Dar es Salaam. Familia ya mwanamke aliyeuawa na mumewe na kisha mwili wake kuteketezwa kwa moto Kigamboni jijini Dar es Salaam, Naomi Orest Marijani, imetoa ratiba ya mazishi ya mpendwa wao.
Familia hiyo ya marehemu Naomi imefikia hatua hiyo baada ya kumalizika kwa kesi ya mauaji ya mwanafamilia huyo na Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam kutoa amri familia kukabidhiwa masalia hayo, pamoja na kukamilisha taratibu nyingine.
Kaka wa marehemu, Ismail Marijani amelieleza Mwananchi leo Jumatano, Machi 12, 2025 kuwa ratiba ya mazishi ya masalia hayo yatafanyika Jumamosi Machi 15, 2025, katika makaburi ya ukoo, jijini kwao Mbambua, wilayani Mwanga, mkoani Kilimanjaro.
Ismail amelieleza Mwananchi taratibu zote za maandalizi ya masalia hayo ya mwili wa marehemu Naomi zimeshakamilika ikiwemo upatikaji wa cheti cha kifo alichokipata jana Jumanne, kutoka Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita).
Amesema ratiba hiyo itaanza rasmi kwa ibada na kutoa heshima za mwisho, itakayofanyika Ijumaa Machi 14, 2025, nyumbani kwa baba yao mdogo, Beda Mchome, Kijichi, Mtaa wa Greenview/Manyara, kabla ya kuanza safari kuelekea kijijini.
“Tutakwenda kuchukua masalia kwa ZCO (Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu Dar es Salaam), Alhamisi (Machi 13), tutalala nayo nyumbani,” amesema Ismail.
“Asubuhi Ijumaa tutafanya ibada kisha litafuata shughuli ya kuaga na baadaye jioni tutaanza safari kupeleka kijijini Mbambua kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika Jumamosi (Machi 15) katika makaburi ya ukoo.”
Kwa mujibu wa kumbukumbu za kesi hiyo ya jinai, Naomi aliuawa na mumewe, Hamis Said Luwongo, Mei 15, 2019 nyumbani kwao, Gezaulole, Wilaya ya Kigamboni, jijini Dar esa Salaam.
Baada ya mauaji hayo, Hamis aliuchoma moto mwili wake kwa kutumia mkaa magunia mawili ndani ya banda la kuku kisha masalia na majivu ya mwili huo akayazika shambani, katika shamba lake lililoko katika Kijiji cha Malogoro, wilayani Mkuranga mkoani Pwani na kupanda migomba juu yake.
Masalia hayo yanayotarajiwa kufanyiwa utatibu huo wa kuyahifadhi kuashiria mazishi ya mwili wa marehemu Naomi ni udongo wenye mchanganyiko wa mafuta yaliyodhaniwa kuwa ya mwilini mwa binadamu.
Udongo huo ulichukuliwa na askari Polisi wa kitengo cha uchunguzi wa sayansi jinai kutoka katika shimo alimofukiwa majivu ya masalia ya mwili wa marehemu, shambani.
Ulipelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali pamoja na mifupa na meno ambayo pia ilikuwa ndani ya shimo hilo, na sampuli nyingine kwa ajili ya uchunguzi wa vinasaba.
Wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, udongo huo uliwasilishwa mahakamani hapo na shahidi wa 12 wa upande wa mashitaka, Meneja wa Kanda ya Kusini ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Hadija Saidi aliyeufanyia uchunguzi pamoja na mifupa.
Shahidi huyo akiongozwa na mwendesha mashtaka aliiomba Mahakama ikaupokea kuwa kielelezo cha 8 cha upande wa mashitaka katika kesi hiyo.
Kuhusu mifupa na meno shahidi huyo aliieleza Mahakama ilitumika na kuisha yote katika mchakato wa uchunguzi wa vinasaba.
Mahakama baada ya kupokea udongo huo wenye mchanganyiko na mafuta, ulikabidhiwa kwa Ofisi ya ZCO, kwa ajili ya kuhifadhiwa, wakati kesi hiyo inaendelea.
Kesi hiyo ilifikia mwisho Februari 26, 2025, Mahakama ilipotoa hukumu ya kesi hiyo, ambapo ilimtia hatiani kwa kosa hilo la kumuua mkewe huyo Naomi, kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, kama ilivyorejewa mwaka 2019.
Hukumu hiyo ilitolewa na Jaji Hamidu Mwanga, aliyesikiliza kesi hiyo, ambapo alimtia hatiani mshtakiwa Hamis na kumuhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa baada ya kuridhika na ushahidi kuwa Naomi alifariki na mshtakiwa ambaye alikuwa mumewe ndiye aliyemuua.
Siku hiyo baada ya kusomwa hukumu mwendesha mashitaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Yasinta Peter aliyeongoza jopo la mawakili wa Serikali walioendesha kesi hiyo, aliiomba Mahakama itoe amri familia ikabidhiwe masalia hayo kwa ajili ya taratibu za kuyasitiri.
Mahakama ilikubaliana na ombi hilo, hiyo ikatoa amri ikiielekeza kwa ZCO.