TFF sasa hivi imekuwa haina masihara na viwanja ambavyo vinashindwa kutimiza vigezo vya kutumika kwa ligi ambapo inavitembezea hasa rungu pasipo kutanguliza mambo ya busara.
Na hiki ndicho ambacho sisi hapa kijiweni tulikuwa tunatamani kitokee kwamba kama viwanja havifanyiwi ukarabati basi timu zinazovitumia zionje shubiri ya kucheza mechi zao za nyumbani kwingineko.
Visipokuwa vinapewa adhabu timu zinajisahau kuwakumbusha wamiliki jukumu lao la kurekebisha upungufu ambao vinakuwa nao na matokeo yake ndio vinafanya mechi zichezwe katika eneo lisiloridhisha la kuchezea na kusababisha bolu lisitembee.
Hivi karibuni viwanja vinne vimepigwa rungu ambavyo ni Ali Hassan Mwinyi uliopo Tabora, CCM Kirumba wa Mwanza, Liti wa Singida na Jamhuri ulio katika makao makuu ya nchi kule Dodoma.
Viwanja hivyo karibia vyote vimefungiwa kwa sababu inayofanana ambayo ni kutokuwa na eneo bora la kuchezea kwa maana ya nyasi ambazo kuna viwanja zimechakaa na vingine hazipo kabisa kwa baadhi ya maeneo.
Wakati viwanja hivyo vikifungiwa kuna uwanja mmoja unatamba hivi sasa na unasifika kwa kuwa na eneo bora la kuchezea ambao ni wa Meja Jenerali Isamuhyo unaotumiwa na timu ya JKT Tanzania kwa mechi zake za nyumbani za mashindano tofauti.
Eneo la kuchezea limesawazishwa vizuri, nyasi imeenea na imefyekwa vyema na ina kijani kilichokolea kudhihirisha kwamba unatunzwa na kuhudumiwa vizuri kama ambavyo inahitajika ili kulinda eneo lake la kuchezea.
Kwa vile upo chini ya umiliki wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), labda unaweza kutumika kama ushawishi kwa wamiliki wa viwanja korofi waingie nalo mkataba wa matunzo ili wawasaidie kuvisimamia na kisha wagawane sehemu ya mapato yanayopatikana kupitia viwanja hivyo.
Jeshi haliwezi kutuangusha tunajua na tuna imani kubwa litatusaidia kuvifanya viwanja hivyo kuwa kama ulivyo uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo.