Kibaha. Kitendo cha baadhi ya maofisa watendaji wa kata nchini kujigeuza kuwa wasuluhishi na waamuzi wa migogoro ya ndoa na ardhi bila kufuata utaratibu, kimeelezwa kinasababisha uvunjifu wa amani katika jamii.
Wahiriki wa mafunzo hayo wskiendelea kufuatilia mada mbalimbali,Picha na Sanjito Msafiri
Kwa mujibu wa kanuni za utendaji zilizopo, maofisa hawa wanaruhusiwa kusikiliza migogoro ya wananchi kwa hatua za awali. Hata hivyo, wanapobaini kuwa suluhu ya migogoro hiyo inaweza kupatikana kupitia mahakama au baraza la ardhi, wanapaswa kuwaelekeza wahusika kwenda kwenye vyombo husika na si kujigeuza kuwa wanasheria.
Hayo yamebainishwa leo Jumatatu, Machi 10, 2025 na mratibu wa mafunzo ya uraia na utawala bora kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Wakili Prosper Kisinini, wakati akitoa mada kwenye mafunzo yaliyofanyika Kibaha, Mkoa wa Pwani.

Mafunzo hayo yamewahusisha maofisa watendaji wa kata pamoja na kamati za usalama za wilaya zote za Mkoa wa Pwani.
“Wakati wa migogoro ya ndoa au ya masuala ya ardhi, maofisa watendaji wanawajibika kusikiliza wananchi na, pindi wanapobaini kuwa suala linahusiana na ndoa, basi wawafahamishe wahusika kwenda maeneo yanayohusika na kama ni ya ardhi, mabaraza ya ardhi yapo, lakini si jukumu lao kushughulikia mpaka mwisho,” amesema Wakili Kisinini.
Ameongeza kuwa Serikali imeweka miundo ya kiutendaji ili kumuwezesha kila mtu kupata haki yake kwa wakati na kuishi kwa amani.
“Kila eneo kuna wasaidizi wa kisheria wanatambulika, hivyo mtendaji anaweza kuwaunganisha wananchi na wawezeshaji hawa ili kusaidiwa na hatimaye kuendelea kuishi kwa amani,” amesema.
Wakili Kisinini amesisitiza kuwa, ikiwa shauri litaendelea kwa muda mrefu, litazalisha mgogoro mwingine ambao unaweza kuzorotesha amani katika jamii, jambo ambalo halikubaliki.
Kwa upande wake, Mratibu Msaidizi wa Polisi, Nicolaus Mhagama, amesema kuwa kutokana na maendeleo ya teknolojia, wanajamii sasa wanapata uelewa mkubwa kuhusu haki zao na wanapohisi kutendewa vibaya, wanajua ni wapi pa kupaza sauti.
Mhagama ameonya kuwa, ili kuepuka migogoro, watendaji wanapaswa kutoa huduma kikamilifu na kwa weledi wa hali ya juu kwa jamii inayowazunguka.
“Serikali imeleta Polisi Kata ili wawepo huko kwa kushirikiana na watendaji, mnapaswa kushirikiana nao katika kubaini vitendo viovu na kuvishughulikia kabla havijaleta madhara kwa jamii,” amesema.

Wahiriki wa mafunzo hayo wskiendelea kufuatilia mada mbalimbali,Picha na Sanjito Msafiri
Ameongeza kuwa ushirikiano na mamlaka mbalimbali ni muhimu ili kuhakikisha utendaji kazi unafanyika kwa wakati, na hivyo kujenga imani kwa jamii.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge, amewashauri maofisa watendaji na wakuu wa usalama wa wilaya zote kuongeza juhudi za utendaji kazi, hasa kwa kuwahudumia wananchi kwenye maeneo yao.
Amesema kufanya hivyo ni kutekeleza agizo la Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye anasisitiza kuwa kipaumbele chake ni kuondoa kero kwa jamii.
Baadhi ya wananchi wameeleza kuwa kuna umuhimu wa maofisa watendaji kupewa mafunzo ya mara kwa mara ili kuboresha utekelezaji wa majukumu yao kwa jamii hasa katika kutatua kero mbalimbali na kubuni miradi ya maendeleo.
Elizabeth Yohana, mmoja wa wananchi hao, amesema kuna umuhimu wa kuwapa mafunzo mara kwa mara maofisa watendaji hali itakayosaidia kuwaongezea uwezo na kuwa wazalendo kwa jamii wanayoihudumia.