Dar es Salaam. Matumizi ya viti mwendo visivyo sahihi yanatajwa kusababisha matatizo makubwa ya kiafya kwa watu wenye changamoto za ulemavu wa miguu, wataalamu wameonya.
Vitimwendo vinachukuliwa kuwa msaada muhimu kwa watu wenye changamoto za ulemavu wa miguu. Hata hivyo, iwapo havitachaguliwa ipasavyo, vinaweza kusababisha matatizo makubwa ya kiafya badala ya kusaidia hali ya mtumiaji.
Akizungumza katika mkutano wa wadau kuhusu matumizi sahihi ya vitimwendo hivi karibuni, Mratibu wa Vitimwendo na Tiba Mazoezi kutoka Hospitali ya CCBRT, Neophita Lukiringi, amesema matumizi ya vitimwendo yasivyo sahihi yanaweza kusababisha matatizo ya kiafya ya muda mrefu.
“Unapompatia mlemavu kitimwendo ambacho si sahihi, unamsababishia magonjwa, ikiwemo vidonda mgandamizo katika uti wake wa mgongo na ufupisho wa misuli, hasa kwa wale ambao kiti mwendo ni kirefu kuliko kimo chake,” Lukiringi ameeleza.
Ameongeza kuwa hali hiyo inaweza kusababisha kupungua kwa uwezo wa kujitegemea na kujiamini, hali inayoweza kumtenga zaidi mtumiaji na jamii.
Ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya mwaka 2023 kuhusu matumizi sahihi ya viti hivyo inaeleza kuwa vidonda kwenye uti wa mgongo na mikazo ya misuli ni miongoni mwa hali zinazosababisha maumivu makali na madhara makubwa kwa watu wanaotumia vitimwendo visivyo sahihi.
Lukiringi amewasihi wadau wanaoshughulika na ugawaji wa viti mwendo kufanya utafiti wa kina ili kuhakikisha kuwa vifaa hivyo vinafaa kwa watumiaji. Hii itahakikisha kuwa watumiaji wanapewa viti vinavyowasaidia kweli katika kutembea kwao, kuboresha maisha yao na kuimarisha ujumuishaji wao katika jamii.
Kwa upande mwingine, mtaalamu wa tiba mazoezi maarufu ‘fiziotherapia,’ Seleman Martine, ameonya kuwa matumizi mabaya ya viti mwendo yanaweza pia kusababisha changamoto za kiafya za kimwili na kiakili.
“Matumizi yasiyo sahihi ya vifaa vya kusaidia kutembea yanaweza kusababisha utegemezi, jambo linaloweza kuathiri afya ya akili kutokana na matatizo ya kimwili yanayotokana na matumizi hayo,” amesema Martine.
Ameeleza zaidi kuwa vitimwendo visivyofaa vinaweza kusababisha vidonda kwenye makalio, nyonga au mgongo, maumivu kwenye mabega na mikono, uharibifu wa mishipa ya fahamu, au hata mikwaruzo kwenye mifupa.
Pia ametaja hatari ya ajali na maumivu ya mgongo kutokana na matumizi mabaya ya viti hivyo.
Ili kupunguza hatari hizo, amehimiza mafunzo sahihi kwa watumiaji, matengenezo ya mara kwa mara na ufuatiliaji wa afya yao.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Kyaro Assistive Tech, kampuni inayoongoza katika utengenezaji wa vitimwendo, Colman Ndetembea, ni muhimu kuzingatia afya ya mtumiaji wakati wa kutengeneza vifaa hivyo.
“Wadau wamekuwa wakitoa viti mwendo, lakini wanapaswa kutilia mkazo afya ya mtumiaji badala ya urahisi wa kusafiri tu,” amesema.
Ametoa wito kwa watengenezaji wa viti hivyo kukusanya taarifa muhimu za watumiaji ili kuhakikisha kuwa viti wanavyotengeneza vinakidhi mahitaji maalumu ya kila mtu badala ya kuongeza matatizo ya kiafya.
“Ni muhimu kuzingatia umri wa mtumiaji, aina ya ulemavu na mazingira anayoishi wakati wa kuchagua kiti sahihi cha magurudumu. Hii itahakikisha kuwa kinamtosheleza kwa ufanisi na kinapatikana kwa gharama nafuu,” ameeleza Ndetembea.