Arusha. Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imezindua mradi wa kuendeleza kilimo wenye thamani ya Sh31.25 bilioni unaolenga kuongeza uzalishaji wa kilimo na uendelevu wake katika ukanda huo.
Mradi huu wa miaka mitatu, unaojulikana kama ‘Sustainable Regional Agricultural Extension’ (ENSURE), unafadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa lengo la kuimarisha huduma za ugani, kuongeza upatikanaji wa pembejeo, na kujenga uwezo wa nchi wanachama wa EAC katika kukabiliana na changamoto za kilimo zikiwamo wadudu waharibifu na magonjwa yanayovuka mipaka.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo jijini Arusha, leo Machi 12, 2025 Naibu Katibu Mkuu wa EAC anayesimamia miundombinu, sekta za uzalishaji, kijamii na kisiasa, Andrea Aguer Ariik amesema kuwa mradi huu unakuja wakati mwafaka ambapo EAC inalenga mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo.
“Hatuna budi kushukuru kwa ufadhili huu kwani umekuja wakati muafaka ambapo EAC tunafanya mageuzi makubwa katika sekta hii ya kilimo kupitia Mpango wa Maendeleo ya Mfumo wa Pembejeo za Kilimo na Mpango wa Uwekezaji wa Kilimo wa Kanda ya EAC (RAIP),” amesema.
Amesema kuwa ENSURE inatarajiwa kunufaisha zaidi ya watu milioni tano, ikiwemo kuzalisha ajira za moja kwa moja milioni moja huku angalau asilimia 50 ya walengwa wakiwa wanawake.

Amesisitiza kuwa kilimo kinaendelea kuwa nguzo kuu ya uchumi wa EAC, kikitoa ajira kwa zaidi ya asilimia 60 ya wakazi wa ukanda huu, na hivyo ni muhimu kuwekeza katika huduma za ugani ili kuongeza tija na kuhakikisha usalama wa chakula kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Teknolojia za Kilimo kutoka AfDB, Dk Innocent Musyabimana amesema kuwa wanajivunia kufadhili mradi huo utakaotoa uhakika wa chakula katika nchi za EAC.
Dk Musyabimana amesema mradi huo wanautarajia kutatua changamoto kuu za wakulima ikiwemo upungufu wa huduma za ushauri na mafunzo, upatikanaji wa teknolojia na pembejeo za kilimo zinazozingatia mabadiliko ya tabianchi, maarifa na ujuzi wa kutumia pembejeo kwa ufanisi.
“Mradi huu unatarajiwa pia kuboresha upatikanaji wa teknolojia na maarifa ya kilimo kwa wanawake na wanaume ili kusaidia utekelezaji wa sera ya jinsia ya EAC, na kuendeleza ubunifu wa kilimo ambao utaweza kuvutia vijana kushiriki katika shughuli za kilimo, na kuongeza uzalishaji wao na mapato” amesema.