Dar es Salaam. Utafiti wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari (SJMC), umebaini katika uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka 2024, wagombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM), ndiyo walioongoza kutajwa katika habari za redio zilizoripotiwa ukilinganisha na wale wa vyama vingine.
Kwa mujibu wa utafiti huo wenye jina la uripoti wa vituo vya redio kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2024, wagombea wa CCM wametajwa mara 55, huku wa Chama cha ACT-Wazalendo wakitajwa mara 13.
Utafiti huo ni wa sita kati ya mfululizo wa tafiti za SJMC kuhusu utendaji wa vyombo vya habari nchini na umehusisha redio 35 katika kanda tano za Tanzania bara.
Akiwasilisha utafiti huo leo Jumatato Machi 12, 2025 , Mtafiti Mkuu kutoka SJMC, Dk Malima Zacharia amesema wagombea wa CCM wametajwa mara 55.
Amesema wagombea wa chama hicho wanafuatiwa na wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) waliotajwa mara 53, huku wa Chama cha Wananchi (CUF) wakitajwa mara 14 na ACT-Wazalendo mara 13.
Sambamba na hayo, ripoti hiyo pia imeonesha katika uchaguzi huo, asilimia 70.2 ya vyombo vya habari (redio) havikurejea ilani ya vyama vya siasa wakati zikiripoti habari za vyama husika.
Kupitia utafiti huo uliohusisha vituo vya redio 35 vilivyopo maeneo mbalimbali nchini, ni asilimia 30 pekee ndivyo vilirejea ilani ya vyama katika ripoti zake.
Dk Zacharia amesema katika habari 248 walizopitia, asilimia 15.3 ziliripotiwa kwa kurejea ilani kwa kiasi kidogo, huku asilimia 4.0 zikirejea kwa kiasi kikubwa.
“Vyombo vya habari kuripoti kuhusu wagombea na kurejea ilani za uchaguzi za vyama vyao ni jambo muhimu kwa sababu huwaelimisha wananchi,” amesema.
Pia, amesema utafiti huo umebaini vituo vya redio viliripoti zaidi matukio ya kuitwa na taasisi mbalimbali, kuliko habari za kutumia jitihada binafsi kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024.
Kwa mujibu wa utafiti huo, kati ya habari 628 asilimia 63 zilikuwa za matukio, huku za kutafuta kwa juhudi binafsi zikiwa ni asilimia 37.
Dk Zacharia amesema ingawa matukio ni muhimu, vyombo vya habari vinapaswa kutafuta habari zake.
“Hii itasaidia kutengeneza ajenda ili kuhimili ushindani na kuwa mbele ya vyombo vingine vya habari,” amesema Dk Zacharia.
Kwa upande wa ushiriki wa wanawake kama vyanzo vya habari,utafiti huo umebaini zaidi ya nusu ya habari 990 zilizoripotiwa na redio 35 nchini katika kipindi cha uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka 2024, hazikuwahusisha wanawake kama vyanzo vya habari.
Ripoti hiyo imeweka wazi kuwa, asilimia 62 ya habari zilizorushwa katika vyombo hivyo vya habari, zilihusisha wanaume na vyanzo vingine, lakini si wanawake.
Hiyo ni sawa na kusema zaidi ya vyombo sita kati ya 10 vya habari havikuhusisha hata mwanamke mmoja kama chanzo cha habari.
Dk Zacharia amesema ni asilimia 22.8 pekee ya habari zilizoripotiwa katika vyombo hivyo, zilihusisha mwanamke mmoja kama chanzo cha habari.
“Ukilinganisha na tafiti zilizotangulia, kipengele cha kujumuisha wanawake kama vyanzo vya habari hakijaimarika,” amesema Dk Zacharia.
Hata hivyo, akitoa tafakuri baada ya kuwasilishwa ripoti ya utafiti huo, mwanazuoni maarufu Profesa Issa Shivji amesema mchakato wa uchaguzi unahusisha uandikishaji, utangazaji wapigakura, kampeni, kupiga kura kuhesabiwa na kutangazwa washindi.
Amesema taarifa ya utafiti haikuangalia mchakato wa uchaguzi bali imepita kwenye eneo dogo la kampeni pekee.
“Ukijikita kwenye kampeni pekee unakosa mambo mengi hasa kwenye uchaguzi wa mwaka 2024 unajikuta umekosa mambo mengi tu,”amesema.
Profesa Shivji amerejea kauli ya Waziri Mkuu mstaafu Jaji Joseph Warioba aliyesema uchaguzi wa 2024 haukuwa tofauti na 2019 na kwamba, hali hiyo ikiendelea itahatarisha amani ya nchi.
Pia, amerejea malalamiko ya vyama vya upinzani vilivyodai uchaguzi wa Serikali za mitaa wapo wanafunzi wa shule ambao hawakufikia umri wa kupiga kura waliandikishwa na video zilisambazwa mitandaoni.
Mwanazuoni huyo amesema utafiti huo haukuhusisha mambo kama hayo iwapo yameripotiwa kwenye vyombo vya habari.
Amesema watafiti walipaswa kuonyesha iwapo vyombo vya habari viliandaa kuhusu mambo hayo yaliyolalamikiwa.
“Kigezo kimoja cha uchaguzi huru ni kuwepo kwa mjadala wakati wote ambako uchaguzi unaendelea. Uchaguzi haupaswi kuwa na siri,” amesema.
Mtazamo wa Profesa Shivji, ni kwamba kutoangalia mchakato wote wa uchaguzi huo, kunaondoa maana nzima ya uchaguzi wote.
Mhariri Mkuu wa Clouds Media Group, Joyce Shebe amesema kupitia utafiti huo imeonekana dhahiri bado vyombo vya habari havijavaa viatu vyake sawasawa wakati vyombo vya habari vina umuhimu mkubwa.
“Habari za uchunguzi zimeshuka kwa kiwango kikubwa, zamani kwenye vyombo vya habari unakuta dawati la uchunguzi na watu wanarithishana ujuzi akiondoka mtu anabaki mwingine, sasa vinapata ugumu kutokana na bajeti ndogo na kukosa ujuzi wa kufanya habari za uchunguzi,” amesema.
Mkufunzi wa Chuo cha SJMC, Dk Elisha Magolanga amesema changamoto inayoonekana kwenye fani ya habari imechangiwa na mifumo ya elimu kuanzia chini kwa kuwa, wanafunzi sasa wanasoma kujibu mitihani na sio kutatua changamoto zinazowahusu.
Changamoto nyingine aliyoitaja amesema, “baadhi ya vyombo vya habari wanalipisha hadi Sh 100,000 kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo hii sio sawa inasababisha tusiwe na waandishi bora kama tulivyotamani.”
Mwanafunzi wa SJMC, Caroline Malewo kwenye mjadala huo amesema namna ambavyo habari zinaandaliwa hususani za siasa haziwavutii vijana, hivyo ni muhimu kuchangamanisha na habari hizo na burudani.