Ninaposema mfanyakazi si lazima aliyeajiriwa na kusubiri mshahara wa mwisho wa mwezi, kuna wale ambao wamejiajiri wakifanya shughuli za hapa na pale zinazowasaidia kuendesha maisha yao na familia zao kwa ujumla.
Awali kundi hili halikuwa kubwa, zamani jukumu kubwa lilikuwa kuhudumia familia, baba akienda kutafuta mama anabaki nyumbani kuangalia watoto na kuhakikisha kila kitu kinakwenda. Kwa kiasi kikubwa huo ndiyo ulikuwa mgawanyo wa majukumu.
Mambo yamebadilika sasa, siku hizi ni kawaida sana kukuta baba na mama wote wanafanya kazi hivyo wanalazimika kutoka nyumbani na kuacha baadhi ya majukumu yao kwa watu wengine.
Hapo kwenye kuacha majukumu ndipo ninapotaka kuweka mjadala wangu kulingana na madini niliyopata jumla hili niliposhiriki kongamano la maadhimisho ya siku ya wanawake lililoandaliwa na Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu (THTU) tawi la Chuo Kikuu Ardhi.
Tofauti na makongamano mengi ya wanawake niliyowahi kuhudhuria, nina uhakika kila mwanamke aliyehudhuria kwenye kongamano hili hakutoka kama alivyoingia labda awe aamue kushupaza shingo.
Nasema tofauti kwa sababu halikuwa kongamano la kuoneshana mishono ya sare, makeup, nywele au nani kapendeza zaidi bali naweza kusema ilikuwa jukwaa la kuwakumbusha wanawake majukumu yao na nafasi yao katika familia.
Mtoa mada Bupe Mwabenga aliwakumbusha wanawake kutenganisha muda wa kazi na muda wa maisha binafsi yanayohusisha familia bila kusahau jukumu lao la msingi ambalo ni malezi, hii haina maana kwamba mwanamke hatakiwi kufanya kazi la hasha lakini anapaswa kutambua msingi wa malezi kwenye familia ni mama.
Inawezekana mama unatumia muda wako mwingi kwenye kazi kwa sababu wewe ndiyo unawezesha familia kupata mahitaji yote ya msingi, bado hiyo siyo sababu wa kushindwa kusimama kwenye nafasi yako kama mke au mama.
Bube ambaye kitaaluma ni mwanasaikolojia anasema kuna wanawake kwa sababu wao ni wafanyakazi basi wanashindwa kutenganisha muda wa kazi au shughuli zao za utafutaji na maisha ya familia.
“Unakuta mwanamke anafanya kazi hadi saa 12 jioni, anaanza safari ya kurudi nyumbani kutokana na foleni inawezekana akatumia saa moja hadi mbili kufika nyumbani. Akifika nyumbani moja kwa moja chumbani anapanda kitandani na laptop kazi zinaendelea.
Sio kwamba hutakiwi kufanya kazi lakini ni lazima ujue kutenganisha muda wa kazi na familia, inawezekana watoto wako ukawapa kila kitu lakini kama hauna muda nao ni kazi bure. Unaweza kutumia muda mwingi kutafuta hela na usizifurahie kwasababu unapaswa kufurahi nao unawaumiza,”
Maneno haya hadi sasa yanazunguka kichwani mwangu, nina uhakika iko hivyo kwa kila mwanamke ambaye alipata fursa ya kumsikiliza kwa makini na kumuelewa mwanasaikolojia huyu.
Kutokana na uhalisia wa maisha ya sasa, wengi tunatumia muda mwingi kwenye utafutaji na kusahau kwamba kuna watu wanatukosa, kwa upekee hapa niwazungumzie watoto.
Inawezekana wanakuhitaji sana lakini hawana uwezo wa kuhoji na hata ikitokea wamehoji wanapewa majibu yasiyojitosheleza.
Ujumbe ule nimeubeba name nimeona nije kuwashirikisha wanawake wengine wapambanaji watambue kwamba ni jambo jema sana kutafuta kwa ajili ya familia lakini ni lazima tujifunze kutenganisha muda wa kazi na muda wa familia.