Simba SC kesho Ijumaa itaingia uwanjani kukabiliana na Dodoma Jiji huku ikielezwa itaikosa huduma ya kipa wake namba moja, Moussa Camara na beki tegemeo, Che Fondoh Malone.
Nyota hao wanatarajiwa kukosekana katika mchezo huo wa Ligi Kuu Bara utakaochezwa Uwanja wa KMC Complex, Dar kutokana na kusumbuliwa na majeraha waliyoyapata Februari 24, 2025 katika sare ya mabao 2-2 dhidi ya Azam.
Kukosekana kwa Camara, kunaendelea kutoa nafasi kwa Ally Salim kukaa langoni kama ilivyokuwa mechi mbili zilizopita dhidi ya Coastal Union (Ligi Kuu) na TMA Stars (Kombe la FA) huku Che Malone nafasi yake ikichukuliwa na Chamou Karaboue.
Kocha Msaidizi wa Simba, Seleman Matola, amezungumzia hali ya kikosi chake kuelekea mchezo huo utakaofanyika kuanzia saa 10:00 jioni akisema Camara na Che Malone ndiyo watakosekana lakini wengine afya zao zipo vizuri.
“Kwa mchezo wa kesho tutaendelea kumkosa Che Malone na Camara ambao ni majeruhi ingawa Camara ameanza mazoezi na tunatarajia mechi zijazo atakuwepo,” amesema Matola.
Kuhusu namna walivyojiandaa kukabiliana na Dodoma Jiji, Matola amesema: “Tumejiandaa kucheza na Dodoma, haiwezi kuwa mechi rahisi hasa ukizingatia huu ni mzunguko wa pili. Dodoma ina mwalimu mzuri, Mecky (Maxime) ni kocha anayependa ushindani kwani hata mechi ya kwanza dhidi yao haikuwa rahisi.
“Tunafahamu namna mchezo utakavyokuwa mgumu, hivyo tumejiandaa kuona namna ya kupata matokeo mazuri.”
Simba inayoshika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 54 ikizidiwa nne na vinara Yanga, inakutana na Dodoma Jiji iliyopo nafasi ya nane huku mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Jamhuri, Dodoma, Simba ikishinda 1-0 kwa bao la mkwaju wa penalti lililofungwa na Jean Charles Ahoua dakika ya 63.
Rekodi zinaonyesha Simba imekuwa wababe mbele ya Dodoma Jiji tangu zianze kukutana kwenye ligi msimu wa 2021-2022.
Katika mechi tisa walizokutana, Simba imeshinda zote, hivyo mchezo wa kesho Dodoma Jiji ina kazi kubwa ya kufanya kufuta unyonge na kuandika rekodi mpya ya ushindi.
Hata hivyo, Dodoma Jiji ina mlima mrefu wa kuupanda inapokwenda kukutana na Simba kwani mbali na kushindwa kupata ushindi, pia haijafuga bao lolote katika mechi saba zilizopita dhidi ya Simba. Kwa jumla imefunga mabao mawili pekee iliyoyapata mechi mbili za kwanza msimu wa 2021-2022 ilipofungwa 1-2 nyumbani na 3-1 ugenini, huku ikiruhusu nyavu zao kutikiswa mara 16.
Hata hivyo, Dodoma Jiji inatambua umuhimu wa pointi tatu za mchezo huu kutokana na nafasi iliyopo ikibakiwa na mechi nane.
Beki wa Dodoma Jiji ambaye amewahi kuitumikia Simba, Abdi Banda, amesema: “Hakuna kingine tunachowaahidi Wana Dodoma zaidi ya kwenda kupambana.
“Utakuwa mchezo mzuri kwa sababu kila timu inataka pointi tatu, sisi zaidi tunazitaka pointi tatu kutokana na namna tulivyoachana pointi na wale tunaokimbizana nao kwenye msimamo.
“Mchezo wa Dodoma na Simba siku zote unakuwa mgumu, sisi wachezaji tunalitambua hilo, hivyo tunafahamu tunakwenda kucheza mchezo wa aina gani kulinganisha na nafasi tuliyopo.”
Naye Kocha Mkuu wa Dodoma Jiji, Mecky Maxime, alisema: “Ligi ni ngumu, Simba wanapambania ubingwa na sisi tunataka kukaa sehemu nzuri, hiyo ndiyo sababu itafanya mechi kuwa ngumu.”