KATIBU Tawala wa Mkoa wa Tabora Dkt John Rogath Mboya ameishauri Mamlaka ya Maaabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) kujenga maabara ndogo ya uchunguzi katika mkoa huo ili kusaidia mikoa ya kanda hiyo kupata huduma za uchakataji wa sampuli au vielelezo kwa haraka na kwa wakati na kuondoa changamoto ya kufuata huduma hiyo umbali mrefu.
Dkt Mboya amesema hayo wakati akizungumza na wadau wa mnyororo wa haki jinai wakiwemo askari Polisi, Mahakimu, waendesha mashtaka, maafisa ustawi wa jamii na madaktari wa wilaya zote za mkoa wa Tabora waliokuwa wakielimishwa namna sahihi ya uchukuaji,uhifadhi, usafirishaji na uchakati wa sampuli katika maabara ya mkemia mkuu wa Serikali ambapo akasema kwa sasa wanafuata huduma hiyo kati ya mikoa ya Dodoma na Mwanza.
Kiongozi huyo amesema matukio mengi yanayojitokeza yanahitaji ushahidi wa kisayansi kuthibitisha ukweli wa namna yalivyotokea hivyo kama huduma itasogezwa jirani itasaidia mchakato mzima wa uchukuaji,uhifadhi, usafirishaji na uchakataji wa sampuli kufanyika kwa haraka na majibu kutolewa kwa haraka ili haki iweze kutendeka kwa wakati.
Hata hivyo akasema kusafirisha sampuli hadi mbali kunaweza kusababisha kuharibika njiani ama vinginevyo ndio maana tunaomba hata tuletewe maabara ndogo na tukio tayari kutafuta eneo, kwani majibu ya kisayansi ni muhimu sana na yanaondoa utata kwenye mashauri ya jinai”Alisema Dkt Mboya.
Katibu tawala huyo wa Mkoa akawataka wadau hao kuzingatia elimu sahihi ya uchukuaji,uhifadhi, usafirishaji na uchakataji wa sampuli ili kuleta haki katika mlolongo mzima wa haki jinai ili ziwe salama kabla ya kuziwasilisha katika maabara ya mkemia mkuu wa Serikali kwaajili ya uchunguzi wa kimaabara bila kuathiri ubora wake.
“Kuna mambo kisheria ya kuboresha kama maboresho ya sheria na kanuni lakini yapo ya moja kwa moja yanayotuhusu sisi wadau wa mnyororo wa haki jinai,na mambo haya ni ya kitaalamu tunapaswa kujipanga kuboresha shughuli zetu hasa za kuchukua,kuhifadhi na kupeleka sampuli katika eneo linalohusika na hukumu ikitoka isiache shaka na haki iweze kutendeka”Alisema Katibu Tawala huyo wa Mkoa wa Tabora.
Dkt Mboya akasema mahakimu hawawezi kufikia tamati nzuri ya kutoa hukumu mahakamani kama bado kuna shaka ya upelelezi hasa eneo moja kushindwa kutimiza wajibu wake wa kupeleka ushahidi na vielelezo kwa wakati ama majibu yanayotegemewa kuwa na dosari hivyo kumtaka kila mmoja aliyeko kwenye mnyororo wa haki jinai kutambua wajibu wake ili haki iweze kutendeka.
Naye Meneja wa ofisi ya kanda ya kati Dodoma katika Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Gerald Meliyo Moleli, akasema licha ya ofisi hiyo ktuoa majibu kwa wakati na kuweka tayari ripoti kwa wakati bado kuna changamoto kwa Jeshi la Polisi kuchukua ripoti hizo imekuwa ni changamoto.
Akasema katika kuondoa changamoto ya ucheleweshaji wa majibu, kila ijumaa wamekuwa wakiandaa Orodha ya ripoti zilizokwisha na kupeleka kwa DCI (Ofisi ya Mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya Jinai) ili wawaambie watu wao nchi nzima wafuate matokeo ama majibu kutoka maabara ya mkemia mkuu wa Serikali, tunachowaomba Polisi wawe wanafuatilia majibu kwa wakati kwani yamekuwa yanatoka kwa wakati.
“Tunamshukuru sana Rais Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kuwezesha mamlaka ya Mkemia mkuu wa Serikali kufanya uchunguzi wa sampuli mbalimbali kwa hali ya juu na kwa ubora na kutoa matokeo sahihi ya kiuchunguzi kwa kuhakikisha kuna mitambo ya kisasa ya hali ya juu ya kiuchunguzi vipimo vya hap ahata ukipeleka kwenye maeneo mengine yenye mitambo ya kisasa duniani majibu yatafanana”Alisema Meliyo.
Akasema wadau hao wa haki jinai wanapaswa kuhakikisha sampuli zinazochukuliwa na kufikishwa katika maabara hiyo zinazingatia utaalamu na weledi wakati wa kuzichukua kuzitunza, kuzisafirisha na hatimaye kuweza kuzichakata katika maabara ya Mkemia mkuu wa Serikali.
Meneja huyo wa kanda ya kati Dodoma kutoka GCLA akasema wameendelea kuwajengea uelewa wadau hao ili kuhakikisha wanafanya kazi yao kwa weledi na kuzingatia usimamizi mzuri ili utendaji wao uwe na ufanisi katika utoaji wa haki mahakamani.
“Tunataka uchukuaji wa sampuli ufanyike kwa usahihi na kutosheleza mahitaji ili kesi zisichelewe mahakamani na watu wapate haki stahiki ikiwemo watuhumiwa wasio na makosa kuondolewa hatia na walio na makosa kuhukumiwa kihalali kwa kufuata taratibu za uchunguzi wa kisayansi”Alisisitiza
Kwa upande wake Msaidizi wa Mkuu wa uchunguzi wa kisayansi mkoa wa Tabora, Mkaguzi msaidizi wa Polisi Omary Matesa, akizungumza kwa niaba ya washiriki alishukuru kwa elimu waliyopewa kwani imeendelea kuwajengea uwezo zaidi katika majukumu yao .
“Kupitia mafunzo haya ipo haja kwa wadau wote wa mnyororo wa haki jinai kuwa na ushirikiano wa karibu ili kusaidiana kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati hasa kwenye ukusanyaji,uhifadhi, usafirishaji na uchakati wa sampuli kwani kila mmoja ana wajibu wake katika hatua hizo zote muhimu za kiuchunguzi”Alisema Mkaguzi msaidizi huyo wa Polisi.