Wanafunzi wanaodaiwa kumlawiti mwenzao waendelea kuhojiwa

Kibaha. Wanafunzi wawili kutoka Miono, Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani, wanaendelea kufanyiwa mahojiano na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumlawiti mwanafunzi mwenzao wakiwa wanacheza usiku.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase, leo Jumapili, Machi 9, 2025, wanafunzi hao wanadaiwa kutekeleza kitendo hicho hivi karibuni usiku, wakiwa wanacheza jirani na makazi yao.

Kamanda Morcase ameeleza kuwa, mwanafunzi anayedaiwa kulawitiwa anasoma darasa la tatu na ana umri wa miaka 10, huku wanaodaiwa kutekeleza kitendo hicho mmoja akiwa na umri wa miaka 16 na mwingine  miaka 10.

 Amesema wanafunzi hao wanatoka katika shule za msingi na sekondari ndani ya Wilaya ya Bagamoyo, na majina yao pamoja na shule zao yametunzwa kwa usalama wa upelelezi.

“Uchunguzi unaendelea na mara utakapokamilika, tutawafikisha kwenye vyombo vya sheria ili hatua zinazohusika zichukuliwe,” amesema  Kamanda Morcase.

Aidha, kamanda huyo ametoa wito kwa wazazi na walezi kuwa makini na mienendo ya watoto wao, hususan wanapokwenda kucheza ili kuepuka vitendo vya ukiukwaji wa maadili na kuenea kwa vitendo vya ulawiti miongoni mwa watoto.

Samuel John, mkazi wa Kibaha amesisitiza kuwa wazazi wanapaswa kutambua umuhimu wa malezi ni bora, zaidi ya kutoa mahitaji ya msingi kama chakula na mavazi.

“Malezi ni zaidi ya chakula na mavazi, ni maelekezo ya tabia njema kwa watoto na ufuatiliaji wa mwenendo wao,” amesema.

Amesema wazazi wanapaswa kuwa karibu na watoto wao, kuwafundisha maadili mema na kuwaangalia kwa karibu ili kuepuka madhara kama hayo.

Ameongeza kuwa, wakati umefika kwa wazazi kuchukua jukumu la kuhakikisha watoto wao wanapata malezi bora ili kujenga jamii imara na yenye maadili.

Selina John amesema changamoto zinazochangia kuenea kwa vitendo vya ulawiti kwa watoto ni baadhi ya wazazi kutowajibika ipasavyo katika malezi.

“Wazazi wengi wamejikita katika kutafuta kipato pekee, wakisahau kuwa malezi bora ni muhimu, watoto wanajiingiza kwenye vitendo viovu kwa sababu wazazi wao hawajui,” amesema.

Related Posts