo wa maji ulitolewa ahadi na Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete Mei 29, 2005 wakati akiomba kura kuingia madarakani kwa kipindi cha kwanza.
Baadaye mwaka 2006, upembuzi yakinifu ulifanyika kwa ajili ya mradi kuanza kutekelezwa, lakini jiwe la msingi la kuanza utekelezwaji liliwekwa mwaka 2018 na hatimaye mwaka 2024 maji yakaanza kutoka, ikiwa imepita miaka 20.
Mradi huo chanzo chake ni Bwawa la Nyumba ya Mungu, ulianza kutekelezwa mwaka 2014 na sasa awamu ya kwanza imekamilika ukiwa umegharimu Sh406.07 bilioni.
Akizungumza leo Jumapili, Machi 9, 2025 katika hotuba yake ya uzinduzi wa mradi huo mbele ya wananchi wa Mwanga mkoani Kilimanjaro, Rais Samia amewashukuru makandarasi waliotekeleza mradi na kuanza kuwanufaisha wananchi, huku akionesha ilivyokuwa ngumu.
“Tulikuwa na kazi kubwa ya kusukumana, kusutana, kushitakiana lakini baadaye tulielewana kazi iliendelea na mradi huu umekamilishwa nashukuru sana,” amesema.

Magumu mengine aliyoyapitia, ni shinikizo la kukamilisha mradi huo alilolipata kutoka kwa Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya akisema ameonana naye mara tatu akimsisitiza kuhusu kukamilisha Same-Mwanga-Korogwe.
“Mara ya kwanza alikuja kuniona nikajua kwa sababu mpya, anakuja kunipa ABC za kuwa Rais kwa hiyo alikuja nikampokea mzee wangu tukazungumza na akanieleza shida yake zilikuwa mbili.
“Moja mradi huu (Same-Mwanga-Korogwe) lakini pili ni ile barabara mnayoita Msuya Bypass. Tukakaa baada ya muda nikatembelea Same-Mwanga-Korogwe nikapita kumsalimia, maneno yake yalikuwa yale yale barabara na mradi.

Rais Samia Suluhu Hassan leo Jumapili, Machi 9, 2025 amezindua mradi wa maji wa Same -Mwanga – Korogwe katika mikoa ya Kilimanjaro na Tanga. Uzinduzi huo uliofanyika Mwanga mkoani Kilimanjaro, pia umeshuhudiwa na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso na Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya.
Amesema Msuya alimfuata tena Ikulu ya Chamwino Dodoma na kumweleza kuhusu mradi huo na alimwahidi maji yangeanza kutoka Juni mwaka jana, jambo lililotimia.
“Lakini mradi huu ulisuasua kwa muda mrefu sana, lakini mimi siamini kwenye kushindwa, nikamwambia Waziri (wa Maji-Jumaa Aweso) na Waziri wa Fedha, (Dk Mwigulu Nchemba) huu mradi lazima tuumalize,” amesema.
Amesema wasaidizi wake akiwamo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa mara kadhaa alitembelea mradi huo na hata Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango alitoa maelekezo mazito kuhusu Same-Mwanga-korogwe.
“Sasa fahari yangu leo ni hatimaye mradi huu umekamilika na nimerudi hapa kuja kuzindua mradi huu, lakini furaha yangu ni kwamba wananchi wameshaanza kutumia maji yatokanayo na mradi huu,” amesema Rais Samia.

Pia, mradi huo uliwahi kuweka rehani wadhifa wa Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango aliyeahidi kuacha kazi, iwapo mambo yasingeenda kama ilivyopangwa.
Katika ziara yake alipotembelea mradi huo, Machi 21 2024, Dk Mpango, alisema hayuko tayari kurudi kwa Rais Samia kumweleza maji hayatoki.
“Kila mtu atimize wajibu wake, kurudi kwa Rais mimi kwamba maji hayatoki…mimi nitaacha kazi, kama maji hayatoki hapa sasa na mimi nikiacha kazi hao wengine sijui, Katibu Mkuu na waziri wake mimi sijui,” alisema.
Waziri Mkuu, Kassima Majaliwa yeye alifanya ziara katika miradi huo si chini ya mara moja na alipoutembelea alikuwa akitoa maelekezo mbalimbali.
Wakati Rais akieleza hayo, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema wapo watendaji waliofukuzwa kazi na wengine kulala polisi wakati wa utekelezaji wa mradi huo, ikiwa ni sehemu ya magumu yaliyopitiwa.
Amesema alipoteuliwa katika Wizara ya Maji, jambo la kwanza aliloambiwa ni kuhusu mradi huo, vivyo hivyo la pili na tatu.
“Nakumbuka siku moja tulikuwa kwenye kipindi cha kurasa nilikuwa nazungumza mafanikio ya sekta, mradi huu niliukwepa kidogo, ulipiga simu mubashara (Rais Samia) ukasema waziri wangu umeongea vizuri lakini Same-Mwanga-Korogwe sijakusikia naomba uende ukatekeleze wananchi wakapate maji,” amesema.

Katika maelezo yake, amekumbushia magumu mengine akisema mradi huo uliwatesa hata viongozi wakuu akiwamo Dk Mpango aliyeahidi kujiuzulu.
“Alikuja hakuwa na maneo mengine alitwambia, wana-Mwanga, wana-Same na Korogwe wanachohitaji maji na mkishindwa kuleta maji hadi Juni mimi nitajiuzulu, nikasema sasa nishaliwa kichwa.
“Kila mkeka ukitoka tunachungulia, lakini kwa dhati ya moyo hakuna jambo nililojifunza kama uvumilivu, umetuvumilia hadi kazi tumeimaliza,” amesema.
Katika kusisitiza magumu hayo, Aweso amesema kazi haikuwa rahisi kwa sababu wapo watendaji waliofukuzwa kazi na wengine wamelazwa polisi na ametumia jukwaa hilo kuwaomba radhi wote waliokwazana nao kwa shughuli hiyo.
“Ilikuwa kwa nia njema kuhakikisha maelekezo ya Amiri Jeshi Mkuu yanatekelezwa,” amesema.
Amesema waliwahi kwenda kwa Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya kutaka historia ya mradi na aliwaeleza kwa kina.
Sambamba na hilo, amesema ulifika wakati hadi alikuwa akipishana na wabunge wa maeneo yatakayonufaika na mradi huo lakini sasa umekamilika na anawashukuru.
“Tumezungumza na viongozi wa kimila, mheshimiwa Rais hapa hadi matambiko yamefanyika kuhakikisha mradi unakamilika,” amesema.
…kukomesha ubambikizaji maji
Katika hotuba yake hiyo, mkuu huyo wa nchi, amemtaka Aweso kuhakikisha zinapatikana mita za maji zitakazomwezesha mwananchi kulipia kwanza huduma ndipo atumie ili kiasi cha fedha atakacholipa kiendane na maji atakayotumia.
“Mkiwawekea zile mita za tumia tu, wanatumia wanavyoweza, wanamwagia mbogamboga ukimpelekea bili atasema unambambikia bili, kwa hiyo jitahidi upate zile mita za kulipia kwanza ndipo utumie maji ili maji yalipwe ipasavyo,” amesema.
Maelekezo yake hayo yanaendana na kile alichosisitiza kuwa, baada ya kukamilika kwa mradi huo, ni muhimu wananchi wasibambikiwe bili.
Pia, amewataka maofisa wa mamlaka za maji katika maeneo ya mradi huo, waharakishe kuwaunganishia wananchi huduma kwa sababu Serikali ilikopa fedha za kutekeleza mradi na ili zirudi inahitaji huduma iunganishwe na fedha zikusanywe na mkopo ulipwe.
“Jinsi mtakavyowaunganishia wananchi wengi na ndivyo tutakavyoweza kukusanya fedha zaidi na tunaweza kulipa mkopo wetu,” amesema.
Rais Samia amesema zimetumika gharama kubwa kupata maji hayo, hivyo kila tone litakalotumika lina gharama zake kubwa.
“Ndiyo maana hatuhamasishi sekta binafsi kuingia kwenye miradi ya maji kwa sababu malipo yake yatakuwa makubwa mno, Serikali tunaleta miradi ya maji, tunatoa ruzuku ya kutosha, ruzuku kubwa sana ili wananchi wapate maji,” amesema.
Ametumia hoja hiyo kuwahamasisha wananchi watakaotumia maji hayo walipie ili Serikali irudishe mkopo na ipate mingine kugharimia shughuli nyingine za maendeleo.
Baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza ya mradi huo, Rais Samia amesema uwezo wa kuzalisha maji umeongezeka kutoka lita milioni 3.7 hadi milioni 6 kwa siku na kutosheleza mahitaji ya mji na wananchi wanaofikiwa kutoka 50,615 hadi 300,000 kwenye vijiji 38.
Amesema huduma ya maji iliyopatikana kwa saa chache kwa sasa yanapatikana saa 24 kila siku.
“Hiyo ndiyo taarifa niliyonayo wananchi, kama ni uongo mtakuja kuniambia nijue vya kushughulika na Waziri (wa Maji- Jumaa Aweso),” amesema.
Amesema kati ya vijiji 14 ni vinne pekee ndivyo vilivyounganishiwa maji hadi sasa na amemtaka Aweso kuingiza vingine 10 viingizwe kwenye mpango haraka.
“Hawa wanaozungumzwa na Bwawa la Nyumba ya Mungu ni wadau muhimu na tunawategemea kutulindia chanzo chetu, sasa kama maji yanawapita watakosa moyo wa kulinda, niombe sana wapatiwe maji kwa haraka ili waendelee kulinda kile chanzo,” amesema.
Amesema anatambua mamlaka ya maji ya Same-Mwanga tayari imeshaunganisha kaya zaidi ya 1,500 tangu Julai mwaka jana na kuwataka waongeze kasi kwa kuwa miundombinu imetandikwa mingi.
Kwa upande wa wananchi wa Korogwe, Rais Samia amesema watafikiwa na huduma ya maji katika awamu ya pili ya mradi huo, huku akisisitiza umuhimu wa kuwepo uendelevu wa huduma.
Hata hivyo, amesema wakati wa upembuzi yakinifu wa mradi huo, kulibainika viashiria vya hatari inayoweza kujitokeza, akitaka vifanyiwe kazi.
“Vile viashiria vya hatari mvifanyie kazi, ile hatari iliyotarajiwa ingetokea kama havifanyiwi kazi basi zisitokee ili huduma hii iendelee,” amesema Rais Samia.
Awali, akitoa taarifa ya mradi huo, Katibu Mkuu, Wizara ya Maji, Mwajuma Waziri amesema mradi huo unatarajiwa kuvihudumia vijiji 38 kati ya hivyo, 17 vipo wilayani Mwanga, 16 Same, Kilimanjaro na vitano wilayani Korogwe mkoani Tanga.
Katika vijiji hivyo, amesema wananchi 456,931 watafikiwa na huduma hiyo ya maji kulingana na usanifu wake na kwamba lita milioni 103.65 zitazalishwa.
Mgawanyiko wa lita hizo, amesema milioni 60.2 kwa ajili ya Same, milioni 40.2 kwa ajili ya Mwanga na milioni 3.3 kwa ajili ya vijiji vya Korogwe.

Katika kuutekeleza mradi huo, amesema Serikali ilipata mkopo kutoka taasisi mbalimbali ikiwao Kuwait Fund na Saudi Fund.
“Kazi zilizofanyika ni ujenzi wa chanzo cha kuzalisha lita milioni 103, mtambo wa kusafisha maji lita milioni 51.65, ulazaji wa bomba kuu la kusafirisha maji kilomita 81.8 na kulaza bomba la kusambaza maji megawati 16 na matanki saba ya kuhifadhi maji kuanzia lita 300,000 hadi milioni tisa,” amesema.
Katika taarifa yake hiyo, amesema vijiji tisa vya Njiapanda, Kisangara, Lembeni, Mbambua, Kiruru, Kiverenge, Mgagao, Njoro na Ishinde vimeanza kupata maji.
Amesema taratibu za kuhakikisha wananchi wa vijiji vilivyobaki wanapata maji zinaendelea.
Imeandikwa na Juma Issihaka (Dar), Janeth Joseph na Florah Temba (Mwanga)