KOCHA wa Simba, Fadlu Davids, amepongeza juhudi za wachezaji wa timu hiyo baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya TMA Stars na kutinga 16 Bora ya Kombe la Shirikisho, lakini akifichua kuhusu Dabi ya Kariakoo iliyoota mbawa saa chache kabla ya kupigwa kwake, akisema Simba waliiitaka sana.
Fadlu alisema kuahirishwa kwa dabi kulifanya wachezaji kushuka morali, lakini alifanya kazi ya ziada kuwarejeshea morali kwa kuwajenga kisaikolojia na anashukuru kuona wamepata matokeo mazuri katika mechi hiyo ya Kombe la Shirikisho, moja ya makombe matatu yanayowindwa na timu hiyo.
Ushindi huo wa juzi umeifanya Simba sasa kukutana tena na timu ya Ligi ya Championship kama ilivyokuwa, TMA Stars katika hatua ya 16 bora kwani itavaana na BigMan (zamani Mwadui FC).
Katika mchezo huo uliochezwa juzi, Jumanne Uwanja wa KMC Complex, Simba ilianza kwa kasi, ikimiliki mpira na kutengeneza nafasi nyingi za kufunga. Licha ya upinzani wa TMA, Simba ilipachika mabao yake kupitia kwa Valentino Nouma, Sixtus Sabilo (alijifunga) na Leonel Ateba ambaye alipoteza nafasi nyingi za wazi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Fadlu alizungumzia changamoto ya kuwarudisha wachezaji katika kiwango sahihi baada ya kuahirishwa kwa mechi ya watani wa jadi dhidi ya Yanga siku chache zilizopita.
“Ilikuwa changamoto kubwa, hasa baada ya kujiandaa kwa mchezo wa watani wa jadi kisha kutochezwa, halafu tena kuwahamasisha kurejea katika mchezo huu na kupata matokeo mazuri,” alisema Fadlu.
Kocha huyo alisem kuahirishwa kwa dabi ambayo wachezaji walikuwa wakiitaka sana, iliathiri maandalizi yao kwa kiasi fulani, lakini anashukuru kuona wachezaji wake wakirejea na ushindi.
“Unapokuwa umejiandaa kwa mechi kubwa kama ile halafu haichezwi, inakuwa vigumu kisaikolojia kujiandaa kwa mchezo mwingine haraka. Wachezaji walilazimika kujitoa zaidi ili kuhakikisha wanapita salama kwenye mchezo huu,” aliongeza.
Hata hivyo, Fadlu aliwapongeza wapinzani wao, TMA, kwa kuonyesha upinzani wa hali ya juu licha ya kushindwa kufurukuta mbele yao.
“Bila shaka, hakuna mchezo rahisi kwenye mashindano haya. TMA walituweka kwenye presha kwa nyakati fulani, lakini tulijitahidi kutoanguka na tukaendelea kucheza kwa mtindo wetu,” alisema.
Baada ya Simba kuwa mbele kwa mabao 2-0, Fadlu aliamua kumpumzisha beki wake wa kati Abdulrazak Hamza na nafasi yake kuingia kiungo mkabaji, Yusuph Kagoma. Wakati ikisubiriwa kuona nini kitatokea mwanzoni mwa kipindi cha pili, Kagoma akaonekana kushuka eneo la chini na kucheza sambamba na Chamou Karaboue.
Licha ya kwamba haijazoeleka kuona Kagoma akicheza nafasi ya beki wa kati, alionyesha utulivu mkubwa katika dakika 45 za kipindi cha pili. Alikuwa makini katika kuusoma mchezo, huku akitumia uwezo wake wa kupiga pasi kwa usahihi na kupangilia mashambulizi kutoka nyuma.
Fadlu alisema uamuzi wa kumchezesha Kagoma eneo hilo ulitokana na hitaji la kufanya majaribio ya mifumo tofauti, huku akisisitiza kuwa mabadiliko hayo yanaweza kusaidia katika mechi zijazo.
“Katika dakika za mwisho, tulimaliza mchezo tukiwa na mabeki watatu, lakini hakuna hata mmoja aliyekuwa beki wa kati halisi. Hii ni moja ya mbinu tunazofanyia kazi kwa ajili ya mechi zijazo,” alisema Fadlu.
Kocha huyo alifurahishwa na namna Kagoma alivyojibu vyema changamoto hiyo. “Kagoma ni mchezaji mwenye akili ya mchezo. Alielewa majukumu yake haraka na alifanya kazi nzuri kwenye nafasi ya beki wa kati, jambo ambalo linaongeza chaguo kwetu kama timu,” aliongeza.
Licha ya kushinda kwa idadi kubwa ya mabao, kocha huyo alikiri kuwa bado kuna maeneo ambayo wanahitaji kuyaboresha. “Hatupaswi kuridhika na matokeo haya pekee. Lazima tuendelee kufanya kazi kwa bidii ili kuwa bora zaidi, hasa tunapokaribia mechi za uamuzi,” alisema.