Dar es Salaam. Wakati Serikali ikisema bado inaendelea na uchunguzi wa kesi ya kuua bila kukusudia inayowakabili wanaodaiwa kuwa ni wamiliki watatu wa jengo lililoporomoka Mtaa wa Mchikichi na Congo, eneo la Kariakoo, kesi hiyo imefikisha siku 71 bila upelelezi kukamilika.
Washtakiwa hao, ambao wote ni wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, ni Leondela Mdete (49), mkazi wa Mbezi Beach, Zenabu Islam (61), mkazi wa Kariakoo, na Ashour Awadh Ashour (38), mkazi wa Ilala.
Mdete na wenzake wanakabiliwa na mashtaka 31 ya kuua bila kukusudia katika kesi ya mauaji namba 33633/2024 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Leo Jumatatu Machi 10, 2025, Wakili wa Serikali, Eva Kassa, ameieleza mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Godfrey Mhini, kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.
“Kesi hii imeitwa kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa wote wapo mbele ya mahakama yako na upelelezi wake bado unaendelea, hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa,” amedai Kassa.
Hakimu Mhini, baada ya kusikiliza maelezo hayo, ameahirisha kesi hadi Apriil 10, 2025, itakapotajwa na washtakiwa wakiwa nje kwa dhamana.
Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani Novemba 29, 2024, na kusomewa shtaka hilo.
Hata hivyo, tangu siku hiyo hadi leo, kesi hiyo imefikisha siku 71 bila upelelezi kukamilika.
Washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa yao kinyume na kifungu 195 na 198 cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa Novemba 16, 2024, katika Mtaa wa Mchikichi na Congo, eneo la Kariakoo, isivyo halali walishindwa kutimiza majukumu yao na kusababisha kifo cha Said Juma.
Katika shtaka la pili hadi la 31, washtakiwa hao, siku na eneo hilo, wanadaiwa kusababisha vifo vya watu wengine kadhaa, akiwemo Hussein Njou, Prosper Mwasanjobe, Shadrack Mshingo, Godfrey Sanga, Neema Sanga, Elizabeth Mbaruku, Hilary Minja, Abdul Sululu, Catherine Mbilinyi.
Vilevile, wanadaiwa kusababisha kifo cha Elton Ndyamukama, Mariam Kapekekepe, Elizabeth Kapekele, Hadija Simba, Frank Maziku, Rashid Yusuph, Ally Ally, Ajuae Lyambiro, Mary Lema, na Khatolo Juma.
Pia, wanadaiwa isivyo halali walishindwa kutimiza majukumu yao na kusababisha kifo cha Sabas Swai, Pascal Ndunguru, Brighette Mbembela, Ashery Sanga, Venance Aman, Linus Hasara, Pascalia Kadiri, Issa Issa, Lulu Sanga, Happyness Malya, na Brown Kadovera.