Nairobi. Geoffrey Odundo ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji na Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Nation Media Group (NMG).
Akitoa tangazo hilo kwa niaba ya bodi leo Jumatatu, Machi 10, 2025, Mwenyekiti Wilfred Kiboro amesema Odundo anajiunga na NMG ili kuimarisha timu na kuendelea kutekeleza jukumu ambalo NMG inatekeleza katika jamii.
Kabla ya uteuzi wake, Odundo alikuwa Mshauri Mkuu wa CPF Group, na awali alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Soko la Hisa la Nairobi (NSE).
“Nina imani kuwa nategemea msaada wenu katika kumuunga mkono Geoffrey anapojiunga na NMG ili kuimarisha timu yetu katika jitihada zetu za kuendelea kutekeleza jukumu letu kwa jamii tunazozihudumia,” amesema Dk Kiboro.
Odundo ataanza kazi rasmi kama Mkurugenzi Mtendaji kuanzia Aprili 7, 2025.
Richard Tobiko, Mkuu wa Fedha wa NMG, amekuwa akikaimu kama Mkurugenzi Mtendaji tangu Agosti mosi, 2024, kutokana na kustaafu kwa Stephen Gitagama, aliyehudumu NMG kwa miaka 17 katika nafasi mbalimbali.
“Odundo ana uzoefu mkubwa katika uongozi, ikiwemo kutumikia katika nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Soko la Hisa la Nairobi (NSE), ambapo aliongoza ubunifu mbalimbali wa soko na kufikia mafanikio ya kihistoria wakati wa kipindi chake cha utumishi kati ya mwaka 2015 na 2024,” amesema Dk Kiboro katika taarifa.
Odundo ameshika pia nyadhifa nyingine za juu, ikiwemo Mkurugenzi Mkuu wa kwanza na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kingdom Securities.
Ana shahada ya umahiri (MBA) katika Usimamizi wa Kimkakati kutoka Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Marekani, shahada ya awali katika Hisabati na Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Egerton, na vyeti vingi vya kitaalamu.