Bandari ya Tanga inavyotoa fursa ya ajira, ongezeko meli na mizigo

Tanga. Imeelezwa idadi ya meli zinazotumia bandari ya Tanga imeongezeka kutoka 118 hadi kufikia meli 307 kwa mwaka 2019 hadi 2025 baada ya uwekezaji uliofanyika wa kuongezwa kina na upanuzi wake.

Pia, bandari imetoa ajira za kudumu 320 kutoka 222 na vibarua 17,000 kutoka 6,000 hali ambayo imewezesha hata kuamsha uchumi wa wananchi wa Tanga kwenye shughuli zao za kiuchumi.

Akizungumza mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu inayofanya ziara ya siku mbili iliyoanza leo Alhamisi Machi 13, 2025 mkoani humo, Mkuu wa Mkoa huo Balozi Batilda Burian amesema uwekezaji wa Sh429.1 bilioni umezaa matunda kwenye  bandari hiyo na kubadilisha taswira ya Mkoa wa Tanga.

Amesema ukusanyaji wa mapato umeongezeka na fursa za ajira katika bandari hiyo huku muda wa kutoa mizigo ukiwa ni mchache zaidi kuliko bandari za jirani na Tanga.

“Zamani tulikuwa tunatumia matishari kwenda katikati ya bahari kupokea mizigo, waliokuwa wakitumia bandari ya Tanga ilibidi walipe malipo ya ziada kwa ajili ya kusafirisha mizigo yao kufika ufukweni,” amesema Batilda.

Amesema kupitia uwekezaji huo sasa tozo hizo hazipo, meli zinafika moja kwa moja kwenye fukwe ikiwemo za mizigo na abiria kupata huduma kwa haraka na kuongeza hadi pato la mkoa.

“Mapato pia yameongezeka, kabla ya uwekezaji mwaka 2019-20 tulikuwa tunapata Sh17.2 bilioni, baada ya uwekezaji tunapata zaidi ya Sh45.6 bilioni,” amesema.

Balozi Batilda anasema kuhusu shehena pia katika bandari hiyo imeongezeka kutoka tani laki 470,000 hadi tani zaidi ya 1.1 milioni baada ya ukarabati na bandari kuanza kufanya kazi.

“Hata idadi ya meli imeongezeka kutoka 118 hadi meli 307  zinatia nanga kwenye bandari hii ambayo pia imetoa ajira za kudumu 320 kutoka 222 na vibarua 17,000 kutoka 6,000,” amesema.

Kwa mujibu wa Batilda, muda wa kutoa mizigo kwenye bandari hiyo umepungua kutoka siku sita za awali hadi siku mbili hadi tatu.

Serikali imewekeza Sh429.1 bilioni katika ukarabati wa gati, kuongeza kina na kuboresha mazingira ya bandari ya Tanga kwa lengo la kutoa huduma bora zaidi kwa ukanda huo wa Kaskazini.

Mapema mwezi huu, Rais Samia Suluhu Hassan aliweka jiwe na msingi la uzinduzi wa mradi wa kuboresha Bandari ya Tanga akisema ameridhishwa na maboresho ya utendaji.

Mradi wa uboreshaji wa Bandari ya Tanga, Rais Samia alisema utekelezaji wake utagharimu Sh429.16 bilioni.

Amesema kazi hiyo si tu imeifufua bandari bali imeongeza ufanisi na sasa muda wa kushusha mizigo umepunguza kutoka siku tano hadi mbili.

“Nataka kurudisha hadhi ya Tanga, iwe Tanga ya viwanda Tanga yenye bandari kubwa lakini pia, Tanga ya uvuvi, ndicho ninachokifanya sasa na Mungu atujalie,” alisema.

Imeandikwa na Rajabu Athuman na Imani Makongoro

Related Posts