Mwanga. Mkutano Mkuu maalumu wa kumpata Mkuu wa Dayosisi ya Mwanga ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) umeanza, huku macho na masikio ya waumini yakisubiri kuona na kusikia ni nani atakayemrithi Askofu Dk Chediel Sendoro, aliyekuwa mkuu wa dayosisi hiyo.
Mkutano huo, unaofanyika katika Kanisa Kuu Mwanga, unatarajiwa kuwa na wajumbe 135 na umebebwa na neno kuu kutoka kitabu cha Kumbukumbu la Torati 2:3 “Mlivyo zunguka mlima huu vyatosha, geuka na upande wa kaskazini”.
Katika mkutano huo, maaskofu mbalimbali, wakiongozwa na Mkuu wa kanisa hilo, Dk Alex Malasusa, wamehudhuria.
Dayosisi hiyo inafanya uchaguzi wa Askofu ikiwa ni miezi sita imepita tangu Askofu Sendoro afariki dunia kwa ajali na hivyo nafasi hiyo kubaki wazi.
Askofu Sendoro, aliyehudumu kama Askofu wa Mwanga kwa miaka minane, alifariki dunia Septemba 9, 2024, kwa ajali ya gari iliyotokea katika eneo la Kisangiro, Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro, saa 1:30 usiku, baada ya gari alilokuwa akiendesha aina ya Toyota Prado, akitokea Kileo kuelekea nyumbani Mwanga, kugongana uso kwa uso na lori.
Historia inaonyesha kuwa Askofu Sendoro ndiye Askofu wa kwanza wa Dayosisi ya Mwanga aliyeingizwa kazini Novemba 6, 2016, baada ya kuzaliwa kwa dayosisi hiyo mpya iliyotokana na kugawanywa kwa Dayosisi ya Pare.
Juzi, akizungumza na Mwananchi, Katibu Mkuu wa Dayosisi ya Mwanga, Mathias Msemo, amesema mkutano huo utakuwa na agenda moja ya uchaguzi.
Aidha, alisema kwa taratibu zilizopo, Askofu anakaa madarakani kwa miaka 10 na baada ya hapo unafanyika mkutano mkuu ambapo anapigiwa kura ya imani na akishinda anahudumu hadi umri wa kustaafu.
“Kwa taratibu zetu, Askofu anakaa miaka 10, na baada ya miaka hiyo anapigiwa kura ya imani, akishinda anakaa hadi muda wa kustaafu. Na wakati anafariki, Askofu Sendoro alikuwa amekaa miaka minane na alikuwa aende mpaka 2026, ndipo ufanyike mkutano mkuu apigiwe kura ya imani,” alisema Msemo.
Alisema kwa mujibu wa katiba, umri wa kustaafu Askofu ni miaka 65 kwa hiari na kwa lazima ni miaka 70.
Viongozi waliohudhuria katika mkutano huo ni Waziri Mkuu mstaafu Cleopa Msuya, Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Mwanahamis Munkunda, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mwanga, Zahara Msangi, na Mbunge wa Mwanga, Joseph Thadayo.
Kuzaliwa Dayosisi ya Mwanga
Dayosisi ya Mwanga ilizaliwa kutoka Dayosisi ya Pare, ikiwa ni Dayosisi ya 25 ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).
Dayosisi hiyo ilizinduliwa na Askofu Dk Fredrick Shoo Novemba 6, 2016, ikiwa na washarika 26,000, waliokuwa wakihudumiwa na sharika 21 na mitaa 66. Hata hivyo, idadi hii imeongezeka baada ya kuanzishwa kwa sharika na mitaa mingine.
Baada ya kuzaliwa kwa Dayosisi ya Mwanga, Askofu mwanzilishi, Mchungaji Chedieli Elinaza Sendoro, aliteuliwa na kuwekwa wakfu ili kuanza majukumu yake siku hiyo hiyo.
Historia ya Kanisa la Kiinjili katika ukanda wa Pare (Vwasu) inakumbusha kuwa Ukristo ulianza mwishoni mwa karne ya 19, baada ya wamisionari wa Kijerumani kutoka chama cha Misioni cha Kilutheri cha Leipzig (Leipzig Lutheran Missionary Society) kuwasili na kuanzisha kituo cha kwanza cha misioni cha Shighatini–Ugweno. Mchungaji Hans Fuchs alikuwa mmisionari wa kwanza, ambaye wapare walimuita “Bwana Fukudha.”
Alikuwa akitokea kituo cha misioni cha Mamba huko Uchagani, na alifika Shighatini na kuanzisha hema la kwanza katika ardhi ya Pare Julai 11, 1900.
Bwana Fukudha, mbali na kufundisha Neno la Mungu, alianzisha shule ya chekechea iliyolenga elimu ya msingi (KKK–Kusoma, Kuandika, na Kuhesabu); alianzisha pia huduma ya utabibu kwa kujenga zahanati, alitengeneza barabara, alifundisha kilimo cha kisasa, na alisisitiza masuala ya biashara, usafi, na maendeleo ya jamii.
Kwa juhudi za Bwana Fukudha na wenzake, na kwa jinsi wenyeji walivyowakaribisha kwa ukarimu wamisionari hao, neno la Mungu pamoja na maendeleo vilienea kwa haraka na kuwa na athari kubwa katika ukanda wa Pare.
Kwa hakika, historia inadhihirisha kuwa waumini wa Kilutheri wa Mwanga ni sehemu muhimu ya utajiri wa historia ndefu ya ukuaji na mabadiliko ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania.
Kanisa hili lilianzia kama Kituo cha Misioni Shighatini na baadaye kuwa sehemu ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanganyika.
Mwaka 1937, Kanisa la Kilutheri la Tanganyika liliungana, na mwaka 1938, Fungamano la Makanisa ya Kilutheri Tanganyika lilianzishwa. Katika mwaka 1963, Dayosisi ya Kaskazini ya KKKT ilianzishwa, na hatimaye, mwaka 1975, KKKT Dayosisi ya Pare ilizaliwa kutoka KKKT Dayosisi ya Kaskazini. Kwa mwendelezo huu, KKKT Dayosisi ya Mwanga ilizaliwa kutoka KKKT Dayosisi ya Pare mwaka 2016.