Kariakoo saa 24 yasuasua, kamera na taa vikitajwa

Dar es Salaam. Wakati zikiwa zimepita siku 12 tangu kuanza kwa biashara saa 24 eneo la Kariakoo, bado ufanyaji biashara usiku unasuasua, huku usalama ukitajwa kuwa ndiyo sababu.

Ufanyaji biashara saa 24 ulizinduliwa rasmi Februari 25 na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, katika hafla iliyofanyika Mtaa wa Mkunguni na Swahili, Kata ya Karikaoo jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwamo wakuu wa wilaya  zote za Dar es Salaam na wakurugenzi  wa halmashauri.

Ufanyaji biashara saa 24 ulilenga kuimarisha uchumi wa mkoa, kuongeza mapato ya Serikali na kutoa fursa za ajira kwa wananchi.

Akizungumza na Mwananchi, leo Jumatano Machi 12, 2025 mmoja wa wafanyabiashara aliyejitambulisha kwa jina la Miraji Bilal, anayefanya shughuli zake Mtaa wa Swahili, amesema maeneo mengi hayana mwanga, hivyo wanahofia usalama wao.

“Tuliambiwa kote huku Karikaoo usiku utakuwa kama mchana kwa taa kufungwa, lakini hadi sasa tunaona kimya, hakuna aliye tayari kuweka usalama wake rehani ndio maana unaona mwitikio bado mdogo wa kufanya biashara usiku,” amesema Miraji.

Eshimuni Eliya, mfanyabiashara Mtaa wa Mafia, amesema walitegemea baada ya uzinduzi kila kitu kingekuwa kimekamilika zikiwamo kamera zilizoelezwa zingefungwa kwa ajili ya kuimarisha usalama, lakini hadi sasa hakuna walichokiona.

“Sisi baadhi ya wafanyabiashara tumefunga kamera kwenye maduka yetu, je huyu mteja anapotoka na bidhaa yake kuelekea kutafuta usafiri na kutoka eneo hili la Kariakoo anahakikishiwaje usalama wake, nadhani viongozi wetu walifanyie kazi suala hili muhimu la ulinzi wa raia na mali zao,” amesema Eshimuni.

Mwenyekiti wa Chama cha Wamachinga Mkoa wa Dar er Salaam, Namoto Yusuph amesema kuna maeneo ambayo wafanyabiashara hadi saa mbili  usiku kwa sasa ukiwamo Mtaa wa Congo.

Hata hivyo amesema ana imani jambo hilo watu wataenda wakibadilika taratibu kwa kuwa ni kitu ambacho hawakuwa wamekizoea.

“Nadhani ni mapema sana kusema hili la ufanyaji biashara saa 24 Kariakoo halijafanikiwa, tujipe muda kidogo, watu watabadilika taratibu,” amesema na kusisitiza kuwa ni muhimu kuwekwa taa maeneo hayo  kwani mbali ya usalama, pia itasaidia watu wasione tofauti ya mchana na usiku.

“Tunashukuru uzinduzi ulifanyika mkubwa sana katika kutekeleza jambo hili, lakini ieleweke uzinduzi  ni kitu kimoja na utekelezaji ni jambo jingine, nina imani mamlaka itazifanyia changamoto zilizopo kazi. Kwa kuwa usalama wa watu ndio kila kitu katika ufanyaji biashara,” amesema Namoto.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo, Severine Mushi  amekiri kwamba bado biashara katika eneo hilo haijachangamka kama watu walivyotarajia.

Mushi ambaye amesema yupo safarini, ameeleza atakaporejea atafanya ziara ya kujua changamoto zilizopo kwa wafanyabiashara tangu hilo la ufanyaji biashara saa 24 lianze na kuahidi kutoa tathiminii yao kwa umma.

Ukiacha wafanyabiashara, wateja usiku kufika maeneo hayo, kwa kuwa, hata hizo huduma za kutoa na kuweka pesa zinakuwa zimefungwa.

“Unaweza useme usibebe hela utaenda kutolea huko, lakini ukifika ndio hivyo, taasisi nyingi za kifedha muda huo zinakuwa zimefungwa, lakini pia mimi usalama wangu napokuwa Karikaoo, basi unajikuta tu unaogopa kwenda,” amesema Zulfa Kimath mkazi wa Kigamboni.

Gasper Hillary mkazi wa Mbezi, amesema maagizo ya maeneo mengine ya mkoa huo kufanya biashara saa 24 yaanze kutekelezwa, kwa kuwa sio kila mtu lazima afike Karikaoo kufanya ununuzi.

“Nilimsikia mkuu wa mkoa akiagiza wakurugenzi wa maeneo mengine nao waanzishe maeneo yao yatakayofanya kazi saa 24, nadhani waanze sasa na huenda wakawa hata mfano kama wakilisimamia hili vizuri kwa kuwa mwisho wa siku ni Dar kuongeza mapato yake,” amesema Hillary.

Sababu kuchelewa kufungwa taa, kamera

Wakati wafanyabiashara na wateja wakieleza changamoto hizo, Mhandisi wa Umeme  Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Juma Omar, amesema kuna sababu kadhaa zilizochelewesha kufungwa kwa taa na kamera.

Akieleza kwa undani, Omar amesema kampuni iliyoshinda zabuni ya kufunga taa hizo, mzigo wake ulichelewa kuwasili nchini baada ya meli waliyoitarajia kupata dharura.

“Hata hivyo, mpaka jana nilivyowasiliana nao, wamesema tayari mzigo umeshawasili na hadi kufika Jumatano watakuwa wameshautoa bandarini na taa hizo kuanza kufungwa,” amesema.

Pamoja na changamoto hiyo, Omar amesema bado wapo ndani ya muda wa mkataba na wao ambao ilipaswa hadi kuisha Machi mwaka huu wawe wamekamilisha shughuli hiyo tangu walivyotiliana saini Desemba  mwaka jana.

Katika kutekeleza hilo, Omar amesema kampuni hiyo katika awamu ya kwanza itafunga taa 213, zikihusisha barabara za  Mtaa wa Pemba, Tandamti, Mafia, Stesheni na Pugu Mnadani ambazo zote zimegharimu Sh800 milioni.

Amesema pia, taasisi nyingine zinasaidia katika hilo wakiwamo Wakala wa Barabara Vijijini na Mjini (Tarura), ambapo katika moja ya masharti kila wanapojenga barabara zao lazima wafunge na taa.

“Sisi mitaa ambayo tunaweka taa hizo ni ile ambayo barabara zilikuwepo tangu zamani kabla ya kuanzishwa kwa Tarura, tunatumia vyanzo vya mapato  ya ndani kuzinunua,” amesema.

Kwa tathmini waliyoifanya mwaka 2022 kwa kushirikiana na Wakala wa Ufundi na Umeme (Tamesa),   amesema mpaka sasa taa zinazohitajika Wilaya ya Ilala ni 38,000 lakini zipo taa 4,000 na gharama ya taa moja ni kuanzia Sh3 milioni hadi 10 milioni.

Wakati kuhusu kamera, amesema zenyewe zilikuwa zikisubiri kukamilika kwa ufungwaji wa taa, kwa kuwa nguzo za taa ndizo zitakazotumika kufungia kamera hizo.

Related Posts