Gugu maji latishia ufugaji wa vizimba Ziwa Victoria

Mwanza. Ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba ndani ya Ziwa Victoria umetajwa kuwa hatarini baada ya gugu maji jamii ya Salvinia SPP kuendelea kuzaliana kwa kasi.

Gugu maji hilo lililobainika hivi karibuni linazaliana mara mbili hadi tatu kila baada ya siku nane, ndani ya Ziwa Victoria.

Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea eneo la Kigongo-Busisi, moja ya maeneo yaliyoathiriwa na gugu hilo leo Jumatatu, Machi 10, 2025, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Cyprian John Luhemeja, amesema kutokana na kasi ya kuzaliana kwa gugu maji hilo, hata ufugaji wa samaki kwa vizimba uliozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan upo hatarini.

“Kama baada ya siku nane magugu maji haya yanazaliana mara mbili hadi tatu, maana yake hata kazi aliyoifanya Rais Samia mwaka jana ya kuzindua ufugaji wa vizimba ipo kwenye hatari sana,” amesema.

Amesema moja ya sababu za kuzaliana kwa kasi kwa gugu hilo ni uchafu mwingi unaoingia ziwani, hivyo ameagiza halmashauri zinazozunguka ziwa hilo kuanzisha kampeni maalumu ya kufanya usafi kwenye maeneo yao, taka kuzihifadhi kwenye madampo na kuzifanyia urejelezaji au uchomaji.

“Lakini, matokeo ni kwamba hatufanyi usafi wa kutosha, hivyo mvua zinapokuja zinauchukua uchafu na kuupeleka ziwani au baharini. Matokeo yake ni fukwe zetu kugeuka dampo, hali inayoshuhudiwa pembezoni mwa Ziwa Victoria na hata katika ukanda wa pwani ya Bahari ya Hindi, kule Pwani na Dar es Salaam,” amesema.

Viongozi na wataalamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Maji, Kilimo, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na Kagera pamoja na wadau wa mazingira wakiangalia hali ya gugu maji Ziwa Victoria eneo la Kigongo-Busisi. Picha na Saada Amir

Ameeleza kuwa hali ni mbaya kwa kuwa gugu maji hilo limeathiri shughuli za uvuvi na usafirishaji kwa vivuko.

“Hili suala ni kubwa sana, tulikuwa tunafikiri ni dogo. Kwa hiyo, nitoe wito kwa wananchi, sisi kama Serikali tunafanya juhudi kubwa za utunzaji wa mazingira, sasa hata wananchi wanapaswa kuunga mkono,” amesema.

Akizungumzia athari kwa usafiri, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amesema kutokana na vivuko kufanya safari kwa shida au kuharibika kwa sababu ya mimea hiyo, zaidi ya wasafiri 10,000 wanaathiriwa kila siku.

“Ukiwa mbali sana huoni ukubwa wa tatizo, lakini ukiwa hapa ndani, kelele yake ni kubwa sana. Malalamiko makubwa zaidi yanahusu vivuko. Hata jana saa nne usiku, mtu mmoja ananiambia, ‘mkuu, tumekaa hapa tangu asubuhi hadi saa nne usiku tunashindwa kuvuka.’

“Ikumbukwe kwamba kwa siku moja, Kigongo-Busisi wanavuka abiria takribani 10,000. Sasa chukua malalamiko ya watu hao ya kukaa masaa sita hadi saba kwenye kivuko, ihamishie kwa mkuu wa mkoa maana wao wanajua mkuu wa mkoa tu,” amesema Mtanda.

Ameongeza kuwa hata kama gugu hilo likitolewa tani 10 kwa siku moja, kesho linazaliwa tani 30, hivyo hakuna mjasiriamali mwenye uwezo wa kuyadhibiti. Matokeo yake, samaki watakufa na uwekezaji mwingine ndani ya ziwa utaathirika.

“Nafikiri ni jambo zuri Katibu Mkuu wa Mifugo na Uvuvi umekuja, kwa sababu anafahamu kuwa magugu haya yakisambaa na kufika kwenye mradi wa vizimba, maana yake jitihada za Rais Samia na uwekezaji wote uliofanyika ziwani zitakuwa sifuri,” ameongeza.

Viongozi na wataalamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Maji, Kilimo, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na Kagera pamoja na wadau wa mazingira wakiangalia hali ya gugu maji Ziwa Victoria eneo la Kigongo-Busisi. Picha na Saada Amir

Ofisa Mazingira wa Shirika la Usimamizi wa Mazingira na Maendeleo (Emedo), Kitogo Laurence amesema ni wakati wa wadau kushirikiana na Serikali ili kukabiliana na changamoto hiyo.

“Kisayansi, uwepo wa gugu maji unaathiri uzalishaji wa samaki. Samaki wanazaliana kwenye maeneo ambayo yanaathiriwa na gugu maji. Lakini pia, gugu maji linapotanda, wavuvi hawawezi kutandika nyavu zao wala kufanya shughuli zao za uvuvi, tofauti na ilivyokuwa mwanzoni,” amesema.

Mkazi wa Kigongo Feli, Yusuph Ndaki, amesema pamoja na kupata shida ya usafiri, hata kambi ya wavuvi imehama kutoka eneo hilo kutokana na wingi wa gugu maji, hivyo kuathiri biashara zao za mazao ya samaki.

Msimamizi wa Mitumbwi Kigongo, David Vitalis, amesema upatikanaji wa samaki umekuwa changamoto kwa kuwa samaki hufuata lilipo gugu maji, lakini wavuvi hawawezi kuwafuata huko kuvua.

Kwa upande wake mkazi wa Mkuyuni, jijini Mwanza, Monica Kamwina, amesema: “Haya magugu yameleta usumbufu sana kwetu sisi abiria. Unajikuta unatumia gharama kubwa kuvuka, lakini bado unakaa hapa kusubiria gari nalo livuke kwa awamu nyingine, wakati wewe umewahi kuvuka.”

Baada ya ziara ya kujionea hali halisi ya uwepo wa gugu maji hilo, viongozi wa Serikali akiwemo Luhemeja, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Riziki Shemdoe, wataalamu kutoka Nemc, Wizara ya Uchukuzi, Wizara ya Maji, Wizara ya Kilimo, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na Kagera pamoja na wadau wa mazingira wamejifungia kujadiliana mikakati ya kulidhibiti.

Related Posts