Jeshi la Zimamoto kuajiri watumishi wapya 1,000

Morogoro. Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Juma Mkomi, amesema katika bajeti ijayo Serikali imepanga kuajiri watumishi wapya 1,000 wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini.

Mkomi amesema hayo leo Jumatatu, Machi 10, 2025, wakati akifungua kikao cha Baraza Dogo la Wafanyakazi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kilichofanyika mkoani Morogoro.

Pia, amelitaka jeshi hilo kuziwajibisha ofisi zote ambazo hazitakuwa na vifaa vya kuzimia moto, kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume na sheria za zimamoto.

Amesema kwenye bajeti ya mwaka 2025/2026 Serikali imepanga kuajiri watumishi 1,000 kwenye Jeshi la Zimamoto na Uokoaji. Pia, amelitaka jeshi hilo kufuata utaratibu wakati wa kufanya mchujo wa kuwapata watumishi wapya na kusisitiza vipimo vifanyike kabla ya kuajiri watumishi wapya.

Mkomi, kwenye hotuba yake, pia amelitaka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini kufanya ukaguzi wa vifaa vya kuzimia moto kwenye ofisi za umma ili kuona kama vinafanya kazi ama vimewekwa kama mapambo.

“Ukaguzi huo uende sambamba na utoaji wa elimu ya kutosha kwa umma kuhusu namna ya kuzuia majanga ya moto na kukabiliana nayo. Kitengo cha mawasiliano kwa umma kiongezewe nguvu, kuna mambo mengi yanayohusu Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ambayo wananchi wanapaswa kujua kupitia kitengo hiki,” amesema Mkomi.

Akitoa taarifa ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Kamishna Jenerali wa Zimamoto na Uokoaji, John Masunga, amesema katika mwaka wa fedha 2024/2025 jeshi hilo limetenga zaidi ya Sh6.5 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ikiwemo uendelezaji wa ujenzi wa vituo saba vya kuzimia moto na uokoaji katika mikoa ya Songwe, Simiyu, Kagera, Njombe, Manyara, Katavi, na Geita.

Aidha, katika bajeti hiyo wataweza kununua vifaa vya kuzimia moto na uokoaji, pamoja na uchunguzi na ukarabati wa kituo cha kuzimia moto na uokoaji katika Mkoa wa Morogoro na kuendeleza ujenzi wa majengo mawili ya ghorofa kwa ajili ya makazi ya askari Kikombo, jijini Dodoma.

Kamishna Masunga amesema jeshi lina jumla ya vituo 80 vya zimamoto na uokoaji katika mikoa ya Tanzania Bara, ambapo kati ya vituo hivyo, 56 vipo katika ngazi ya wilaya na 24 kwenye viwanja vya ndege.

“Jeshi lina uhitaji wa vituo vipya 237 katika wilaya na maeneo mengine ili kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi,” amesema Kamishna Masunga.

Amesema utaratibu wa upatikanaji wa mkopo wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 100 tayari umesainiwa Februari 15, 2024, kati ya Serikali na Taasisi ya Abu Dhabi Export Office (ADEX) kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE). Mkopo huo ni kwa ajili ya ununuzi wa vitendeakazi mbalimbali, vikiwemo magari 150 ya kuzima moto na uokoaji, magari 40 ya kubebea wagonjwa, boti 23 za kuzimia moto, na helikopta moja ya kuzimia moto.

Kamishna Masunga ametaja changamoto zinazolikabili Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kuwa ni pamoja na uhaba wa vifaa na vitendeakazi kwa ajili ya utoaji huduma, uchache wa vituo vya kujazia maji ya kuzimia moto, na ujenzi holela katika maeneo mengi hasa mijini, hali inayosababisha askari kushindwa kufika kwa urahisi wakati wa dharura za moto na majanga mengine.

Related Posts