KIKOSI cha Yanga jana kilikuwa uwanjani kuvaana na Coastal Union katika mechi ya hatua ya 32 Bora ya Kombe la Shirikisho, lakini mapema kocha mkuu wa timu hiyo, Miloud Hamdi aliweka wazi silaha tatu zinazombeba katika mechi mbalimbali tangu ajiunge na vijana wa Jangwani.
Hamdi alijiunga na Yanga Februari 5 mwaka huu, amewataja viungo wakabaji wa timu hiyo, Khalid Aucho, Duke Abuya na Mudathir Yahya kuwa ndio injini wa timu hiyo na anafurahia namna walivyo katika ubora na kuwa msaada mkubwa kwa timu inapokuwa uwanjani kitu anachojivunia kuwa nao.
Aucho (31) anayeitumikia Yanga kwa msimu nne sasa, amekuwa mmoja kati ya viungo wachache ambao nafasi zao zimeshindwa kupata mrithi licha ya sajili nyingi kupita klabuni hapo, huku akiwa chaguo la kwanza la kiungo mkabaji kuanzia kwa makocha Nasreddine Nabi, Miguel Gamondi, Sead Ramovic hadi kwa Hamdi.
Katika mechi 22 ambazo Yanga imecheza hadi sasa, amekosa michezo mitatu tu, huku katika mabao 58 amechangia moja na kocha Hamdi anamtaja kama roho ya timu licha ya kikosi hicho kuwa na mastaa wanaoifanya iwe tishio mbele ya wapinzani.
Akizungumza na Mwanaspoti, kocha Hamdi alisema kati ya mastaa anaojivunia Yanga Aucho ni miongoni mwao, kwani amekuwa muhimili mkubwa kuiunganisha timu.
Hamdi alisema, Aucho ni kiungo bora kuwahi kufanya naye kazi na ana uwezo mkubwa wa kutengeneza uwiano mzuri eneo la kati na ulinzi.
“Aucho akiwa eneo la kati anajua kutengeneza uwiano bora kwa walinzi na kutoka kati kwenda mbele, kuwa na kiungo kama huyo ni kama bahati kubwa kwenye kikosi changu. Kama ningekuwa kocha wa timu pinzani wa Yanga, ningekuwa napata tabu kujua namna gani naweza kumfanya Mganda huyo kutocheza kwa utulivu,” alisema Hamdi na kuongeza;
“Ubora wa Aucho pia umerahisisha viungo wa juu kucheza kwa kiwango kizuri, kwa sababu ya mchango mkubwa alionao pale kati unaowapa wepesi wachezaji wenzake na tabu kwa wapinzani.”
Hamdi pia aliwataja Mudathir Yahya, ambaye huu ni msimu wa tatu ndani ya Yanga, na Abuya huu ukiwa msimu wa kwanza akitokea Singida Black Stars.
Aliwapongeza viungo hao, huku akisema, wamekuwa wakifanya kazi kubwa na nzuri ya kumsaidia Aucho kwenye eneo hilo.
“Nisipowapongeza hawa viungo wawili nitakuwa nakosea, kwani ni wachezaji wanaoshirikiana vizuri na Aucho, hawa ni watu wanaojua kufanya kilichowaleta.”
Kutajwa kwa nyota hao watatu ambao Hamdi anasema ndio roho ya timu, ina maana waliosalia katika eneo hilo akiwamo Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Jonas Mkude, Shekhan Ibrahim na Aziz Andambwile wafanye kazi ya ziada ili kumshawishi kocha huyo raia wa Ufaransa mwenye asili ya Algeria, hasa wakati huu dirisha kubwa la usajili likitarajiwa kufunguliwa miezi michache ijayo.