Tanga. Polisi Mkoa wa Tanga limesema linamshikilia kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani humo, Swahibu Mwanyoka kutokana na tuhuma zilizoripotiwa.
Katika taarifa iliyotolewa na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi leo Jumatano Machi 12, 2025 imeeleza uchunguzi unaendelea ili hatua stahiki zichukuliwe kwa mujibu wa sheria.
“Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga linathibitisha kukamatwa kwa Swahibu Juma Mwanyoka kwa tuhuma zilizoripotiwa polisi, uchunguzi unaendelea ili hatua stahiki zichukuliwe kwa mujibu wa sheria,” imeeleza taarifa hiyo ya Kamanda Mchunguzi pasipo kufafanua tuhuma hizo zinahusu nini.
Kada huyo ambaye ni mjumbe wa kamati ya siasa Mkoa wa Tanga taarifa za kupotea kwake ziliripotiwa Ijumaa Machi 7, 2025 kwenye mitandao ya kijamii kwamba amepotea akiwa maeneo ya Royal Village Magomeni jijini Dar es Salaam alikokwenda kuonana na rafiki zake.
Mkazi wa Goba jijini Dar es Salaam, Ashraf Juma ambaye ni kaka wa Mwanyoka amesema ndugu yake alikuwa jijini Dar es Salaam kwa matembezi, akiwa nyumbani kwake aliaga kutoka kwenda kukutana na rafiki zake.
Amesema siku hiyo ya tukio ilikuwa Ijumaa ya Machi 7, 2025 akiwa maeneo ya Royal Village Magomeni ambapo aliongozana na ndugu yake mwingine ndio walikutana na watu waliojitambulisha ni Polisi na walimtaka apande kwenye gari lao.
“Kwamba hawakuwa na uhakika waliomchukua ni polisi hivyo iliwabidi kuanza kufuatilia kwa ukaribu kubaini ni watu gani wamemchukua, wakatoa taarifa Kituo cha polisi Magomeni ambaKo walifungua jalada la uchunguzi na baadaye kuhamishiwa kituo cha Oysterbay kwa ufuatiliaji zaidi,” amesema.
“Mimi ni kaka yake baada ya mimi ndio anafuata yeye, siku ya Ijumaa Machi 7, akiwa hapa nyumbani Goba alinitaarifu kwamba anakwenda mjini kwa sababu gari lake nilikuwa nalo mimi alitaka nimpeleke, kwamba kuna watu anakwenda kukutana nao Mbezi saa tatu asubuhi na nilifanya hivyo, akaondoka na mwenzake na kuishia kupata mkasa huo,” amesema Ashraf.
Anasema baada ya muda mchache alipata taarifa kuna kutoelewana baina ya watu waliomuita Mwanyoka baada ya kutakiwa kupanda kwenye gari, hivyo wakaanza kufuatilia ila simu zake zikawa hazipatikani.
Katibuwa Siasa, Uenezi na Mafunzo wa CCM Mkoa wa Tanga, Samwel Mngazija amekiri Mwanyoka kuwa ni kada wao na wamepata taarifa kuhusu kitu gani kimetokea ila wanafuatilia kujua zaidi na kama taasisi watatoa taarifa kwa umma.
“Hii ni taasisi kwa hiyo inafanyia kazi taarifa rasmi kwani na sisi tumeona kama mlivyoona nyie, kwa hiyo tutakapokuwa tumepata taarifa rasmi na kwa utaratibu wa miongozo yetu tutasema,” amesema Mngazija.