Dar es Salaam. Waombolezaji wameendelea kuhani msiba wa kiongozi na mwanataaluma hayati Profesa Philemon Sarungi, aliyefariki dunia jioni ya Machi 5, 2025 nyumbani kwake Oysteybay jijini Dar es Salaam kwa tatizo la moyo.
Ikiwa siku moja ya kabla ya kupumzishwa kwenye nyumba yake ya milele Jumatatu Machi 10, viongozi mbalimbali wamewasili nyumbani kwa Profesa Sarungi kutoa pole kwa mjane wa marehemu, Veronica, pamoja na familia kwa ujumla.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu aliwasili saa 8:30 mchana kisha kuwasalimia waombolezaji, kusaini kitabu cha maombolezo na kuingia ndani kuonana na mjane wa marehemu.
Wakati Lissu akiwa ndani, dakika 10 baadaye aliyekuwa kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo Zitto Kabwe naye alifika kisha kusaini kitabu cha maombolezo.

Baadaye majira ya saa 9:18 aliwasili Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete naye akaenda kusaini kitabu cha maombolezo kabla ya kuingia ndani kumpa pole mjane wa marehemu.
Alivyotoka Kikwete moja kwa moja akaenda kusalimiana na Lissu, kisha kukaa pamoja na wakaonekana wakizungumza na kucheka kwa dakika kadhaa.

Rais wa awamu ya nne Jakaya Kikwete akisaini kitabu cha maombolezo mara baada ya kuwasili nyumbani kwa hayati Profesa Philemon Sarungi aliyefariki dunia Machi 5 2025 nyumbani kwake Osterbay jijini Dar es Salaam. Picha na Sute Kamwelwe
“Naona uko vizuri bwana…umenenepa kuliko mimi” alisema Kikwete huku akigusa tumbo na wakati huo Lissu akicheka pamoja na waombolezaji waliokuwa karibu nao.
Lissu alisikika anamsalimia Kikwete ‘shikamoo’ na Kikwete akaitikia marahaba na Lissu akamjibu na wewe unaoneka uko vizuri. Kisha wawili hao wakakaa pamoja sawia na waombolezaji wengine na wakaendelea na mzungumzo.
Walichokisema juu ya Sarungi
Akimzungumzia Sarungi Lissu amesema Hayati Sarungi ni mtu wa heshima kulingana na utumishi wake enzi za uhai wake.

“Alikuwa moja ya wazee wetu, wenye heshima kubwa. Profesa Sarungi alikuwa Waziri wa Afya, Elimu, Michezo na Ulinzi, amehudumu maeneo mbalimbali na katika maeneo yote aliyotumika hakuwa na mawaa,” amesema Lissu.
“Ameondoka na kupumzika bila kuhusishwa na uchafu. Ni mtu wa heshima sana,” amesisitiza.
Kwa upande wake Zitto amesema msiba wa Profesa Sarungi ni mkubwa kwake akieleza walivyokutana na kumlea kisiasa wakati anaingia bungeni mwaka 2005.
“Alikuwa ananieleza namba ya kuongea alikuwa ananifunda namna ya kuzungumza alikuwa ananipigia simu wakati wote, tulikuwa tunashauriana naye,” amesema.
“Sijamfahamu kwenye vyombo vya habari bali tumefahamiana ndani bungeni, taifa limepoteza hazina, mwanataaluma, waziri aliyefanya kazi kwa muda mrefu, mkurugenzi na mzee mwenye mambo mengi,” amesema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), Dk Mpoki Ulisubisya amesema katika sekta ya afya Profesa Sarungi ameacha alama kubwa kwani wazo la kuanzisha taasisi hiyo yeye ndiye aliliandika.
“Amesoma shule ya Ikizu ambayo nimesoma na mimi, tunaabudu wote Kanisa la Waadventista Wasabato, alitusaidia mimi na marehemu Faustine Ndugulile akatupatia tiketi za kwenda Afrika Kusini,” amesimulia.
Amesema maisha yake yamezunguka kwenye sekta ya afya na kazi aliyoifanya imeleta mchango kwenye taasisi kufanya mambo makubwa si tu Tanzania, bali hadi nje ya nchi, ikiwemo kubadilisha nyonga, magoti.
Profesa Sarungi (89) ambaye aliwahi kuwa mbunge wa Rorya, alifariki kutokana na maradhi ya moyo na anatarajiwa kuzikwa kesho katika makaburi ya Kwa Kondo Kunduchi wilayani Kinondoni jijini Dar.
Uamuzi wa kuzikiwa Dar es Salaam umetokana na kikao cha familia pamoja na wosia wa marehemu, kwa mujibu wa msemaji wa familia Martin Sarungi.