Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Collins Leitich mkazi wa Kaunti ya Uasin Gishu nchini Kenya anashikiliwa na polisi nchini humo kwa kosa la kuanzisha kituo cha polisi na kukiendesha kinyemela bila ya idhini ya Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS).
Kwa mujibu wa mtandao wa Tuko wa nchini humo, Leitich alipaka kituo hicho rangi ya polisi ili kionekane ni halali, ingawa mamlaka za eneo hilo zilishitukia ujanja wake na kutoa taarifa polisi juzi Machi 8.
Kwa sasa polisi wamemkamata kwa kosa hilo, huku wakazi wakionyesha kushangazwa kwani wengi wao waliamini kilianzishwa ili kuboresha usalama na wengine wakipongeza ujasiri wake.
Kwa sasa anashikiliwa na mamlaka inachunguza ni muda gani mshukiwa amekuwa akiendesha kituo hicho na iwapo wakazi au hata maofisa wa polisi walikuwa wanafahamu kuwepo kwake.
“Tunachunguza ikiwa kuna ofisa yeyote alijua kuhusu wadhifa huu usio halali na ikiwa kuna watu waliokamatwa huko. Pia tunataka kubaini kama kuna wakazi walitafuta huduma za polisi kutoka kituo hicho.
“Tulishangaa kugundua kuwa kituo cha polisi hakikuwa rasmi. Wengi wetu tulidhani kilikuwa juhudi halali za kuboresha usalama katika eneo letu,” amesema mkazi mmoja, kulingana na ripoti ya Citizen Digital.
Kulingana na Sheria ya Huduma ya Polisi ya Kitaifa ya mwaka 2014, ni Inspekta Jenerali (IG) wa Polisi pekee mwenye mamlaka ya kuanzisha vituo rasmi vya polisi. Sheria hiyo inataka vituo vya polisi visambazwe kwa usawa katika kaunti zote na viwe kama vituo vya kiutawala na vya uongozi wa utekelezaji wa sheria