MSIMU huu umekuwa na upepo ambao sio mzuri kwa makocha na hadi hapa akili za kijiweni zinapochakata kuna makocha kama 14 hivi wameondoka kwenye timu zao kwa kufungishwa virago.
Ni makocha wawili tu ambao wameondoka kwa uamuzi wao binafsi na sio kwa sababu ya matokeo yasiyoridhisha ambao ni Abdi Moalin na Sead Ramovic walioziacha timu zao zikiwa haziko vibaya katika ligi.
Abdihalim Moallin aliamua kuiacha KMC baada ya kupata ofa nono ya kujiunga na Yanga ambayo baadaye ikaondokewa na kocha wale mkuu Ramovic aliyepata dili tamu kule Algeria katika timu ya CR Belouizdad.
Presha ya kuhitaji matokeo mazuri hivi sasa inaonekana imetawala kwa timu zote zinazoshiriki Ligi Kuu hivyo viongozi wao wanaonekana wako tayari kuchukua uamuzi mgumu muda wowote wanapoona mambo sio mazuri ili timu iwe na mwenendo mzuri.
Tumeshuhudia makocha ambao walitimuliwa huku timu zao zikiwa hazipo kwenye nafasi mbaya katika msimamo wa ligi lakini kitendo cha kuangusha pointi katika mechi chache tu kikawaponza.
Na hilo ndilo limenifanya niwakumbuke wazawa wenzetu ambao timu zao hivi sasa zinaonekana kuwa katika mazingira salama ambao ni kocha wa Pamba Jiji, Felix Minziro na kocha wa JKT Tanzania, Ahmad Ally.
JKT Tanzania kwa sasa ipo nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi ikiwa imekusanya pointi 30 na Pamba Jiji inashika nafasi ya 13 ambapo imekusanya idadi ya pointi 22 katika mechi 23.
Ukilinganisha na ilivyokuwa katika mzunguko wa kwanza, unaona kabisa Pamba imepiga hatua kubwa na angalau sasa hivi imekuwa ikivuna pointi jambo ambalo linatoa matumaini kwa mashabiki wake kuwa inaweza kubaki.
Hata hivyo, Ahmad Ally na Minziro wanapaswa kuangalia kilichotokea kwa wenzao ambao ajira zao zimesitishwa na kuandaa mpango bora mkakati wa kuhakikisha wanamaliza vyema mechi zao walizobakiza kwenye ligi.
Kwa ambacho kimetokea msimu huu upepo unaweza kubadilika ghafla na wakajikuta wanaingia katika mkumbo wa wenzao.