Yanga imetoa msimamo mzito ikisema haitakubali kurudiana na Simba kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara namba 184 huku ikidai pointi tatu baada ya mpinzani kushindwa kutokea uwanjani.
Taarifa ya Yanga iliyotoka usiku huu kufuatia kikao Cha Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo iliyokutana kwa dharura imesema haitakubali kurudiana na watani wao hao kufuatia mchezo huo kuzuiwa jana Jumamosi, Machi 8, na Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB).
Kwenye taarifa hiyo Yanga imetoa maazimio matatu ya Kamati yao ya utendaji ikisema inataka kupewa ushindi kama ambavyo timu moja inaposhindwa kutokea uwanjani.
Yanga pia imelitaka Shirikisho la Soka Tanzania TFF kuvunja Kamati ya usimamizi wa ligi iliyo chini ya Mwenyekiti wake Steven Mnguto (Mwenyekiti wa TPLB) na katibu wake Almas Kasongo (Afisa Mtendaji Mkuu TPLB) kwa kile ilichosema kukosa imani na kamati hiyo na kuteua watakaokuwa na nia njema na waadilifu kwa maslahi ya mpira.
Hatua hiyo ya Yanga kuikataa kamati hiyo imesema inatokana na Mnguto mapema jana asubuhi kueleza wazi kwamba hakuna mabadiliko ya mechi hiyo kuahirishwa huku akitaka mashabiki kuendelea kununua tiketi na kwenda uwanjani.
Aidha Yanga pia imeweka wazi kwamba Simba haikutoa taarifa kwenye kikao cha maandalizi ya mchezo huo kilichofanyika kwenye Hoteli ya Spice jijini Dar es Salaam kwamba ingetaka kutumia haki yake ya msingi ya kufanya mazoezi na badala yake iliibuka Ijumaa usiku (Machi 7) ikitaka kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara imewaomba radhi mashabiki wa soka Tanzania kwa kukosa mchezo huo huku ikisema timu yao ilijiandaa kikamilifu kucheza mechi hiyo ambayo ilipangwa kufanyika Jana Jumamosi Machi 8,2025.