Dar es Salaam. Mkazi wa Bagamoyo, Fred Chaula (56) na wenzake wawili wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashtaka ya kumuua ndugu yao, Regina Chaula (62).
Mbali na Fredy, washtakiwa wengine ni Bashir Chaula (49), dereva bodaboda na mkazi wa Tegeta pamoja na Denis Mhwaga, mkazi wa Iringa.
Washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo leo, Jumatano, Machi 12, 2025 na kusomewa mashtaka mauaji na wakili wa Serikali, Tumaini Mafuru.
Hata hivyo, kabla ya kusomewa shtaka hilo, Hakimu Mkazi Mkuu, Rahim Mushi aliwaeleza washtakiwa hao kuwa hawatakiwi kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi za mauaji.
Pia, alisema shtaka la mauaji linalowakabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria.
Baada ya kueleza hayo, Wakili Mafuru aliwasomewa mashtaka yao kuwa wanadaiwa kutenda kosa hilo, Januari 18, 2025 eneo la Bahari Beach, Wilaya ya Kinondoni.

Inadaiwa siku hiyo ya tukio, washtakiwa kwa pamoja walimuua Regina Chaula, ambaye ni mwanafamilia mwenzao, na mwili wake kuutupa kwenye shimo la maji machafu, lililopo katika nyumba ya marehemu, wakati wakijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Baada ya kusomewa shtaka hilo, upande wa mashtaka ulidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu Mushi aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 27, 2025 kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande.