Kinshasa. Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imetangaza zawadi ya Dola 5 milioni za Marekani (Sh13 bilioni) kwa mtu atakayetoa msaada utakaofanikisha kukamatwa kwa viongozi wakuu wa kundi la wapiganaji wa M23.
Viongozi hao ni Rais wa M23, Bertrand Bisimwa, Jenerali Emmanuel Sultani Makenga ambaye ni Kamanda wa kijeshi wa waasi na Corneille Nangaa ambaye ni mratibu wa Muungano wa Makundi ya Waasi wa Alliance River Congo (AFC/M23).
Katika taarifa iliyotolewa jana Jumamosi Machi 8, 2025 na Waziri wa Sheria wa DRC, Constant Mutamba, viongozi hao wanatafutwa na mfumo wa haki wa DRC kwa tuhuma za ugaidi.
Mutamba pia alitangaza zawadi ya Dola4 milioni (Sh10.4 bilioni) kwa yeyote atakayetoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa washirika wawili wa M23 waliokimbilia mafichoni, Perrot Luwara na Irenge Baelenge.
Mutamba alisisitiza Serikali ya DRC itahakikisha malipo na ulinzi kamili wa utambulisho na taarifa binafsi kwa wale watakaosaidia kukamatwa kwa viongozi hao wanaosakwa kwa udi na uvumba.
Kulingana na Mutamba, maofisa kadhaa waandamizi wa Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (FARDC) wamekamatwa na mchakato wa kuwafungulia mashtaka unaendelea kwa tuhuma za kuziacha nafasi zao na kusababisha waasi hao kuiteka miji mikubwa ya Mashariki mwa DRC.
Pia, amesema maofisa hao wakati wa kutoroka mapigano waliacha silaha, risasi, vifaa vya kijeshi na majeruhi hasa katika miji ya Goma na Bukavu, ambayo kwa sasa iko chini ya udhibiti wa AFC/M23.

Mapigano kati ya waasi wa M23, Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (FARDC) na muungano wa waasi wa AFC/M23 yalitokea Ijumaa katika vijiji vya Lwanguba, Kanii, Kivuye na karibu na Parokia ya Masisi eneo la Masisi, Mkoa wa Kivu Kaskazini.
Waasi wa M23 waliteka mji wa Goma Januari na tangu wakati huo wameendelea kusonga mbele wakiteka maeneo zaidi ya Jimbo la Kivu Kusini nchini humo ikiwa ni pamoja na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Goma, Uwanja wa Ndege wa Kavumu na Mji wa Bukavu, Mkoa wa Kivu Kusini.
Tangu machafuko ya M23 yalipoanza tena mwaka 2022 yakiongozwa na Bertrand Bisimwa na Emmanuel Sultani Makenga, Serikali ya DRC, mara kwa mara imeishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23 madai ambayo Rwanda na M23 wameyakanusha.
Hata hivyo, Rais Paul Kagame wa Rwanda alipofanya mahojiano na CNN alikanusha kuwaunga mkono waasi hao huku akiishutumu Serikali ya Rais Felix Tshisekedi kwa kuwaunga mkono wa wapiganaji wa jamii ya Kihutu wa Kundi la FDLR wanaolenga kuteteresha amani ya Rwanda.
Pia, Serikali ya Rwanda inadai kuwa wapiganaji hao wa FDLR wanaodaiwa kutumiwa na Serikali ya Tshisekedi walihusika kwenye mauaji ya kimbali ya mwaka 1994 nchini Rwanda yalioacha makumi kwa maelfu ya raia wakiwa wamefariki dunia.
Waasi wa M23 wanasema mapambano yao yanahusu kupinga ufisadi, chuki dhidi ya wageni na ubaguzi ndani ya uongozi wa DRC.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.