Baada ya kuajiriwa kwa zaidi ya miaka, 20 Rhoda Magoiga sasa anamiliki kampuni iliyoajiri zaidi ya watu 20 na vibarua 60 akionyesha mfano wa ukombozi wa wanawake kiuchumi.
“Matokeo niliyopata kwa miaka mitano sijawahi kuyapata kwa miaka Zaidi ya 20 niliyokuwa nimeajiriwa,” amesema Rhoda alipozungumza na Mwananchi hivi karibuni.
Rhoda aliyekuwa ameajiriwa na kampuni mojawapo ya pembejeo nchini, inayojishughulisha na biashara za mbolea na pembejeo za kilimo, aliona fursa na kuamua kuingia mwenyewe kwenye biashara hiyo.

“Mwaka 2019 nilianzisha jina la biashara na mwaka 2021 nilipoacha kazi nilisajili rasmi kampuni ya Mwana wa Afrika Investment Company Ltd, hivyo mimi ni mkurugenzi na mwanzilishi,” anasema.
Mbali na mbolea, kampuni yake pia inasambaza mbegu za mahindi, alizeti na kwa sasa imeingia ubia na kampuni za usambazaji wa viatilifu, huku pia ikilenga kujenga kiwanda cha mbolea za asili.
“Niliona nisiende mbali na kazi niliyokuwa nikiifanya, na ndio maana niliamua kujiajiri kwenye eneo hilihili la kilimo na hapo ndipo nimekuwa nikikutana na wadau walewale wa mbolea na wakulima walewale,” amesema.
Akisimulia safari yake ya mafanikio, Rhoda anasema tayari alikuwa na uzoefu wa biashara hiyo, hivyo akaamua kujitosa rasmi.
“Niliamua kuacha kazi baada ya kuona kipato hakitoshelezi, kwani nilikuwa na mahitaji makubwa kuliko mshahara ninaoupokea, sikuweza kujikimu kimaisha, kupeleka watoto shule na mengineyo.
“Kabla sijaacha kazi, nilianza na duka la kwanza Songea mkoani Ruvuma kwa mtaji wa Sh3 milioni, na baada ya kuacha kazi nikapata fedha kutokana na mafao niliyopata, nikaongezea mtaji nikafungua duka la pili eneo la Mapinga wilayani Bagamioyo Mkoa wa Pwani kwa mtaji wa Sh7 milioni,” amesema.

Safari moja huanzisha nyingine, hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Rhoda, kwani aliingia ubia na kampuni moja ya uzalishaji mbolea ya asili (organic fertilizer), huku baadhi ya kampuni zinazoagiza mbolea zikibisha hodi kutaka kufanya naye kazi.
“Mwaka 2022 nilipata kazi ya Serikali ya kusambazia mbolea nchini na hapo ndipo nilipofungua vituo vingi zaidi na kuajiri watu wengi zaidi,” amesema.
Baada ya mzunguko wa biashara yake kuongezeka, Rhoda amesema alipata mkopo kutoka moja ya benki nchini ili kukuza biashara hiyo.
Akizungumzia hatua inayofuata katika biashara yake, Rhoda anasema kwa sasa mtazamo ni kuwa na kiwanda chake cha kuzalisha mbolea za asili na kuzalisha chokaa mazao (agricultural lime).
Alidokeza kuwa kiwanda hicho tayari kinajengwa na kinatarajiwa kuanza kazi Mei mwaka huu, kitaajiri wafanyakazi 30.