Dar es Salaam. Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo, Othman Masoud amesema mwekeleo wa sasa wa chama hicho, ni kufanya siasa za mapambano na si laini na nyepesi zisizotoa dira ya demokrasia ya kweli.
Othman ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, amesema mapambano hayo, siyo ya kupigana bali kutafuta mageuzi katika mfumo wa siasa ili kupata demokrasia ya kweli.
Mwenyekiti huyo ameeleza hayo, leo Jumatano Machi 12, 2025 wakati akifungua kongamano la viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam, lililofanyika makao ya ACT- Wazalendo, Magomeni, ikiwa ni hatua za awali za uzinduzi wa operesheni kubwa ya chama kupigania na kulinda demokrasia.
Othman aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, amesema uamuzi huo umefikiwa katika kikao cha halmashauri kuu ya ACT-Wazalendo kilichoketi Februari 23, 2025 kuazimia chama hicho, kibadili uelekeo wa siasa zake nchini.
“Sasa ni wakati wa kwenda na hali ya bahari ilivyo, kama ipo vibaya hatukuitaka bali tuliipambania kwenda katika maridhiano.Tunatoka kwenye siasa za maridhiano, tunakwenda siasa zinazohitajika wakati huu za mapambano,” amesema.
“Tunaposema siasa za mapambano hatupigani na mtu, bali tunapigani jambo tunaloliamini. La kwanza ni kupigania demokrasia katika nchi yetu,” amesema Othman.
Sababu za kubadili uelekeo, Othman amesema ni kutokana na awali ACT- Wazalendo ilimua kufanya siasa nyepesi kwa sababu ya mazingira yaliyokuwa, akitolea mfano mwaka 2015/20 hakukuwa na mazingira rafiki kwa upinzani.
Hata hivyo, Othman amesema lakini mwaka 2021 Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ilipoingia na kauli ya kuliponya Taifa, chama hicho kiliamini kila kitu kitakuwa sawa.
Othman alikumbushia namna ya aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Abdulrahman Kinana alivyoeleza dhamira ya Serikali ya kuhakikisha chaguzi za Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu zitakuwa huru na haki.
Kinana alieleza hayo Machi 5, 2024 alipomwalikisha Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan katika Mkutano Mkuu wa ACT- Wazalendo uliofanyika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
“Lazima tuseme ukweli, hofu ya viongozi wenzangu wa vyama vya siasa na asasi za kiraia na viongozi wa dini msingi wa hofu yao ni yale yaliyotokea 2019/20, naomba nikiri Rais Samia ameamua uchaguzi wa mwaka 2024 na 2025 utaachwa ili wapigakura wafanye uamuzi,” amesema Kinana.
Katika maelezo yake Othman, amewaambia viongozi wa ACT- Wazalendo Mkoa wa Dar es Salaam, kuwa maelezo ya Kinana ndiyo ilikuwa kauli ya Rais Samia aliyeahidi uchaguzi utakuwa huru na haki.
“Kama hukuwasikiliza, wala hukuwaamini watu hawa, utakwenda kumwamini nani? Tukumbuke kwamba tulipewa ahadi na matumaini. Ukitoka kwenye shida mtu akikupa matumaini hasa mama utaamini au huamini? Akijibiwa na viongozi utaamini.
“Kikaja kikosi kazi, ACT tukashiriki kwa namna ya kipekee, tukatoa mawazo kuliko chama kingine tena kwa maandishi kuhusu reforms za uchaguzi. Pia, ACT tulisimamia kwa kiwango kikubwa kutafsiri 4R (ustahimilivu, kujenga upya, mageuzi na maridhiano,” amesema Othman.
Mbali na hilo, Othman amesema ACT- Wazalendo, ilifanya siasa kwa mujibu wa hali ilivyokuwa, huku akinogesha kwa msemo kwamba katika vita haipaswi kutumia nguvu kama mahali hapaitaji nguvu.
“Siasa tulizotoka ni za kuaminishwa kwamba tunakwenda kwenye siasa za maridhiano. Tulifanya kila liwezekanalo katika ngazi zote ndani na nje, hakuna kiongozi wa CCM ambaye hakufikiwa kumweleza maridhiano, tuliamini katika maridhiano na siasa na kistaharabu,” amesema Othman.
Othman amesema licha ya jitihada za ACT-Wazalendo kuwa mstari wa mbele kufanikisha maridhiano, lakini chama hicho kiliambulia viongozi wake kukamatwa, kuwekwa ndani na kufunguliwa mashtaka ya uongo katika mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba 27, 2024.
Othman amesema baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji, ulioshuhudiwa CCM ukinyakuwa viti vingi, wapo ndani ya chama hicho waliodhani taasisi hiyo haikufanya siasa za mapambano.
“Wengi badala ya kutazama tatizo liko wapi, hata baadhi ya viongozi wetu walianza mchezo wa kulaumiana,”amesema Othman.
“Ndugu zangu mnaona hata kwenye makundi ya mitandao ya kijamii badala ya kutafuta adui yupo wapi au tatizo liko, badala yake tunatafutana uchawi ndani yetu wenyewe, tunapotea…Tutazame tatizo liko wapi,” amesema Othaman.
Makamu huyo, amesema katika mapambano hayo watashirikiana na vyama vya upinzani makini na wameshaanza mazungumzo ya awali ya kufanikisha lengo hilo.
Awali, Makamu mwenyekiti wa ACT Wazalendo (Bara), Isihaka Mchinjita amesema kwa hatua za awali chama hicho, kimesusia ushiriki wa kikao cha siku cha Baraza la Vyama vya Siasa, kinachofanyika mkoani Morogoro.