LIGI Kuu Bara inatarajiwa kuendelea tena kesho kwa mchezo wa kiporo baina ya Simba dhidi ya Dodoma Jiji ikiwa ni funga hesabu kwa mechi za raundi ya 23 kabla ya ligi hiyo kusimama hadi Aprili Mosi kupisha kalenda ya mechi za kimataifa kwa timu za taifa na michuano ya Kombe la Shirikisho.
Hata hivyo, wakati ligi ikienda mapumziko kupisha kalenda ya Fifa kwa mechi za kimataifa, katika mechi 180 zilizopigwa hadi sasa kuna baadhi ya timu yaani ukilenga langoni tu, watu wanahesabu bao kutokana na kuruhusu mabao mengi.
Rekodi zinaonyesha kuwa katika mechi 180, yamefungwa mabao 400, huku Fountain Gate na KenGold zikiongoza kwa kuruhusu mabao mengi zaidi zikifungwa 40 kila moja katika mechi 23 zilizocheza kila moja, ilhali Simba ikiwa ndio timu iliyoruhusu mabao machache (8).
Timu hizo zimekuwa na wastani wa kuruhusu bao 1.73 kila moja kwa kila mchezo hadi sasa katika Ligi Kuu zikiwa ndizo zenye ukuta mbovu kuliko zote, huku Fountain yenyewe ikifunga 28 ikiwa nafasi ya saba katika msimamo kwa pointi 28, wakati KenGold ikifunga 20 ikiburuza mkia na pointi 16.
Yanga inayoongoza msimamo ndio kinara wa kufunga mabao kwa sasa ikiwa nayo 58 sawa na pointi ilizonazo na yenyewe ikishika nafasi ya pili kwa kuruhusu idadi ya mabao machache (9) nyuma ya Simba, huku Azam FC iliyopo nafasi ya tatu ikiwa ni ya tatu kwa kufungwa mabao 12 na kufunga 36.
Yanga na Simba zina kiporo kimoja cha mechi ili kukamilisha 23 kutokana na pambano la Dabi ya Kariakoo kushindwa kupigwa wikiendi iliyopita kwa kuahirishwa na Bodi ya Ligi baada ya Simba kutishia kugomea kwa ilichodai ni kuzuiwa na makomandoo wa Yanga kufanya mazoezi siku moja kabla ya mchezo.
Timu hizo pekee zinazochuana kileleni ndizo zilizofungwa idadi ya mabao chini ya 10, lakini zilizosalia 14 zimevuka idadi hiyo na kutofautiana, huku Fountain na KenGold zikiongoza orodha ya kuruhusu mabao mengi zaidi.
Ukiondoa Fountain na KenGold, timu zinazofuata kwa kufungwa idadi kubwa ya mabao katika ligi hiyo ni KMC iliyopo nafasi ya 11 katika msimamo ikiwa imefungwa 34, huku yenyewe ikifunga 16 katika mechi 23.
KMC msimu huu imewatumia makipa watatu tofauti akiwamo Fabien Mutombola, Wilbol Maseke, Ali Ahamada na Ismail Mpanki, lakini mambo bado yamegonga mwamba na wapinzani kufunga mara kwa mara.
Vipigo vikubwa alivyokutana navyo Mpanki hadi sasa ni dhidi ya Yanga 5-0 na Azam FC 5-0, hivyo amefungwa mabao 10 kwenye mechi mbili, huku mengine tisa katika mechi nyingine 10 kitu kinachoiweka katika presha kubwa timu hiyo katika mechi saba zilizosalia ili kufunga msimu huu.
Wazoefu wa ligi na zilizo katika janga la kushuka daraja yaani Kagera Sugar na Tanzania Prisons ndizo zinafuata kuwa na uchochoro ukutani baada ya KMC, zenyewe zikiwa zimefungwa mabao 31 kila moja, huku zikifuata katika msimamo juu ya KenGold, Prisons ikiwa ya 15 na Kagera ikishika nafasi ya 14.
Timu hizo miongoni mwa zilizofanya mabadiliko ya mabenchi ya ufundi, zimetofautiana pointi moja tu katika msimamo Kagera ikiwa na 19 na Prisons 18, huku Kagera inayofundishwa na Juma Kaseja ikiwa na mabao 18, sita zaidi na waliyo nayo maafande wa Prisons chini ya Josiah Amani.
Timu tatu za Tabora United, Namungo na Mashujaa zinafuata katika orodha hiyo ya zilizoruhusu mabao mengi zikiwa zimefungwa 28 kila moja, japo zinatofautiana katika msimamo wa ligi hiyo – Tabora United ikiwa nafasi ya tano wakati Mashujaa ni ya 10 ilhali Namungo ipo nafasi ya 12 kutokana na tofauti za pointi na uwiano wa mabao ya kufunga.
Tabora United imefunga mabao 27, ikiwa ni tofauti na bao moja na yale iliyofungwa ikiwa imekusanya pointi 27, wakati Mashujaa imefunga 19 ikiwa imevuna pointi 24 kupitia mechi 23, huku Namungo imefunga mabao 16 ikikusanya pointi 22 ikishuka pia uwanjani mara 23.
Timu ya tisa kwa kufungwa mabao mengi ni Dodoma Jiji iliyopo nafasi ya nane ikiwa imekusanya pointi 26 kupitia mechi 22 na ikiwa na kiporo dhidi ya Simba kitakachopigwa kesho Ijumaa, kwani timu hiyo imefungwa mabao 27 na kufunga 22, huku Pamba Jiji ikifunga hesabu ya timu 10 zilizo na beki mbovu.
Pamba iliyorejea Ligi Kuu Bara baada ya msoto wa miaka 23 tangu iliposhuka daraja mwaka 2001, imefungwa mabao 25, huku ikifunga 14 katika mechi 23 na kushika nafasi ya 13 baada ya kukusanya pointi 22, ikiwa ni kati ya timu zilizopo katika presha ya kushuka daraja msimu huu.
Kwa timu zenye ukuta mgumu ukiondoa Simba (8), Yanga (9) na Azam (12), nyingine zinazokamilisha idadi ya timu 16 msimu huu na mabao yao kwenye mabao ni JKT Tanzania (17), Singida Black Stars (19) na Coastal Union iliyofungwa 23 kupitia mechi 23 ikiwa na wastani wa kuruhusu bao moja kwa kila mchezo.
Mapema kocha wa Namungo, Juma Mgunda, Fred Felix ‘Minziro’ wa Pamba Jiji na Mecky Maxime wa Dodoma Jiji walikaririwa kwa vipindi tofauti wakieleza namna wanavyopambana kurekebisha tatizo la mabeki wa timu hizo kuruhusu mabao kirahisi, kwani yanawakwamisha kupata ushindi.