Umemuandaaje mtoto wa kiume kuwa mtu bora?

Bwana Yesu apewe sifa, karibu katika tafakari ya ujumbe wa leo. Ninayekuletea ujumbe huu ni mtumishi wa Mungu, Mwalimu Peace Marino kutoka Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Ebeneza Nyashimo Jimbo la Kaskazini Busega.

Tumekuwa na wiki ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani (IWD) iliyoambatana na mikutano kadhaa ya makanisa.

Jumamosi Machi 8, 2025 ilikuwa kilele cha maadhimisho ambayo kitaifa yalifanyika mkoani Arusha. Kipekee niwashukuru kina baba kwa kutuvumilia wiki hii na kuturuhusu kuungana na wanawake wenzetu kuadhimisha siku yetu, tunatambua na kuthamini mchango wenu katika kufanikisha mambo yetu. Mwenyezi Mungu awabariki.

Ujumbe tuliopewa leo unasema: “Umemuandaaje mwanao wa kiume kuwa mtu bora?”

Jamii nyingi zimekuwa zikimthamini mtoto wa kiume na kumpa hadhi kubwa na kusahau kuwa anahitaji mafunzo yatakayomsaidia kuwa bora katika jamii, kwenye kanisa na Taifa kwa ujumla.

Efeso 5:23b inasema: “Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe kama Kristo naye ni kichwa cha kanisa.”

Tumetumia muda mwingi kumfundisha mtoto wa kike na kusahau hiki kichwa (mume) kinatakiwa kufunzwa ili kifananie na Kristo kwa maana nyingine, tabia za Kimungu zionekane ndani ya mwanaume.

Tito 2:3-4. Inazungumza kwa habari ya wazee wa kike kufundisha mema na kuwapa maarifa wanawake, vijana ikiwa ni pamoja na kuwa na kiasi, kuwa safi, kufanya kazi, kuwa wema, kuwatii waume zao, kuwa wavumilivu na mambo mengine mengi. Jamii na kanisa tumejitahidi kutimiza jukumu hili.

Watoto wa kike wanapokosea tunawawajibisha kwelikweli na hakuna mama au baba anayetaka binti yake aharibikiwe, hivyo jicho la baba na mama liko kwa mtoto wa kike. Wakati mwingine hatujawapa nafasi ya kujieleza kwa nini amekosa au ameingia kwenye changamoto fulani badala yake huwa tunawaadhibu bila hata kujua chanzo cha tatizo. Tunafanya yote haya kwa sababu ya kuogopa kupata aibu.

Naomba nikuulize mpendwa, hivi nguvu unayotumia kumlinda binti yako ni sawa na unayotumia kumlinda mwanao wa kiume? Kwa nini binti akichelewa kurudi nyumbani anaadhibiwa vikali lakini kijana wa kiume hata aingie usiku jamii inaona ni sawa tu, jambo kama hili siyo sawa kwani halimuandai mwanao wa kiume kuwa bora.

Tito:2:6 inasema: “Vivyo hivyo na vijana waume uwaonye kuwa na kiasi.” Katika hili tunahitaji rehema ya Mungu kwani tumesahau kabisa kuwa tunalo jukumu la kuwasaidia watoto wa kiume na kama tunafanya ni kwa kiasi kidogo. Hatuna budi kuamka na kulichukulia jambo hili kwa uzito ili kunusuru kizazi chetu.

Paulo anamwambia Timotheo kuwa: “Naikumbuka imani uliyonayo isiyo na unafiki, ambayo ilikaa kwanza katika bibi yako Loisina katika mama yako Eunike, nami nasadiki wewe nawe unayo.”

2 Timotheo 1:5: “Kina mama hawa walimfundisha kijana wao na kumrithisha imani akakua nayo na hakuiacha.” Wewe unawarithisha nini wanao, nani anajivunia wanao kutokana na jinsi ulivyowafunza vizuri?

Tupate wapi kina baba kama Ayubu tusipowafundisha? Tupate wapi kina baba ambao Mungu anajivunia tusipowafundisha? (Ayubu 1:5) inasema: “Ayubu aliamka asubuhi na mapema akasogeza sadaka kwa hesabu ya watoto wake wote akisema yamkini hawa wanangu wamefanya dhambi na kumkufuru Mungu mioyoni mwao.”

Tuna kina baba wangapi katika jamii zetu wanaokumbuka kutoa sadaka kwa ajili ya watoto wao au hata kufunga na kuomba kwa ajili ya watoto wao na uzao wao?

Kila binti anatamani kuolewa na kijana mwenye hofu ya Mungu ndani yake. Hiyo hofu ya Mungu ataitoa wapi ikiwa hakuna wa kumfundisha? Wazazi tumekataa wachumba ambao mabinti zetu wametuletea kwa sababu tuliwaona hawana hofu ya Mungu ndani yao, kama hujaweza kumfundisha mwanao wa kiume ili afae kuwa mume wa binti fulani kina nani watamfundisha mkweo?

Binti akibeba mimba nje ya utaratibu ni kosa lisilo sameheka, mama itabidi utoe maelezo ya kutosha kwa baba yake limetokeaje jambo hilo. Mabinti wengine wamepigwa, wengine wamefukuzwa na maisha yao yakaharibika kabisa lakini vipi kama kilichompata ni kama kile kilichompata Dina (Mwanzo 34) na Tamari (2 Samweli 13:1-14) mabinti hawa walibakwa.

Wakati mwingine mabinti zetu wanapitia changamoto nyingi na ngumu na hawana namna na wapi pa kusemea. Ni lini baba au mama umekaa na binti yako na kutaka kujua anapitia changamoto gani?

Jambo kama hili linapotokea kwa watoto wa kiume hatuoni kama lina madhara linachukuliwa kama la kawaida. Mwanzo 34:8 Shekemu anapomtendea hiana Dina, baba yake Shekemu (Hamori) anakwenda kwa Yakobo kuomba watoto waoane bila hata kujali ni maumivu kiasi gani Dina anapitia. Hatuoni ni wapi Hamori anamuwajibisha mwanaye wa kiume kwa kosa alilolifanya.

Mpendwa dhambi yoyote anayoifanya mwanao wa kiume na ukaifumbia macho ni mbegu unapanda na matunda yake utayaona, Yesu atuhurumie.

Tunapohitimisha ni kusihi umwangalie mwanao wa kiume kwa ukaribu na kumfundisha kama unavyofanya kwa mwanao wa kike ili kila mmoja afae kwa ufalme wa Mungu. Mungu akubariki sana.

Kwa maombi, semina na ushauri: 0783 999 044.

Related Posts