Dodoma. Siku moja baada ya Serikali kuwasilisha Mapendekezo ya bajeti ya Sh57.04 Trilioni, wachumi na wananchi wameonyesha hofu ya kuhitaji mikopo zaidi.
Hofu hiyo inatokana na mahitaji makubwa ya fedha kwa ajili ya uchaguzi, ulipaji madeni na kuandaa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) ambayo yametajwa kuwa yatatafuna fedha nyingi na hivyo kushindwa kuendelea na miradi.
Hata hivyo, Serikali katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha 2025/2026 imetangaza kutokuanzisha miradi mipya badala yake wataendelea kukamilisha iliyoanzishwa.

Jana Waziri wa Fedha Dk Mwigulu Nchemba aliwasilisha bajeti hiyo huku akitaka vipaumbele sita ambavyo ni kulipa deni la Serikali, mishahara, uchaguzi mkuu, maandalizi ya AFCON, uimarishaji wa Demokrasia, amani na utulivu.
Dk Mwigulu anasema katika bajeti ijayo, Sh40.09 Trilioni ambayo ni asilimia 69.7 ni fedha za ndani wakati Sh16.7 trilioni ni fedha za nje zinazobeba asilimia 30.3.
Mchumi na mtaalamu wa masuala ya biashara kutoka Mwanza Zacharia Jackson anasema bajeti haina ubaya isipokuwa ipo hatari Serikali kuingia kwenye mikopo zaidi.
Zacharia anasema vipaumbele vilivyowekwa ni muhimu na vyote vinahitaji fedha nyingi hivyo kuna uwezekano mkubwa Taifa likaingia kwenye madeni tena.
“Mfano AFCON ni muhimu sababu inaotangaza nchi yetu, lakini suala la uchaguzi nalo ni muhimu zaidi, hivyo kama hawakuwa makini tujue fedha zote zitaelekezwa huko na hakuna cha maana kitafanyika,’ amesema.
Anasema katika kipindi cha miaka mitano kumekuwa na ongezeko la bajeti kila mwaka ambalo huelezwa zinakwenda kuchochea Maendeleo ya uchumi na baadhi ya maeneo kumeshuhudiwa hayo.
Hata hivyo anaeleza ili kuepuka hayo ni muhimu kila kilichopangwa kisimamiwe na kupelekwa kwa malengo yaliyokusudiwa.
Mchumi na mtaalam wa masuala ya fedha Sablina Kaijage anataja eneo litakalotumia fedha nyingi ni kwenye uchaguzi akieleza kusimama kwa miradi hata inayoendelea kwa sasa.
Sablina anasema huwa ni ngumu kutenga fedha toshelevu kwa ajili ya uchaguzi kwani mara nyingi kuna mambo hujitokeza katikati na kujikuta serikali inatumia kiasi kikubwa nje ya bajeti.

Hata hivyo anashauri mawazo ya watu yaelekeze Sh40.09 ambazo ni fedha za ndani kuliko kuwazia kiasi kinachotegemewa kutoka nje.
“Tunapaswa kubajetia fedha za ndani, hapa tukumbuke nyakati za uchaguzi watu wengi huwa hawatoi misaada kama inavyotakiwa, kwa kuwa uchaguzi ni muhimu na AFCON naona fedha zitakwenda huko na kiasi kinachobaki zitakuwa mishahara,” anasema Sablina.
Mfanyabiashara wa mitumba soko la saba saba Aidan Chedego anasema kwake yeye muhimu Watumishi wakipata mishahara ili waendelee kuingia sokoni.
Chedego anabainisha kuwa maeneo mengine kwao ni kama hayana faida licha ya kukiri kuhusu uwepo wa amani na mambo lakini boashara ni muhimu.