Bugando kuanza upandikizaji figo mwaka huu

Mwanza. Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando imesema inatarajia kuanza kutoa huduma ya upandikizaji wa figo kwa wagonjwa wanaofanyiwa huduma ya usafishaji damu (Dialysis) mwaka huu.

Taarifa hiyo imetolewa leo Alhamisi, Machi 13, 2025, na Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji Bugando, Dk Alicia Masenga, kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Bugando, Dk Bahati Wajanga.

Dk Masenga amesema uamuzi huo unalenga kuboresha utoaji wa huduma na kukabiliana na changamoto ya ongezeko la wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo katika mikoa ya Kanda ya Ziwa ambayo inahudumiwa na hospitali hiyo.

Amesema tayari wataalamu kutoka Wizara ya Afya wamefika Bugando kufanya tathmini ya mazingira na kuridhishwa, huku akidokeza kinachosubiriwa ni kurejea kwa wataalamu wa upasuaji huo wanaohitimisha masomo nje ya nchi.

“Maandalizi ya kuanza upandikizaji wa figo kwa wagonjwa wenye matatizo ya figo yanaendelea vizuri. Mwaka huu, huduma hii ya upandikizaji figo itaanza kutolewa Bugando,” amesema Dk Masenga.

Kuanza kutolewa kwa matibabu hayo Bugando kutafanya idadi ya hospitali zinazotoa huduma hiyo kufikia nne, ikitanguliwa na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (Upanga na Mloganzila) ya Dar es Salaam na Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma.

Awali, Mkuu wa Kitengo cha Dialysis Bugando, Dk Said Kanenda, amesema maandalizi ya kuanza upandikizaji wa figo yamefikia asilimia 90.

Dk Kanenda amesema wastani wa wagonjwa 140 hupatiwa huduma ya usafishaji wa damu (dialysis) kila wiki, huku mgonjwa akitakiwa kulipia hadi Sh200,000 kila anapofanyiwa huduma hiyo, ambapo mgonjwa hutakiwa kufanyiwa angalau mara tatu kwa wiki.

Takwimu za Wizara ya Afya hadi mwaka jana zinaonyesha kuwa idadi ya watu wenye matatizo ya figo wanaopata huduma ya usafishaji damu (dialysis) iliongezeka kutoka 1,017 mwaka 2019 hadi 3,231 kufikia Desemba 2023.

Dk Kanenda ametaja baadhi ya visababishi vikuu vya magonjwa ya figo kuwa ni pamoja na shinikizo la damu, kisukari, na kukojoa protini, huku kukiwa na wanawake wanaokumbwa na tatizo la figo kufeli kutokana na kutokwa na damu nyingi na kifafa cha mimba wakati wa kujifungua.

“Kitengo chetu kinapata wastani wa wanawake watatu hadi sita kwa mwezi wanaohitajika kufanyiwa dialysis kutokana na changamoto zinazoibuka wakati wa kujifungua.”

“Ndiyo maana tunasisitiza wajawazito kuwahi hospitalini na kufuata ushauri wa madaktari wakati wote wa ujauzito, ikiwemo kutumia dawa za kuongeza damu,” amesema Dk Kanenda.

Kuhusu uchunguzi wa hiari, Dk Kanenda amesema siku moja kabla ya maadhimisho hayo, Bugando ilifanya uchunguzi wa siku moja wa viashiria vya matatizo ya figo kwa wakazi wa Mwanza 178, ambapo kati yao 56 sawa na asilimia 31 walikutwa na tatizo la shinikizo la damu.

Amesema wanane kati yao, sawa na asilimia 4.5, walikuwa na tatizo la kisukari, 17 walikutwa na maambukizi ya bakteria kwenye njia ya mkojo, huku 20 wakipitisha protini kwenye mkojo wao, jambo linaloashiria kuwa wako hatarini kuugua magonjwa ya figo.

“Shinikizo la damu, kisukari, na kusitisha protini kwenye mkojo ni matatizo makubwa. Maana yake ni kwamba machujio ya figo hayafanyi kazi vizuri, na hivyo mtu anaweza kukumbwa na hitilafu kubwa inayoweza kusababisha figo kufeli,” amesema.

Mgonjwa anayepatiwa huduma ya dialysis, Clement John, ameeleza kufurahishwa na mpango wa upandikizaji wa figo, huku akisema utaokoa maisha ya mamia ya watu wanaohudhuria kupata huduma ya kusafishwa figo kila wiki.

“Bugando kupandikiza figo ni jambo zuri sana. Mimi nimeshapata mtu wa kunipatia figo, lakini changamoto iliyopo ni sehemu ya kupatiwa matibabu. Najua huduma hii inapatikana Dar es Salaam na Hospitali ya Benjamin Mkapa, lakini gharama za kukaa huko zinaniwia vigumu,” amesema John.

Mgonjwa mwingine, Elvina Vitalis, ameishukuru Serikali na Bugando kwa kusogeza huduma ya dialysis katika kanda hiyo, huku akisema anaamini kuwa kuanza kwa huduma ya matibabu ya upandikizaji wa figo huenda yakamuondolea maumivu ya kusafisha damu kila wiki.

Kwa mujibu wa wataalamu tabia hatarishi zinazoweza kuchochea mtu kukumbwa na magonjwa ya figo ni pamoja na uzito uliopindukia, uvutaji wa sigara, matumizi ya vyakula vyenye sumu, hususan viuatilifu kwenye mboga na matunda, na kutofanya mazoezi (tabia bwete).

Related Posts