Dar es Salaam. Mahakama ya mwanzo Kariakoo, imemuhukumu John Batebuye (26) kifungo cha miezi sita jela baada ya kupatikana na hatia ya kujifanya mtumishi wa Serikali wakati akijua kuwa ni uongo.
Batebuye ambaye ni mkazi wa Kigamboni, alikutwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili( MNH) iliyopo Upanga, akijifanya ni daktari wa binadamu wa hospitali hiyo, wakati akijua kuwa si kweli.
Hukumu hiyo imetolewa leo, Machi 13, 2025 na Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Scholastic Odoyo, baada ya mshtakiwa kukiri shitaka lake.
Kesi hiyo iliitwa mahakamani hapo kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa shitaka lake kwa mara ya kwanza, lakini aliposomewa alikiri shitaka hilo na ndipo Mahakama ilipomtia hatiani na kumuhukumu.
“Mshtakiwa umetiwa hatiani kama alivyoshtakiwa na mahakama hii inakuhukumu kifungo cha miezi sita gerezani, ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hizi” amesema Hakimu Odoyo.
Hata hivyo, kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, mshtakiwa aliomba apunguziwe adhabu kwa sababu ana familia inayomtegemea.
“Mheshimiwa hakimu, naomba mahakama yako unihurumie na inipunguzie adhabu, sitarudia tena na pia nina familia inayonitegemea” aliomba.
Awali, kabla ya kuhukumiwa, karani wa mahakama hiyo, Shabani Hamad alimsomewa mshtakiwa shitaka lake.
Amesema kuwa Batebuye alitenda kosa hilo Machi 11, 2025 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) iliyopo wilaya ya Ilala.
Siku hiyo saa 8:00 mchana katika hospitali hiyo, mshtakiwa alikamatwa na Ofisa Utawala wa Hospitali hiyo, aitwaye Ramadhani Bakari(45), akijifanya mtumishi wa Serikali wa hospitali hiyo.
Inaelezwa baada ya kukamatwa mshtakiwa alimueleza Bakari kuwa yeye ni daktari, wakati akijua kuwa ni uongo na kitendo ambacho ni kinyume cha sheria za Tanzania.