Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amewataka wakazi wa mkoa huo kutokubali kufanya biashara na taasisi yoyote ya Serikali bila kuwa na mkataba na nyaraka rasmi za makabidhiano ya huduma iliyotolewa.
Amesema hatua hiyo itaepusha migogoro kati ya wananchi na taasisi za Serikali ambazo wanafanya nazo biashara, kama ilivyotokea kwa Martha Lazi, ambaye alifanya kazi ya Hospitali ya Amana na sasa wanasumbuana kwenye malipo.
Hata hivyo, alipotafutwa Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Amana, Dk Bryceson Kiwelu kuzungumzia suala hilo alisema kwa kuwa Mkuu wa Mkoa ameshazungumzia na kutoa maelekezo hana cha kuongeza.
Msingi wa kauli ya Dk Kiwelu ni maelekezo yaliyotolewa na Chalamila kuhusu kumalizana na Martha Lazi.
Akizungumza baada ya kukutana na Martha, Chalamila amesema ni kosa kufanya biashara au kutoa huduma yoyote kwa Serikali bila kuwa na nyaraka na kufuata mchakato stahiki.
“Tumeshamuelekeza mganga mkuu alishughulikie suala hili kwa haraka ili ulipwe kile unachostahili, lakini kitu cha pili usije ukakubali kufanya biashara na Serikali pasipo nyaraka. Mtu na mtu huwa wanaweza kukopana hela, lakini kwa Serikali hata kama ni Sh500 inatoka kwa nyaraka, umefanya kazi na Serikali lazima upewe nyaraka.
“Tena siku hizi tunaanza na mchakato wa kutangaza zabuni wanakuja wengi atashinda mmoja, cha pili tutamtathimini aliyeshinda kuangalia uwezo wake halafu unafuata mkataba na malipo yote yanawasilishwa kwa njia ya akaunti. Bidhaa yoyote inayoletwa Serikali inapaswa kuandikwa kwenye reja kuthibitisha kuwa tumepokea.
Hilo limeelezwa pia na wakili Joyce Komanya aliyesisitiza kuwa kuna umuhimu mkubwa wa watu kuwa na mkataba wanapoingia kwenye biashara.
“Mkataba kisheria unabeba uthibitisho wa makubaliano baina ya pande mbili na unalinda pande zote kisheria. Maneno pekee hayawezi kuleta uzito wa kile kinachoelezwa kama mambo yamekwenda kombo kati ya pande hizo.
Mkataba ni lazima uwe wa maandishi na uwe na mashahidi. Kwa tukio la huyu mama angekuwa na mkataba angeweza kuishtaki hospitali, mahakama haiamini katika maneno linapokuja suala la biashara,”amesema na kuongeza
“Pia, watu wajue mikataba ina ukomo, mingi inakuwa ndani ya miaka mitatu ikihusisha utekelezaji, malipo na muda wa kufungua kesi ikiwa kutakuwa na uvunjaji au ukiukwaji wa masharti ya mkataba, ikizidi muda huo hata mahakama inaweza isisikilize,”.
Kupitia mitandao ya kijamii mama huyu alilalamika kuzungushwa malipo yake baada ya kufanya biashara na Hospitali ya rufaa ya Amana, hata hivyo ilikuja kubainisha kuwa hakuwa na nyaraka wala mikataba inayothibitisha kufanyika kwa biashara hiyo.
Kupitia video hiyo Martha ambaye ni fundi wa cherehani ameeleza kuwa mwaka 2017 alipata kazi ya kushona nguo kwa ajili ya kuvaliwa chumba cha upasuaji zikiwa na thamani ya Sh3 milioni.
“Baada ya kukabidhi zile nguo nikaanza kufuatilia malipo yangu, mambo yalienda vizuri hadi nikafikia hatua ya kulipwa, lakini kabla sijalipwa ikaingia Uviko-19, nikaambiwa sitaweza kulipwa hadi hali itakapokaa sawa.
“Nilielewa kwa kipindi kile mambo mengi yalisimama, hivyo nikarudi nyumbani maisha yakaendelea hadi pale ugonjwa ulivyoisha ndipo nikarudi tena kufuatilia malipo yangu,” amesema Martha.
Amesema awamu hii alipoenda kufuatilia malipo yake akapewa kazi nyingine ya kushona pazia kwa ajili ya hospitali hiyo, ili aunganishiwe na malipo ya awali.
“Nilipopewa kazi nyingine ili malipo yaunganishwe sikuwa na wasiwasi nilitumia vyanzo vyangu kupata fedha za vitambaa nikashona na kwenda kuwakabidhi yale mapazia,” amesema Martha.
Baada ya kukamilisha kazi hiyo na kuanza mchakato wa malipo ikaingia awamu ya pili ya Uviko-19 ndipo taratibu za ulipaji zilipositishwa kwa mara nyingine tena, akiwa anadai jumla ya Sh5.48 milioni zikihusisha sare za chumba cha upasuaji na mapazia ya hospitali.
Wakati mchakato wa kukusanya nyaraka kwa ajili ya malipo hayo ukiendelea Chalamila amempatia Martha Sh2 milioni kama sehemu ya mchango wake binafsi kwenye biashara ya mama huyo mjane.
Akizungumza na Mwananchi leo Machi 13,2025 Martha amesema ameridhishwa na hatua iliyochukuliwa na mkuu wa mkoa kuingilia kati sakata hilo kwa sababu alishapoteza matumaini.
Kuhusu nyaraka amesema anazo nyaraka mbili ambazo ameziwasilisha kwenye uongozi wa hospitali hiyo wakiendelea kuzifanyia kazi na endapo watajiridhisha kuwa anastahili malipo hayo atakuwa tayari kuyapokea.
“Tumekaa kikao na wamepitia vifungu vinavyohusisha utoaji wa zabuni katika Hospitali ya Amana, nimewasilisha mkataba wa awali ambao niliingia nao nilipowashonea nguo na nikapeleka ankara ya madai ya malipo (invoice) nilipopeleka mapazia. Nasubiri wao waamue wakiona nastahili kulipwa naamini nitalipwa,”amesema Martha.